Wiki iliyopita nilihitimisha makala hii kwa aya hii: “Kumbuka kuna biashara zina leseni zaidi ya moja, hivyo kama nilivyosema kabla ya kuanzisha biashara, unapaswa ufanye utafiti kufahamu aina ya biashara unayotaka kuifanya, eneo unalopaswa kufanyia, aina ya wateja, aina za kodi, leseni na mengine mengi. Ikumbukwe hapa nazungumzia mtu aliyechagua kuanzisha biashara kama mtu binafsi, hapa sijazungumzia jina la biashara au kampuni. Tukutane wiki ijayo.”

Katika eneo la leseni, kimakosa nilitumia neno ‘kodi’ unayopaswa kulipa kwa Afisa Biashara wa Wilaya. Usahihi ni ‘ada’ ya leseni na si ‘kodi’. Wasomaji wengi mmeniuliza aina ya kodi zinazolipwa, hili naomba iwe mada inayojitegemea siku zijazo. Kwa sasa nieleze mchakato wa kuanzisha biashara katika makala hii ya ‘Jinsi ya Kuanzisha Biashara Tanzania’.

Unapofika kwa Afisa Biashara wa Wilaya, ambaye anapatikana kwenye Halmashauri ya Wilaya unakofanyia biashara, utahitajika kukaguliwa eneo lako unalofanyia biashara kabla ya kupewa leseni. Wapo watu walioniuliza kwa nini wanakwenda kulipia leseni wanacheleweshwa kupewa kwa kuelezwa kuwa wanatakiwa kukaguliwa.

Sitanii, kulingana na aina ya biashara na kama ni mara ya kwanza watoa leseni watalazimika kukagua eneo lako la biashara. Mmoja ni “Bwana/Bibi Afya.” Kuna baadhi ya watu wanaanzisha biashara lakini hawana choo cha watumishi wao wanaoendesha biashara kwa ajili ya kujisaidia. Kama hauna choo nakuhakikishia utanyimwa leseni.

Ni lazima eneo la biashara liwe safi. Lisiwe na vitu hatarishi. Liwe na maji ya kutosha wafanyakazi kujisafisha muda wowote. Kulingana na biashara unayofanya, kama ni viwanda vidogo vidogo, utatakiwa kukaguliwa pia na Jeshi la Zimamoto, kujiridhisha kuwa unavyo vifaa vya kuzimia moto katika eneo lako la biashara.

Ikiwa biashara yako inahusu vyakula na vinywaji, unaweza kutakiwa kukaguliwa na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Halmashauri ya Mji/Jiji/Manispaa au Mamlaka ya Mji Mdogo kujiridhisha iwapo una sifa zote za kufanya biashara katika eneo hilo na biashara yako haitahatarisha maisha ya watu wanaofanya kazi kwenye eneo lako au majirani zako.

Ukaguzi unaweza kuwa wa aina mbalimbali kulingana na aina ya biashara nilivyosema. Utapewa orodha na Afisa Biashara wa Wilaya ni ukaguzi wa aina gani unapaswa kufanywa. Baada ya ukaguzi kukamilika, basi Afisa Biashara wa Wilaya atakujulisha iwapo maombi yako ya leseni yamekubaliwa au yamekataliwa.

Kuna mchakato wa leseni kukubaliwa au kukataliwa. Maombi yako lazima yapelekwe kwenye kikao cha Baraza la Madiwani la Halmashauri husika. Madiwani watapitia nyaraka zilizoambatanishwa na kuridhia iwapo umekidhi vigezo au la. Kwa hiyo usidhani mtu pekee anayemaliza suala la leseni yako ni Afisa Biashara!

Sitanii, iwapo maombi yako yamekataliwa, utaelezwa sababu na upungufu uliopo katika eneo lako la biashara, ambapo utapewa muda wa kurekebisha na kukaguliwa tena. Ikiwa umekubaliwa, basi utapewa namba ya malipo (control number) na kiasi unachopaswa kulipa. Fedha hizo unaweza kuzilipa benki katika tawi lililoelekezwa au kupitia simu ya mkononi.

Baada ya hapo utaelezwa muda wa kwenda kuchukua leseni yako. Kumbuka, ukipewa leseni uigeuze nyuma na kusoma masharti ya leseni. Haimaanishi kuwa ukipewa leseni ndiyo umemaliza. Leseni yako kwa mujibu wa masharti yaliyoandikwa nyuma ya leseni husika, usipotimiza masharti hayo inaweza kufutwa.

Sitanii, pia itambulike kuwa leseni inakatwa kila mwaka. Kuna watu wamenipigia simu wakilalamika kuwa wamefungiwa biashara kwa kuelezwa kuwa hawana leseni wakati leseni wanazo. Ni kweli kuwa kati ya mwaka 2004 na 2014, leseni zilikuwa hazibadilishwi. Ilikuwa ukipata leseni ya biashara inakuwa ya kudumu.

Tangu mwaka 2014 mambo yalibadilika. Leseni zinapaswa kuhuishwa (renew) kila mwaka. Unapaswa kuangalia tarehe ilipokatwa leseni yako na mwezi mmoja kabla ya tarehe hiyo uende kwenye halmashauri iliyokupatia leseni kwa ajili ya kulipa ada ya mwaka, kukaguliwa kama bado unaendelea na biashara uliyotaja kuwa unaifanya, hivyo kupewe leseni mpya ya mwaka husika. Usipokwenda kuna adhabu (penalty) ya kuchelewa kulipia leseni yako.

Kumbuka, kabla ya kwenda kwenye halmashauri kuhuisha leseni yako, unapaswa kwenda TRA kukadiriwa mapato ya mwaka mpya na kupewa cheti cha mlipakodi kipya baada ya kulipa angalau fungu la kwanza la kodi uliyokadiriwa na ndipo upewe hicho cheti utakachokipeleka kwa ajili ya kupewa leseni mpya.

Nasisitiza, utaratibu huu nilioueleza hapa katika makala hii ni wa mtu anayefanya biashara kama mtu binafsi. Wiki ijayo nitaeleza mtu anayetaka kufanya biashara kwa Jina la Biashara (Business Name). Kwa mfano, ikiwa unaanzisha nyumba ya kulala wageni (Guest House). Biashara hii ni vema angalau kama hujaanzisha kampuni, iwe na jina la biashara. Nitaeleza umuhimu wa jina la biashara na taratibu za kupata jina la biashara kwa nia ya kuendesha biashara yako. Tukutane wiki ijayo.

699 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!