Wiki iliyopita nilihitimisha makala hii kwa aya hii: “Je, unafahamu taratibu zikoje ukifika TRA hadi unakadiriwa kiwango cha kodi utakayolipa kwa mwaka? Je, unafahamu ukiishalipa hayo malipo ya TRA ni ofisi ipi nyingine unapaswa kwenda kupata leseni ya biashara? Usiikose JAMHURI wiki ijayo uweze kusoma sehemu ya 4 ya makala hii ambayo baadaye itajumuishwa na kuchapishwa kama kitabu.”

Sitanii, ndani ya wiki iliyopita yametokea mambo makuu mawili; kifo cha Ruge Mutahaba na Edward Lowassa kurejea CCM. Nimeshindwa kwenda Bukoba kumzika Ruge kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wangu. Nimemteua Katibu wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Neville Meena, aliwakilishe Jukwaa. Nawapa pole familia ya Clouds, familia ya Prof. Mutahaba, familia ya waandishi wa habari nchini na Watanzania kwa ujumla.

Ruge alikuwa mtu wa aina yake. Nina muda mrefu sijaona mazishi mazito kama ya Ruge. Wapo walioyalinganisha na ya Mwalimu Julius Nyerere. Ruge anazidi kutufundisha jambo, kuwa tuishi na watu vizuri. Tukifanya hivyo, miili yetu haitatafutwa makaburini. Tutaendelea kuishi vichwani mwa watu baada ya vifo vyetu. Raha ya milele umpe Ruge ee Bwana, na Mwanga wa milele umwangazie.

Suala la pili ni hili la Lowassa kuhamia CCM. Hadi mwaka 2015 ndani ya CCM walikuwapo wawili hawa. Lowassa na Rais John Magufuli. Historia ya utendaji wao iliwapa la kuonyesha mbele ya macho ya wananchi. Ni bahati wote waligombea urais. Waliwaeleza wananchi walitaka kuifanyia nini Tanzania. Fursa imepatikana ya wawili hawa kuunganisha mawazo.

Sitanii, kuleta mabadiliko katika nchi si lazima uwe rais au waziri mkuu. Kwa wanaosoma historia ya dunia hii warejee mwaka 1979 kilichotokea China. Mwanasiasa wa kawaida, Deng Xiaoping, alianzisha mfumo wa “Nchi Moja, Mifumo Miwili.” Mfumo huu umeipatia China utajiri wa kutisha. Hakuwa rais huyu, bali alishauri na mawazo yake yakakubaliwa. Naamini CCM na Rais Magufuli watasikilizana na Lowassa.

Ukiniuliza mimi kutoka kwenye sakafu ya moyo wangu nimechoka kusikia Tanzania ikiitwa nchi maskini kwa rasilimali zote tulizonazo. Haiwezekani sisi madini yote, bahari, bandari, maziwa, misitu, njia kuu za usafirishaji, viwanja vya ndege, Watanzania wenye akili timamu, halafu tuendelee kukubali sifa ya umaskini. Nasema hapana. Naamini Lowassa na Magufuli wakisikilizana, tukaacha siasa za kutafuta mchawi, nchi yetu itaondoka hapa tulipo.

Sitanii, ni kwa bahati mbaya nchi hii imeanzisha utamaduni wa baadhi ya watu kumgombanisha kila rais aliyeko madarakani na baadhi ya wanasiasa wachache. Kwa kufanya hivyo, wanaona wanapata fursa ya kuwa karibu na rais, kumbe wanamchelewesha katika kufanya uamuzi wa maana, wenye kuleta maendeleo, anabaki kugombana na watu. Imetokea hivyo mwaka 2000, 2010 na ilielekea kuwa hivyo mwaka 2015. Muda umefika, tujenge nchi, tuache ugomvi wa kisiasa.

Sitanii, leo makala yangu imechepuka kwa kiasi kikubwa. Ila naomba kukurejesha na itaendelea wiki ijayo. Kwamba ukifika TRA unaonana na ofisa wa TRA anayekadiria mapato (ikiwa unafanya biashara kama mtu binafsi). Pale atakuhoji unafanya biashara ya aina gani? Unaifanyia wapi? Mtaji wako ni kiasi gani? Kwa siku unauza shilingi ngapi? Na maswali mengine mengi.

Katika hatua hii ndipo nimepata malalamiko mengi. Baadhi ya watu wanashindwa kuelewa maswali wanayoulizwa yanalenga nini mwisho wa siku. Anajikuta ana mtaji wa Sh 100,000, akiulizwa mauzo anajibu swali la mtaji. Akipigiwa mzunguko wa Sh 100,000 kwa siku huyu anajikuta anaambiwa ana mzunguko wa Sh milioni 36 kwa mwaka.

Ni bahati mbaya pia kuwa kuna watu wanauza bidhaa mbazo faida yake ni Sh 200 hadi 500. Kwa mfano, mtu anayeuza saruji, ananunua mfuko wa saruji Sh 13,500, anauuza Sh 14,000. Hapo kuna gharama za kodi ya pango, wafanyakazi, umeme na gharama nyingine. Huyu akiuza mifuko 10 kwa siku, atahesabiwa anaingiza Sh 140,000. Kumbe uhalisia ameingiza Sh 5,000, zilizobaki amezungusha mtaji.

Ni katika hatua hii, wafanyakazi wa TRA watamkadiria kodi mhusika, asipoangalia anaweza akajikuta baada ya miezi 6, mtaji wa kununua saruji wote ameutumia kulipa kodi. Kwa mantiki hiyo, ni vema ukiona biashara yako haina faida inayolingana na makadirio anayokufanyia ofisa wa TRA, mwambia muambatane hadi eneo la biashara akashuhudie vitabu vyako vya mauzo aweze kuelewa unaingiza shilingi ngapi.

>>Itaendelea wiki ijayo.

Please follow and like us:
Pin Share