Leo naandika makala hii nikiwa hapa Bukoba. Nimesafiri kutoka Dar es Salaam hadi Bukoba kwa kutumia usafiri wa gari dogo (IST). Kauli aliyopata kuitoa Rais John Pombe Magufuli kuwa ipo siku mtu atasafiri kwa teksi kutoka Mtwara hadi Bukoba, hakika ni ya kweli. Waswahili wanasema: “Baniani mbaya, kiatu chake dawa.”

Sitanii, hakika Rais Magufuli anajenga miundombinu. Mikoa yote niliyopita, Pwani, Morogoro, Dodoma, Singida, Tabora, Shinyanga, Mwanza, Geita na Kagera (si kwa kupita barabara kuu, bali kwa kukaa siku 1 hadi 2 nikikagua masoko ya gazeti letu), nimeshuhudia ujenzi mkubwa wa barabara. Nilichokiona, kimenitia moyo, ila nikaona ni Kata ya Kitunda pekee katika Jiji la Dar es Salaam iliyosahaulika katika ujenzi wa miundombinu!

Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Magufuli inastahili pongezi kwa kujenga barabara kuu na barabara za mitaa katika miji mbalimbali. Miji kama Biharamulo na Muleba iliyokuwa imesahaulika miaka mingi, kwa sasa nayo lami zinajengwa kila kona. Hii inastahili kupongezwa, lakini pia ni fursa ya biashara.

Nimeamua kuligusia hili, kwa maana naeleza katika makala hii jinsi ya kufanya biashara. Biashara zimekuwa ngumu hapa nchini kutokana na miundombinu hafifu. Kama una barabara za wilaya zisizopitika kwa miezi 10 katika mwaka, basi ufahamu taifa hilo haliwezi kuendelea.

Kwamba, kwa mfano unauza nyanya, mchicha au mayai kutoka Uyui kwenda Tabora au unauza maziwa (fresh) kutoka Kisesa kwenda Kwimba au Mwanza mjini, kama barabara ni mbovu, nakuhakikishia biashara hii itaharibika kabla ya kufika sokoni.

Na kwa kuharibika, mfanyabiashara anakosa fedha na serikali inakosa kodi, ambayo ni mapato yanayojenga utajiri wa serikali. Hivyo, barabara na reli ni muhimu katika kukuza uchumi.

Sitanii, ahadi yangu wiki iliyopita ilikuwa ni kuzungumzia usajili wa “Jina la Biashara.” Nimeulizwa na wasomaji kadhaa wiki iliyopita wakitaka kujua “Jina la Biashara” ni nini? Na mwingine amehoji linasaidiaje katika kuendesha biashara kama ya gesti?

Kwa mujibu wa Sheria ya Usajili wa Jina la Biashara ya Mwaka 1930 kama ilivyorekebishwa mwaka 1972, 2002 na 2007, Jina la Biashara ni Jina au Maneno unayoyatumia kuendesha biashara yako. Kwa mfano unaweza kuamua kuita biashara yako Lubabi, Kikonya, Nkuba, Waridi, Kyoma au Ntondo.

Sheria hii inakuruhusu wewe kama mmiliki wa biashara kuchagua aina ya jina unalohitaji kulitumia katika biashara unayoianzisha na kulisajili kwa nia ya kuitambulisha biashara yako.

Nimeulizwa maswali mengi na wasomaji wangu kuwa ina faida gani kusajili Jina la Biashara. Kimsingi faida ni nyingi. Ni vigumu kwa mfano kuanzisha na kutangaza biashara kwa kutumia jina lako ikakubalika kwa watu wa kada mbalimbali. Katika jamii wapo wanaokupenda na wapo wanaokuchukia.

Ukitumia jina lako halisi kwenye biashara unaweza kupoteza baadhi ya wateja uliokwaruzana nao au wanaokuchukia kwa wajihi wako tu. Suala la pili, jina la biashara linakusaidia kutambua biashara yako na kujitangaza kwa urahisi. Unapaswa kuchagua jina linalotamkika na linalovutia wateja.

Jina kama “Ntandamanjuile”, si wote wanaoweza kulitamka. Litafukuza wateja. Jina kama “Ujenzi” linatamkika kwa kila awaye. Hata watoto hawatapotea dukani kwako wakitumwa. Majina rahisi na yanayotamkika vizuri katika biashara ni tangazo na kivutio tosha kwa wateja wako.

Tatu, ukisajili jina la biashara, sheria inaruhusu kupeleka nakala ya hati ya usajili benki ukafungua akaunti ya hundi, hivyo ukaondokana na mchezo wa kutumia taslimu katika biashara yako.

Si hilo tu, kwa kutumia jina la biashara unaweza kuingia ubia au ukaunganisha nguvu na watu wengine kuanzia mmoja na kuendelea na mkafanya biashara kisheria.

Sitanii, Jina la Biashara unaweza kulisajili kama mtu binafsi, washirika mlioungana, kampuni iliyosajiliwa au kampuni zinazolenga kufanya biashara pamoja kwa kuunganisha nguvu na mambo ya aina hiyo.

Kimsingi, kusajili jina la biashara ni hatua muhimu na ya msingi, inayomwelekeza mhusika katika kumiliki kampuni iliyosajiliwa baada ya kuwa amefanya biashara na kupata uzoefu.

Usajili huu unamwondoa mfanyabiashara wa Kitanzania katika uchuuzi na umachinga na kuanza kumiliki taasisi inayoeleweka ambayo mwisho wa siku itaishia kuwa kampuni yenye ukomo na inayotengeneza faida kubwa ikiongozwa vema milele na milele.

Je, unafahamu utaratibu wa kisheria wa kusajili Jina la Biashara, gharama ya usajili, muda wa kukamilisha usajili, nyaraka zinazotakiwa, umri wa mtu anayetaka kusajili Jina la Biashara na matakwa mengine ya kisheria? Usikose nakala yako ya gazeti hili makini la uchunguzi JAMHURI Jumanne ijayo.

By Jamhuri