Wiki iliyopita nilihitimisha makala yangu kwa kuzungumzia ukadiriaji wa mapato/mauzo/mzunguko, kiwango ambacho hutumika kumkadiria kodi ya mapato mfanyabiashara. Kabla sijaendelea, yametukuta tena. Mtangazaji maarufu nchini, Ephraim Kibonde, amefariki dunia. Kibonde, ndiye alikuwa mwendesha shughuli ya maziko ya Ruge Mutahaba huko Bukoba, sasa naye amefariki dunia.

Naipa tena pole familia ya Clouds na wanahabari wote hapa nchini. Ni habari mbaya, niko nje ya Dar es Salaam na naomba Mungu ainusuru tasnia ya habari maana kasi ya waandishi kufariki dunia imetisha ndani ya miaka hii miwili. Naipa pole pia familia ya mzee Kibonde, ndugu, jamaa na marafiki. Mungu ailaze mahala pema peponi roho ya Kibonde. Amina.

Sitanii, misiba imeingilia makala hii kwa wiki mbili sasa. Kwa ubinadamu, lisingekuwa jambo jema kuona watu wawili kama Ruge na Kibonde, niliofanya nao kazi kwa nyakati tofauti wafariki dunia ilivyotokea, mimi niendelee na makala hii bila kugusia misiba yao kana kwamba sitambui kilichotokea. Naamini hata wewe msomaji wangu utakuwa umekubaliana nami, na tushirikiane katika kuomboleza vifo hivi.

Nikirejea katika makala hii ya ‘Jinsi ya Kuanzisha Biashara Tanzania’, naomba niseme jambo moja kubwa kabla ya kuendelea. Watanzania tunapaswa kujisikia fahari kulipa kodi. Najua nchi yetu biashara si utamaduni wetu, hivyo si jadi yetu kulipa kodi, hasa ikikumbukwa dhana ya ‘Kodi ya Kichwa’ iliyokuwa kodi ya manyanyaso. Tunahitaji kuwajenga Watanzania wajue umuhimu na wakubali kulipa kodi.

Sitanii, mimi kwa mfano najisikia fahari kubwa kuona kupitia kampuni yangu nalipa kodi isiyopungua Sh milioni 60 kwa mwaka, kupitia kodi kama VAT, PAYE, SDL, WCF, NHIF… Malipo haya naamini yanachangia kujenga uchumi wa taifa letu. Natamani biashara yangu ikue, niweze kulipa kiasi hiki cha kodi kwa siku au zaidi, kwa maana kwa mwaka niweze kulipa kodi ya Sh bilioni 21 au zaidi.

Binadamu tunapaswa kujiwekea malengo. Ukiweka malengo ya chini, utaishia kushindwa. Nilikuwa na mwalimu wangu aliyenifundisha kidato cha tano, namkumbuka kwa jina la Mutembei. Alikuwa akitwambia hivi: “Aim higher, work harder, your failure will be your success.” Tafsiri yake ni: “Weka malengo ya juu, fanya kazi kwa bidii, kushindwa kwako kutakuwa mafanikio yako.”

Sitanii, mfano huu unamaanisha nini? Mimi kwa mfano kwa kuweka lengo la kulipa kodi ya Sh bilioni 21 kwa mwaka katika siku ambayo Mungu ataichagua kutokana na juhudi ninazozifanya, nikishindwa nikaishia kulipa Sh bilioni 6, si haba, nitakuwa nimeingiza si chini ya Sh bilioni 20. Haya ndiyo malengo.

Naandika makala hizi kuhamasisha Watanzania kuweka malengo ya juu, kwani kwa kufanya hivyo Watanzania wanatajirika na nchi inatajirika. Wanaposema kufuta umaskini, ufutaji huo unaanzia kwa mtu mmoja mmoja na aliyefutiwa umaskini akilipa kodi, huduma za jamii kama ujenzi wa barabara, reli, viwanja vya ndege, maji, elimu, huduma za afya, usafi wa mazingira na mengine zinaimarika.

Katika makala zilizotangulia niligusia suala la kila Mtanzania mwenye umri wa miaka 18 na kuendelea kuwa na Namba ya Mlipa Kodi (TIN). Kuna dhana kuwa ukipewa namba hii unalipishwa kodi, si kweli. TIN ni namba unayoipata bure, na itatumika siku unayoanzisha biashara au kununua usafiri kama pikipiki, gari na vyombo vingine kama Bajaj.

Sitanii, ukianzisha biashara, namba yako ya TIN ukienda TRA kufanyiwa makadirio, ndiyo itakuwa mlango wa kulipia kodi utakayokuwa umekadiriwa. Kadiri unavyokua kibiashara, ndivyo utahama kutoka kwenye kukadiriwa kodi, ukalazimika kutengeneza hesabu zilizokaguliwa kama kampuni au mtu binafsi kulingana na kiwango cha mtaji na hapo utapaswa kupata namba nyingine ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT).

Baada ya kukadiriwa kodi ya mwaka inayolipwa kwa vipindi vinne ndani ya mwaka, unapolipa mkupuo wa kwanza TRA inapaswa kukupatia Cheti cha Mlipakodi (Tax Clearance Certificate). Cheti hiki kinakusaidia unapokwenda kuomba leseni ya biashara. Huwezi kupewa leseni ya biashara bila kuwa na ‘Tax Clearance Certificate.’

Ukiishapewa hiki cheti unakipeleka katika halmashauri ya wilaya unakofanyia biashara yako ndipo unapewa leseni ya kufanya biashara hiyo. Hapo unapaswa kumwona Afisa Biashara wa Wilaya, ambaye kwa maelezo ya aina ya biashara unayoifanya ataangalia kwenye orodha ya kiwango cha kodi na kukwambia unapaswa kulipia shilingi ngapi kwa mwaka.

Kumbuka kuna biashara zina leseni zaidi ya moja, hivyo kama nilivyosema kabla ya kuanzisha biashara, unapaswa kufanya utafiti ili kufahamu aina ya biashara unayotaka kuifanya, eneo unalopaswa kufanyia, aina ya wateja, aina za kodi, leseni na mengine mengi. Ikumbukwe hapa nazungumzia mtu aliyechagua kuanzisha biashara kama mtu binafsi, hapa sijazungumzia jina la biashara au kampuni. Tukutane wiki ijayo.

By Jamhuri