Wiki iliyopita nilieleza sehemu ya pili ya taratibu za kuanzisha biashara kwa mtu yeyote mwenye nia ya kufanya hivyo hapa Tanzania. Nimeandika mwendelezo wa hatua ya kwanza ambayo ni ‘wazo la biashara’ na nikagusia hatua ya pili ambayo ni ‘eneo la kufanyia biashara’. Jambo la tatu katika kuanzisha biashara unapaswa kuamua MFUMO WA KUFANYA BIASHARA yako.

Sitanii, mfumo wa kufanya biashara yako unapoamua ni upi unakuwa umeweka dira ya kudumu na kuanzia hapo utaweza kuandika Mpango wa Biashara (Business Plan), ambao nitaueleza katika makala zijazo pia na kuendelea kwa nia ya kuwa na biashara endelevu.

Mfumo wa kufanya biashara namaanisha moja kati ya ifuatayo; kufanya biashara kama mtu binafsi, kusajili jina la biashara, kufungua kampuni yenye ukomo kwa hisa (limited company by shares) au kufungua kampuni isiyo na ukomo wa hisa (unlimited Company by shares).

Ukiishafanya uamuzi ni mfumo upi unapaswa kuutumia (na hii inategemea ukubwa wa biashara), utaanza kutafuta aina ya usajili unaopaswa kuwa nao, leseni au kiwango cha kodi unachopaswa kulipa.

Ikiwa umeamua kufanya biashara kama mtu binafsi (utaratibu unaotumiwa na Watanzania wengi kwa sasa), hapa utafanya hatua zifuatazo. Utalazimika kwenda katika eneo la kufanyia biashara, ufanye maandalizi binafsi kama unajenga chumba au unaweka kontena. Pia utatakiwa kuangalia kama si chumba, basi unajenga banda na kuweka mazingira ya kufanyia biashara. Utaweka mfumo wa ulinzi wa biashara yako.

Baada ya kuwa umeandaa eneo la kufanyia biashara, ni vema ukatafuta bidhaa unazotaka kuuza ukaingiza kwenye banda au duka lako. Kumbuka katika hatua hii utapaswa kuwa umelipa kodi kwa mwenye eneo kama unakodisha au umenunua eneo unalotaka kufanyia biashara liwe lako.

Sitanii, kwa nia ya ujirani mwema, inakuwa vema unapokuwa umefikia hatua hii ya kuweka bidhaa kwenye duka au eneo lako la biashara, uufahamishe uongozi wa mtaa au kijiji unakofanyia biashara yako wakutambue na waitambue aina ya biashara unayofanya (ni lazima biashara yako iwe halali).

Taarifa kwa uongozi wa mtaa au kijiji unapofanyia biashara yako ifahamike kuwa si ya kulipishwa kodi. Baada ya kutoa taarifa na ikiwezekana ukaijaribu biashara yako kwa muda angalau wa mwezi mmoja ukafahamu mzunguko wa awali wa biashara unayoanza kuifanya, litakuwa jambo jema.

Nasema ufungue na kuendesha biashara kwa angalau mwezi mmoja kutokana na uzoefu. Uzoefu ninaouzungumzia, yaliwahi kunikuta mimi wakati naanzisha biashara ya kwanza. Nilikwenda hatua nitakayokushauri si muda mrefu, kumbe ukienda huko wanajua tayari biashara inafanya kazi, hivyo unakadiriwa kodi.

Kumbuka hii nazungumzia biashara unayofanya kama mtu binafsi, isiyo kubwa. Huwezi kufungua kituo cha kuuzia mafuta chenye mtaji wa hadi Sh milioni 400 bila kupata vibali husika ukasema unajaribu kwanza, hii nazungumzia biashara zinazohusiana na uchuuzi au vibanda vya aina mbalimbali.

Baada ya biashara yako kuwa tayari, kama unafanya kama mtu binafsi, ukafahamu kwa siku unauza shilingi ngapi litakuwa jambo jema. Nasema hivi, maana niliwahi kulipishwa kodi kwa miezi mitatu kabla ya kuanza biashara, kwa sababu tu nilikwenda Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na niliyezungumza naye akanikadiria kodi.

Kuna takwa la msingi katika kupata leseni ya biashara kutoka kwenye halmashauri. Takwa hili ni la kuwa na Uthibitisho wa kuwa Mlipakodi. Wakati unaandaa eneo la biashara ni vema pia ukaenda TRA ukapata Namba ya Mlipakodi (TIN). Namba hii ndiyo itatumika mbele ya safari kukupatia uthibitisho wa kuwa wewe ni mlipakodi na umelipa kodi (Tax Clearance).

Sitanii, bila Tax Clearance huwezi kupata leseni. Hii Tax Clearance utaipata kwa kwenda TRA baada ya kufahamu kwa siku unauza shilingi ngapi. Utafanyiwa makadirio ya kodi (presumptive tax). Makadirio haya yatagawanywa kwa vipindi vinne, hivyo utahitajika kulipa robo ya ulichokadiriwa ndani ya kila miezi mitatu, kwa maana Januari – Machi, Aprili – Juni, Julai – Septemba na Oktoba – Desemba.

Robo ya kwanza ya mwaka itakwenda sambamba na asilimia 10 ya malipo ya kodi ya pango la sehemu unapofanyia biashara. Kumbuka mwanzo nilikwambia utapaswa kuufahamisha uongozi wa kijiji au mtaa unakofanyia biashara uamuzi wako wa kufanya biashara katika eneo lao la utawala.

Kodi yako ya pango itabidi kuthibitishwa na uongozi wa Serikali ya Mtaa au Kijiji, na huo ndiyo utakuwa msingi wa TRA kukutambua kuwa ni kweli upo katika eneo unalolitaja na unafanya biashara katika eneo hilo.

Je, unafahamu taratibu zikoje ukifika TRA hadi unakadiriwa kiwango cha kodi utakayolipa kwa mwaka? Je, unafahamu ukiishalipa hayo malipo ya TRA ni ofisi ipi nyingine unapaswa kwenda kupata leseni ya biashara? Usiikose JAMHURI wiki ijayo uweze kusoma sehemu ya 4 ya makala hii ambayo baadaye itajumuishwa na kuchapishwa kama kitabu.

Please follow and like us:
Pin Share