Mpendwa msomaji, leo ni siku nyingine tunapokutana hapa. Nikiri wiki iliyopita nilihitimisha makala hii na maneno haya: “Mwisho, nawaomba wasomaji wangu, mniruhusu nisiwe ninawajibu maswali yenu kwa sasa kwani ni mengi. Nikiingia katika kujibu maswali hayo kama nilivyofanya leo, hakika sitaweza kukamilisha mada hii inayopaswa kuwa na makala zisizopungua 12 zikiwa msingi wa jinsi ya kufanya biashara Tanzania. Tukutane wiki ijayo.”

Sitanii, nikiri sikuwa sahihi. Nikiwa Dodoma wiki iliyopita, nimekutana na wasomaji wangu wengine, wengi wakiwa wabunge. Nimepokea simu kadhaa zinazoomba ufafanuzi katika eneo la kupata leseni. Hakika busara imenituma niwasikilize wasomaji wangu nini wanachokihitaji, kwani nia ni kuwezesha watu kufanya biashara kwa urahisi badala ya kuendelea kuhangaika kama hali ilivyo kwa wengi sasa.

Kimsingi sikufahamu kuwa watu walio wengi hawafahamu taratibu za kupata leseni ya biashara. Kutokana na hata baadhi ya wabunge niliozungumza nao kuuliza swali hili, sasa naomba nieleze taratibu za kupata leseni za biashara.

Kama nilivyoeleza katika makala iliyotangulia awali, leseni za biashara zipo za aina mbili. Hata hivyo, sikuwa nimeingia kwa kina katika eneo hili kwa kudhani kuwa wengi wanaofanya biashara wanao uelewa katika eneo hili kumbe sikuwa sahihi.

Kutokana na maombi kuwa mengi, nimeona sina sababu ya kuandika makala isiyojibu shida halisi za wasomaji wangu. Kwa mantiki hiyo, kwa kuwa hili suala la kupata leseni ni la msingi, iwe unatumia jina la biashara au kampuni au unafanya biashara kama mtu binafsi, nimeona ni bora nilipe msisitizo unaostahili, kwa kueleza aina ya leseni unayopaswa kuwa nayo na inapatikana wapi.

Sitanii, kupata leseni ya biashara iwe unafanya kama mtu binafsi, kwa kutumia jina la biashara au kampuni, inakupasa kujaza “Fomu ya Maombi ya Biashara” Na. TFN 211. Fomu hii inatolewa chini ya Kifungu cha 11 cha Sheria ya Leseni Na. 25 ya Mwaka 1972 kama ilivyorekebishwa mara kadhaa.

Leseni zipo katika makundi mawili; Kundi A na Kundi B. Makundi haya yanatokana na aina ya biashara unayofanya. Kwa kila kundi unapaswa kujaza nakala mbili za fomu hii kwa kutoa taarifa zifuatazo;- Ikiwa unahuisha maombi yako, fomu yenyewe inasema maombi yanayorudiwa, mara tu baada ya kujaza fomu hiyo unaipeleka kwa ofisa aliyekupa leseni ilioisha kuandikiwa kiwango cha ada ya mwaka unayopaswa kulipa, maana kwa mujibu wa kanuni ada hubadilika kila zinapopitishwa na Bunge.

Sitanii, tatizo ni kwa waombaji wa mara ya kwanza. Hawa wengi ndio hawajui waanzie wapi na wafanye nini. Nimesema unapaswa kujaza Fomu ya Maombi ya Leseni ya Biashara. Fomu hii inapatikana kwenye mitandao ya halmashauri na Brela (www.brela.go.tz).

Kifungu cha 14 cha fomu hiyo kinaeleza hatua zote unazopaswa kupitia kujaza fomu hii (nitaeleza vema katika makala ijayo). Unapaswa kupita katika ngazi zote kuhakikisha zinajazwa na wahusika, bila kujali ni biashara ipi unayoifanya.

Mwombaji anayeruka moja ya ngazi nitakazozitaja hapa, hatapewa leseni, na wakati mwingine pia akitoa maelezo ya uongo, anaweza kushtakiwa kwa mujibu wa sheria na kulipishwa faini au kufungwa jela. Kuna jambo ninapaswa kulisema wazi hapa, kuwa maombi ya leseni hayapaswi kuunganishwa na masharti yasiyo ya kisheria kama kulazimishwa kulipa michango ya Mwenge au maendeleo ya eneo unakotaka kufanyia biashara.

Unapoomba leseni unapaswa kutaja jina la mwombaji. Hili eneo la kwanza unajaza jina kama inayoomba ni kampuni, jina la biashara au mtu binafsi. Ikiwa umesajili kampuni au jina la biashara, unapaswa kuandika namba ya hati ya kusajiliwa. Kwa mtu binafsi hii haikuhusu, unaiacha wazi.

Sharti la tatu ni kuthibitisha uraia wa wanahisa kwa wenye kampuni. Sharti la nne, ni kuweka anwani yako, kisha kuonyesha wilaya, kata na mtaa unakotaka kufanyia biashara. Unapaswa kuonyesha namba ya kiwanja unakofanyia biashara, namba ya leseni ya zamani kama unayo, namba ya mlipakodi (TIN), jina la mkurugenzi au meneja wa biashara pia linapaswa kutajwa.

Taja aina ya biashara unayotaka kufanya. Pia hapa kuna leseni ndogo inayotolewa kwa ajili ya tawi la biashara ile ile unayoifanya. Kwa mfano una leseni ya biashara Dar es Salaam, unapaswa kuwa na tawi Dodoma au Mwanza, unachofanya ni kutaja namba ya leseni ya kwanza kisha ukaeleza kuwa unaomba leseni ya tawi.

Sitanii, bila kushurutishwa unapaswa kueleza katika leseni hiyo, iwapo ndani ya miezi 12 iliyopita umewahi kuhukumiwa kifungo jela au la. Kisha unathibitisha maombi yako, na kuyawasilisha kwa mamlaka husika. Uamuzi utafanywa katika ngazi mbalimbali kama nitakavyozieleza wiki ijayo. Pia nitaeleza fomu hiyo unapaswa kuipeleka kwa nani isainiwe au kupitishwa kabla hujaipeleka ama wizarani au kwenye halmashauri husika. Usikose nakala yako ya JAMHURI kupata undani wa taratibu za kufanya biashara Tanzania.

Please follow and like us:
Pin Share