Wiki iliyopita nilihitimisha makala hii kwa kusema kuanzisha biashara ni sawa na kujenga nyumba. Nyumba iliyo bora inapaswa kuwa na ramani. Na si ramani tu, bali hesabu za vifaa vitakavyotumika. Hii itakuwezesha kujua utatumia saruji mifuko mingapi, nondo ngapi, mabati mangapi, kokoto kiasi gani, mchanga, maji, gharama za ufundi na mambo mengine.

Sitanii, katika sehemu ya kwanza nilikwambia mpendwa msomaji, mfanyabiashara au mfanyabiashara mtarajiwa kuwa hatua ya kwanza katika kuanzisha biashara ni kuwa na wazo. Hili nililieleza vema wiki iliyopita na aina ya maswali unayopaswa kujiuliza kabla ya kuanzisha biashara.

Hatua ya pili ni mwendelezo wa nini kinafuata baada ya kupata wazo la biashara. Ni lazima ufahamu ENEO LA KUFANYIA BIASHARA. Jambo hili kuna watu hawalitilii maanani wakati wanaanzisha biashara na wanaishia kupata hasara kubwa. Eneo la kufanyia biashara ni sehemu muhimu katika ufatifi wa kuanzisha biashara yako.

Nitatoa mfano niweze kueleweka. Mfano huu unakwenda mbali zaidi na kugusia suala nililolisema wiki iliyopita la muda wa kufanya biashara. Nianze na hili la eneo. Usipofanya utafiti, unaweza kufungua biashara kwa mtaji mkubwa, ila ukakosa wateja na ukaishia kuifunga biashara.

Kwa mfano, unaweza kupata chumba kizuri na kikubwa cha kufanyia biashara, lakini inategemea chumba hicho kipo wapi na ni biashara ya aina gani unayotaka kufanya kulingana na wazo lako la biashara. Ukienda karibu na shule ya msingi iliyojengwa na kukamilika au sekondari au chuo kikuu ukafungua duka la saruji na mabati, naamini biashara hii utaifunga ndani ya muda mfupi.

Sitanii, matarajio halali na mikakati katika biashara inatarajia aina ya wateja na mahitaji ya wateja. Karibu na shule au chuo, matarajio halali ni kwamba utafungua biashara kama ya kuuza madaftari, kalamu, kurudufisha nakala na ikiwezekana kuuza chakula. Siku hizi kwa mji kama wa Dodoma wataalamu wameongeza bidhaa mpya jirani na vyuo; kuuza vinywaji baridi na vikali baada ya wanafunzi kupata ‘boom’.

Duka la vifaa vya ujenzi kama saruji, mabati, mchanga, nondo na rangi, unapaswa kulifungua sehemu ambayo kuna makazi mapya. Kwa mfano sasa hivi serikali inajenga Jiji la Dodoma, vifaa vya ujenzi kwa mtu mwenye mtaji ndiyo muda mwafaka wa kufungua duka la aina hiyo hapo Dodoma.

Sitanii, unaweza kuwa na biashara sahihi kabisa, inayohitajiwa na wateja wako, lakini lazima ufahamu muda wa kufungua biashara yako. Kwa mfano, kama unauza karanga sitarajii ufike na kapu la kuuza karanga katika shule ya msingi au sekondari wakati muda wa mapumziko umekwisha na mwalimu wa zamu ameshika kiboko mkononi anafukuza wanafunzi kurejea madarasani!

Ikiwa mapumziko ni saa 04:00 hadi saa 04:30 asubuhi, wewe kama muuza karanga unapaswa kufika pale angalau saa 03:30 asubuhi upange eneo lako safi tayari kuhudumia wateja wako watakapokwenda mapumziko. Biashara ya karanga unaweza kuilinganisha na ya baa. Ukifungua baa saa 12 asubuhi na mwenzako akafungua saa 12 jioni, naamini unafahamu nani atauza zaidi.

Nitoe mfano mwingine. Sikukuu ya mwaka mpya, Eid au Noel, kwa mfanyabiashara anayefahamu anachokifanya, anafanya maandalizi makubwa ya kuuza nguo, vyakula… Januari, maduka yanauza madaftari na vitabu. Utakuwa wa ajabu mno, kufungua baa karibu na kanisa la walokole au msikiti, ukitarajia kuwa waumini wakimaliza ibada watapita kwenye baa yako kukata kiu.

Sitanii, nimesema makala hii nalenga mwisho wa siku iwe kitabu cha jinsi ya kufanya biashara Tanzania. Hadi wakati nahitimisha makala hii, nitaangazia biashara ndogo ndogo, biashara za kitaifa na biashara za kimataifa.

Baada ya kuwa umepata wazo la biashara na umetafiti na kufahamu eneo unalotaka kufanyia biashara, kwa maana ya kuwafahamu wateja wako, wiki ijayo nitazungumzia hatua ya tatu katika mchakato wa kufanya biashara, ambayo ni uchaguzi wa utaratibu unaotaka kuutumia kufanya biashara. Ukiishafikia hatua hiyo, nitaeleza utakavyopaswa kufanya uchaguzi iwapo uwe na andiko la mradi au la kulingana na ukubwa wa biashara husika.

Wiki ijayo nitazungumzia iwapo utafanya biashara kama mtu binafsi, kwa kutumia jina la biashara, kampuni yenye hisa na ukomo au kampuni yenye hisa zisizo na ukomo. Nawashukuru nyote mlionipigia simu na mlioahidi kuwa wa kwanza kununua kitabu hiki. Tukutane wiki ijayo kupitia safu hii ya SITANII.

2040 Total Views 1 Views Today
||||| 1 I Like It! |||||
Sambaza!