catoon 2 copyUkiwa ni mwezi mmoja tangu Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete, ang’atuke kikatiba, duru za uchunguzi zinaonyesha kuwa kiongozi huyo aliliumiza Taifa kwenye nyanja nyingi.

Wakati akiingia madarakani mwaka 2005, deni la Taifa lilikuwa Sh trilioni 5.5; lakini miaka 10 baadaye deni hilo amelipaisha hadi kufikia Sh trilioni 41.

Mwaka 2005 dola moja ya Marekani ilikuwa Sh 1,166 lakini wakati Kikwete, anatoka madarakani mwaka huu dola moja ilikuwa wastani wa Sh 2,200.

Kuongezeka kwa deni la Taifa na kushuka kwa thamani ya shilingi kunatajwa na wataalamu wa uchumi kwamba kumesababishwa na uuzaji bidhaa nje ya nchi kupungua na ongezeko la mikopo kutoka kwenye benki za kibiashara na mashirika ya fedha ya kimataifa.

Pamoja na kufanikiwa kuongeza makusanyo ya kodi kutoka wastani ya Sh bilioni 170 kwa mwezi hadi Sh bilioni 900 kwa kipindi hicho, badi ukwepaji kodi ulikithiri na kuathiri mno ukuaji uchumi.

Ukwepaji kodi uliokithiri katika Bandari na kwa wafanyabiashara wengi kutolipa kodi kunatajwa kuwa miongoni mwa sababu zilizofanya umaskini uongezeke miongoni mwa Watanzania licha ya takwimu za kiuchumi kuonyesha kuwa uchumi ulikuwa ukikua kwa kasi.

Chini ya uongozi wa Rais Kikwete, Tanzania ilijulikana kama pepo ya wakwepa kodi, huku kukiwapo madai kuwa, ama yeye, au familia yake walibariki baadhi ya wafanyabiashara kuitumia Ikulu kukwepa kodi.

Makontena zaidi ya 330 yaliyotolewa kwenye Bandari Kavu (ICD) ya Azam bila kulipiwa ushuru/kodi yenye thamani ya Sh bilioni 12 yanachukuliwa kama kilelezo halisi cha namna Serikali ya Rais Kikwete, ilivyokuwa dhaifu kwenye ukusaji kodi. Tayari wafanyabiashara wameshalipa Sh bilioni 10 serikalini baada ya agizo la Rais John Magufuli, la kuwataka wafanyabiashara hao wawe wamelipa ndani ya siku saba vinginevyo wangekutana na mkono wa kisheria.

Rais Mstaafu Kikwete, akiwa Chalinze wiki iliyopita, alisema wakwepa kodi wataendelea kuwapo, na kwamba kinachotakiwa kufanywa na Rais Magufuli ni kuendelea kupambana na wahusika.

Hata pale sakata la fedha za Akaunti ya Tegeta Escrow lilipoibuka, Rais Kikwete aliutangazia umma na ulimwengu kuwa Serikali haikuwa na chake kwenye fedha hizo. Wananchi kadhaa wenye weledi na masuala ya kodi walimpinga wakisema waliochota fedha za Escrow walipaswa kulipa kodi serikalini kutoka kwenye mapato waliyopata.

 

Mambo yalivyokuwa

Kwenye kipengele cha 7.0. cha utetezi huo wa BoT kinahusu‘Ushauri wa kuujulisha uongozi wa nchi’.

Kinasema hivi: “Mnamo tarehe 24 Oktoba, 2013, BoT ilimuandikia PST, ikimuomba kuchukua hatua kadhaa kuhusiana na malipo ya IPTL. Miongoni mwa mambo yaliyoshauriwa na BoT yalikuwa ni:

“(i) Kwamba ufungaji wa Escrow Account uzingatie kwamba mamlaka ya kufanya hivyo yako kwa Paymaster General;

“(ii) Kwamba, kwa kuzingatia unyeti wa suala hili na ukubwa wa malipo husika, Waziri wa Fedha apate fursa ya kuwajulisha Mheshimiwa Rais na Mheshimiwa Waziri Mkuu ili waeleze kama wanaridhia au la; na

“(iii) Kwamba GoT iombe kutolewa kwa kinga itakayoikinga GoT dhidi ya madai yanayoweza kujitokeza baada ya malipo hayo kufanyika.”

Maelezo hayo ya BoT yanafafanuliwa na wafuatiliaji wa sakata la Escrow kwamba yanathibitisha ushirikishwaji wa viongozi wakuu kwenye utoaji fedha hizo.

Ofisa mmoja ndani ya BoT, aliyezungumza kwa masharti ya kutotajwa jina, amesema: “Ikulu haiwezi kuchomoa katika hili, pengine inataka kusema Mbena alishiriki yeye mwenyewe kama yeye bila kufuata utaratibu. Ikulu inataka kusema Mbena, ama alighushi barua, au hakuwashirikisha wakubwa kutoa maelezo hayo.”

Anasema BoT isingeweza kuchukua hatua kubwa ya kuruhusu utoaji fedha kama isingepata baraka kutoka Ofisi ya Waziri M.kuu na Ikulu

Kipengele cha 10.0 cha utetezi wa BoT kinahusu Kibali cha kuhamisha fedha kwenda IPTL.

Kinasema: Mnamo tarehe 14 Novemba, 2013, PST aliwasilisha kwa utekelezaji, maagizo ya Mheshimiwa Rais ambaye aliagiza kwamba “Maamuzi ya Mahakama Kuu yatekelezwe kama alivyoshauri AG”. Maagizo ya Mheshimiwa Rais yaliwasilishwa kwa PST kwa barua ya tarehe 13 Novemba, 2013, na ilisainiwa na Katibu wa Rais, Bwana Prosper Mbena.”

Baada ya kupata maelekezo hayo, ndipo BoT ilipomwandikia PST, ikiomba muongozo kuhusiana na suala la madai ya TRA kuhusiana na VAT.

Barua hiyo iliandikwa Novemba 15, 2013, na nakala yake kupelekwa kwa AG.

Kilichozingatiwa na BoT ni kwamba madai ya kodi za Serikali yanachukuliwa kama madai yenye umuhimu wa juu katika malipo yoyote.

Kwenye taarifa yake, BoT inasema: “Hata hivyo, BoT ilikwenda mbali kuhakikisha kwamba utekelezaji wa uamuzi wa Mahakama, pamoja na Makubaliano ya kukabidhi fedha unapata baraka za wakuu wa nchi kama vile Mheshimiwa Rais na Waziri Mkuu.”

Rekodi za Bunge (Hansard) zinaonyesha kuwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, aliihusisha Ikulu moja kwa moja na uchotwaji wa fedha hizo, Sh bilioni 320 kutoka Tegeta Escrow.

Alimtaja Mnikulu, Shabani Gurumo, kwamba ni miongoni mwa waliopata mgao wa Sh milioni zaidi ya 800.

Aidha, alisema kampuni ya Independent Tanzania Power Limited (IPTL) iliingia nchini wakati Rais Jakaya Kikwete akiwa Waziri wa Nishati na Madini.

Akaongeza kuwa mchakato wa malipo ya IPTL ulianza wakati Rais Kikwete akiwa Waziri wa Fedha, na kwamba fedha zimechotwa Kikwete akiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Licha ya kashfa hiyo ya kujipatia mamilioni ya fedha, Kikwete, akiwa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na msimamizi wa vikao vyote vikuu vya chama hicho, alibariki uamuzi wa Mbena wa kugombea ubunge Jimbo la Morogoro Kusini; na akashinda. Vyanzo vya habari vimeliambia JAMHURI kuwa siku chache baada ya Rais Magufuli kuapishwa, Mbena ameitwa kuhojiwa katika Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuhusu fedha hizo za Escrow.

 

Mamia ya safari za Kikwete nje ya nchi

Rais Mstaafu Kikwete, anatajwa kuwa ndiye anayeshikilia rekodi miongoni mwa marais wa Afrika, ya kusafiri nje ya nchi kuliko rais yeyote.

Tangu aingie madarakani mwaka 2005, Kikwete, amesafiri safari zaidi ya 300.

Baadhi ya safari alizoshiriki zilikosolewa na wananchi kwani nyingine zilistahili awakilishwe na wakurugenzi au wakuu wa idara.

Kwa safari 300 pekee, ikichukuliwa kuwa kila safari alitumia wastani wa siku nne, hiyo ina maana Rais Kikwete aliweza kuwa nje ya nchi kwa siku 1,200 ambazo ni miaka 3 na miezi mitatu hivi. Baadhi ya safari alizosafiri Ulaya na hata Marekani, aliweza kukaa huko hadi wiki mbili; na wakati fulani alibaki huko kwa wiki tatu.

Ujumbe wa Rais mara kadhaa huhusisha mkewe, walinzi, mawaziri, Waziri wa Mambo ya Nje, wasaidizi binafsi wa Rais na wale wa mke wake; na mara kadha wana familia. Uzoefu unaonyesha kuwa msafara wa Rais Kikwete, ulikuwa hauwezi kukosa watu 25.

Mwaka 2006 kwa viwango vya Serikali vya wakati huo, watu wanaosafiri kwenye msafara wa rais walilipwa kati ya dola 350 na 500 za Marekani (Sh. 600,000 kwa siku).

Rais hulala katika hoteli yenye hadhi ya nyota tano ambayo gharama yake huweza kuzidi dola 2,000 kwa siku moja.

Hotelini hapo hulala pia na wasaidizi wa karibu, wakiwamo walinzi, madaktari na hata wahudumu wa chakula.

Kwa safari kama ya Mei 12 hadi Mei 26 mwaka 2006, wakati Rais Kikwete alipokuwa nje ya nchi kwa karibu wiki mbili, alitumia mamilioni.

Katika safari yake hiyo, Rais Kikwete alitembelea Uganda, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Ufaransa na Marekani.

Uchunguzi umeonyesha kuwa safari nyingi za Kikwete, zilikuwa nje ya Afrika, hasa Ulaya na Marekani. Pia kwenye nchi za Afrika alikaa wastani wa siku mbili, lakini katika mataifa ya Ulaya na Marekani alikaa hadi wiki mbili.

Mwaka 2006 akiwa ndiyo kwanza ameupata urais, Rais Kikwete alifanya safari nyingi; jambo lililowashitua wananchi, hasa walipakodi. Tangu wakati huo safari zake ziliendelea kuongeza kwa kasi.

Kwa mwaka huo pekee, safari zake zilikuwa kama ifuatavyo:

Januari 19-25 alikuwa Khartoum, Sudan kuhudhuria mkutano wa nchi za Afrika (AU)

Machi 23 alifanya ziara ya siku moja ya kiserikali kujitambulisha Kigali, Rwanda.

Machi 22 alikwenda Kampala, Uganda kwa ziara ya siku moja ya kujitambulisha

Machi 24 alikwenda Nairobi, Kenya. Aprili 19-20 alikuwa Lesotho na Swaziland.

Aprili 21-22 Aprili alikuwa ziarani Maputo, Msumbiji;

Aprili 28 alikuwa Harare na Bulawayo, nchini Zimbabwe; Aprili 6 alikuwa Gaborone, Botswana; alikuwa ziarani Namibia kuanzia Aprili 10-12; Mei  7-9 alikuwa Pretoria, Afrika Kusini; Mei 12 alianza ziara ya wiki mbili katika nchi za Uganda (13 Mei), Arabuni (Mei 15), Ufaransa (Mei 16-19) na Marekani (Mei 21-26).

Mei 31 hadi Juni 3 alihudhuria Jukwaa la Kiuchumi la Dunia mjini Cape Town, Afrika Kusini; Julai 4 alihudhuria mkutano wa AU, Banjul nchini Gambia; Julai 10-12 alikuwa Cape Town, Afrika Kusini kuhudhuria mkutano wa viongozi wa serikali ulioandaliwa na kampuni ya Microsoft ya Marekani.

Julai 20 alihudhuria mkutano wa Leon Sullivan, Abuja nchini Nigeria.

Rais alikuwa Berlin Julai 21 na 22 kwa ajili ya kuchunguza afya yake;

Alihudhuria mkutano wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), Maseru nchini Lesotho kati ya Agosti 19 na 20.

Agosti 21-22 alikuwa ziarani Angola; Alienda Cuba Septemba 12 kwa maandalizi ya kikao cha Nchi Zisizofungamana na Upande Wowote (NAM);

Septemba 15 alikwenda Madrid, Hispania kwenye Uwanja wa Mpira wa uwanja wa Santiago Bernabeau unaotumiwa na klabu ya Real Madrid.

Septemba 15 hadi18, alikuwa Havana, Cuba kwa mkutano wa NAM

Septemba 19 na 25 Septemba, alikuwa kwenye Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, New York nchini Marekani. Ziara hizi zilizidi kuongezeka mwezi hadi mwezi.

 

Ukawa wamvaa Kikwete

Septemba, mwaka huu Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ulidai Kikwete amefanya safari 409 nje ya nchi katika kipindi cha utawala wake, akitumia shilingi zaidi ya trilioni 4.

Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, James Mbatia, alitoa madai hayo kwenye mkutano na waandishi wa habari.

Mbatia alisema katika kipindi hicho, Kikwete alifanya safari ambazo baadhi hazikuwa na umuhimu, akitoa mfano wa safari za kupokea digrii za heshima, kazi ambayo alisema ingeweza kufanywa na mabalozi.

Alisema Sh trilioni 4 zingeweza kutumika kwenye ujenzi wa vyuo vya ufundi, vyuo vikuu au hospitali.

 

Makala ya Vasco Da Gama

Mwandishi mmoja, mwaka 2012 katika Gazeti la Raia Mwema aliandika haya yafuatayo: 

Ni katika kutafakari kulingana kwa watu, matukio na mambo mbalimbali nilijikuta nikimuangalia Rais Jakaya Kikwete na kujaribu kutafuta mtu wa kihistoria ambaye anafanana naye kimsingi. Baada ya kuangalia kwa muda mrefu nimejikuta na mtu mmoja ambaye sisi watu wa Afrika ya Mashariki tunalijua jina lake vizuri kwani mtu huyo amepitia katika maeneo yetu karibu miaka mia tano iliyopita. Huyu si mwingine bali ni msafiri, mwanasiasa na mvumbuzi wa Kireno, Vasco Da Gama.

Ndiye huyo ambaye historia inamrekodi aliyeweza kuonesha njia ya kutoka Ulaya kwenda India kuzunguka kusini mwa Afrika. Rais wetu Jakaya Kikwete anafanana sana na Vasco da Gama na ni kufanana huko ambako leo kunanituma kuangalia safari za Rais Kikwete nje ya nchi, safari ambazo kwa hakika siyo tu zimekuwa za uvumbuzi bali ni za utambuzi, ugunduzi na kwa hakika zimekuwa ni safari za mwanasiasa, mwanadiplomasia na za kiongozi.

Mwanzoni mwa utawala wake na mara alipoanza safari hizi za kwenda nje ya nchi, tuliambiwa kuwa Rais wetu anafanya hivyo ili kujitambulisha kwa viongozi wa nchi za kigeni kuwa yeye ndiye “Rais mpya wa Tanzania”. Wengi tulikubali dhana hiyo bila kuihoji kwa undani kwa sababu tuliamini kabisa kuwa mataifa ya kigeni hayakufuatilia uchaguzi wa Tanzania na kwa hakika hawakujua Rais mpya wa Tanzania ni nani.

Na kwa vile Rais Kikwete alitaka atambulike hivyo ilibidi aende yeye “mwenyewe” kuwaonesha sura yake na tabasamu lake la kukata na shoka.

Hivyo safari zake za mwanzo kwenye nchi jirani zilikuwa na lengo la kujitambulisha. Hivyo ndivyo tulivyoambiwa. Miaka miwili baadaye safari za Rais Kikwete na wapambe wake zimezidi kupamba moto bila kukoma. Hivi karibuni Rais Kikwete ataondoka tena kwa ziara ya siku kadhaa huko Marekani.

Kati ya vitu ambavyo tunaambiwa kuwa Rais Kikwete anaenda kufanya ni kutangaza rasmi ujio wa Mkutano wa Kimataifa wa Taasisi ya Sullivan ambao utafanyika nchini mwakani. Kinachoshangaza sisi ambao ni wachunguzi wa mambo ya kisiasa nchini ni ulazima wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenda kutuutangazia ulimwengu ujio wa mkutano huo nchini.

Hivi ni kweli kuna ulazima wa Rais kwenda kufanya jambo hilo na hakuna kiongozi mwingine anayeweza kumuwakilisha kwenye tukio hilo? Imepangwa kuwa katika hafla hiyo Rais Kikwete atatumbuizwa na kundi la muziki lililotamba mwanzoni mwa miaka ya tisini la Boyz II Men.

Endapo tumefikia mahali kuwa Rais wetu ni lazima aende kwenye vihafla hivi na vimkutano hivi, kwa kweli kuna jambo moja tu ambalo ni dhahiri; nalo ni kwamba Rais Kikwete anapenda kusafiri sana, na safari zake hizi za uvumbuzi na utambuzi zimeanza kukaribia zile za yule msafiri wa Kireno, Bw. Da Gama.

Hata hivyo, watetezi wa safari hizi na makada wa chama tawala wanatuambia kuwa safari hizi siyo za utambuzi tu bali pia ni safari zenye “maslahi makubwa kwa Taifa”. Wanapotetea safari hizi makada hawa wanajaribu kutushawishi tuamini kuwa pasipo Rais Kikwete kwenda huko anakokwenda (iwe Uarabuni, Marekani au Ulaya), basi, misaada hiyo na uwekezaji huo hautakuja.

Mfano mzuri unaotolewa ni ahadi ya kutoka Shirika la Changamoto ya Milenia ambako tumeambiwa kuwa Tanzania itapata karibu dola nusu bilioni miaka michache ijayo. Ilipotangazwa habari hii miezi michache iliyopita, Rais Kikwete alikuwa Marekani na waliopiga baragumu la ushindi wakatuambia kuwa (japo si kwa maneno hayo moja kwa moja) kuwa tumepata msaada huo toka Marekani kwa sababu Rais Kikwete alikwenda huko.

Kitu ambacho hawakutuambia ni kuwa Tanzania haikuwa nchi peke yake iliyopewa ahadi kama hiyo baada ya kutimiza vigezo fulani fulani. Lesotho, nchi yenye watu milioni 2.3 (chini ya idadi ya watu wa Jiji la Dar), imepewa msaada kama wa kwetu wa dola milioni 362), Mongolia, yenye watu kama milioni 3 hivi, na wenyewe walipata msaada kama wa kwetu wa dola milioni 285 na El Salvador, yenye watu karibu milioni sita, wao wamepewa msaada huo toka kwenye akaunti ya Changamoto ya Milenia wenye kiasi cha dola milioni 461.

Hivyo, kufikiri kuwa tulipata msaada huo kwa sababu ya Kikwete kwenda huko ni kujidanganya. Ukweli wa mambo ni kuwa kuna misaada tunayoipata ambayo inaweza kuja bila ya Rais Kikwete kwenda huko kuomba au kuonesha sura yake. Endapo tutaweza kutimiza masharti au malengo fulani fulani wahisani wataona na watasaidia kama wanataka.

Binafsi, naamini kabisa kuwa baadhi ya safari hizi na msururu mzima unaoandamana na Rais Kikwete kwenda nje ya nchi siyo za lazima na zinaweza kufanywa na kiongozi mwingine ye yote yule kama Makamu wa Rais au Waziri Mkuu. Mfano mzuri ni ziara iliyopita ya Makamu wa Rais huko Iran na Misri. Kwa nini Makamu wa Rais hapewi mojawapo ya hizi ziara za kwenda Marekani? Kwa nini Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano asiende kwenye mojawapo ya misafara hii?

Isitoshe, safari hizi ni gharama kubwa kwa walipa kodi masikini wa Tanzania. Kwa mfano, kwa mwaka jana peke yake, inakadiriwa kuwa ziara za Rais zilitumia karibu shilingi bilioni 20 (safari, posho, na masurufu mbalimbali). Mwaka huu peke yake sina uhakika, lakini kama kuna mtu atakuwa tayari kutuambia ziara za Rais na viongozi wa juu zimegharibu kiasi gani, tunaweza kupatwa na shinikizo la moyo.

Wasafari wanaoambatana na Rais kwa hakika ni lazima na wenyewe “waambulie” kidogo. Mojawapo ya safari zake Rais Kikwete aliambatana na watu karibu 30 (sina uhakika msafara wa kawaida huwa na maafisa wa ngapi), lakini kwa Rais wa nchi ya daraja la tatu, na ambayo licha ya kelele za viongozi wake bado haijaanza kupaa, inasikitisha kuwa tunatumia fedha nyingi katika misafara hii.

Nina uhakika kabisa endapo safari za viongozi wote kwenda nje ya nchi zikifanyiwa hesabu bila ya shaka jumla yake itatushangaza. Sitoshangaa kabisa kuwa tukijumlisha fedha zilizotumika katika safari za Rais, Makamu, Waziri Mkuu na Mawaziri wengine kwenda nje ya nchi kwa miaka iliyopita, madarasa mengi tu ya shule za sekondari na zahanati vingejengwa, na wananchi husika wasingelazimika kuchangia!

Leo hii tunahangaika kuchangisha fedha za kujenga madarasa jijini Dar-es-Salaam. Hivi safari moja ya Rais inaweza kujenga madarasa mangapi? Je msafara mmoja wa Makamu wa Rais au Waziri Mkuu unaweza kusaidia kujenga vyoo vingapi vyenye maji katika shule ya Azania? Je, ile misafara ya watetezi wa bajeti walioenda mikoani ingeweza kuweka mapaa mazuri na kununua vifaa vingapi vya zahanati?

Binafsi, naamini kabisa tunaweza kupima mafanikio ya ziara hizo kwa kuangalia hesabu nyepesi. Endapo misaada ambayo tumeahidiwa katika ziara za viongozi wetu pamoja na uwekezaji ambao umefuatia ziara hizo unazidi kwa kiasi kikubwa gharama za kuwasafirisha kina Vasco da Gama wa kileo, basi, taifa linakuwa limepata faida.

Hata hivyo, endapo misaada hiyo na uwekezaji huo hauzidi gharama zilizotumika kuitafutia, basi, Watanzania hatunufaikinazo. Na hapa sizungumzii misaada na ahadi zote, ila ile tu ambayo “bila ya ziara za viongozi” isingewezekana.

Leo hii kuwaaimbia wimbo wa uwekezaji Wamarekani na Waingereza ni kama kurudia kibwagizo kile kile kwa kwaya yako. Wamarekani wangekuwa wanavutiwa na Tanzania wangeshaanza kuwekeza muda mrefu uliopita. Siyo kwa sababu hawajui; ni kwa sababu Tanzania haina maslahi makubwa kwa Wamarekani.

 

Urafiki na Marekani kimsingi unatokana na maslahi na hata wanapommwagia sifa rais wetu na kumpamba kwa pambio na maua tujue kuwa wanafanya hivyo kwa sababu moja tu; Rais wetu anakidhi maslahi yao katika eneo la Afrika ya Mashariki na hasa katika maslahi ya Marekani ulimwenguni.

 

Msumari wa Dk. Magufuli kwa wapenda safari

Dk. Magufuli ambaye aliapishwa Novemba 5, aliwataka watumishi wa umma wafanye zaidi ziara za vijijini ili kufahamu shida zinazowakabili wananchi. Akasema wapo watu wanaosafiri safari nyingi nje ya nchi kuliko wanavyokwenda vijijini kuwasalimu baba na mama zao.

Akizindua Bunge mjini Dodoma Novemba 20, mwaka huu, Rais Magufuli alisema: “Safari zote zisizo za lazima nje ya nchi serikalini tutazidhibiti na badala yake tutawatumia mabalozi wetu kutuwakilisha kwenye mikutano ya aina hiyo. Na pale inapolazimu kiongozi au mtumishi mwandamizi kusafiri tutahakikisa kwamba haandamani na msururu wa watu wengi ambao hawana umuhimu wala shughuli za kufanya katika safari hizo.

“Katika kusisitiza hili napenda niwape takwimu za fedha zilizotumika ndani ya Serikali, Mashirika ya Umma na Taasisi nyingine za Serikali kwa safari za nje kati ya mwaka 2013/14 na 2014/2015. Jumla ya shilingi bilioni 356.324 zilitumika kwa ajili ya safari za nje kama ifuatavyo:

•     Tiketi za ndege (Air ticket) zilitumia shilingi bilioni 183.160;

•     Mafunzo nje ya nchi (Training Foreign) zilitumia shilingi bilioni 68.612;

•     Posho za kujikimu (Per Diem Foreign) zilitumia shilingi bilioni 104.552;

“Wizara na Taasisi zinazoongoza kwa matumizi ya safari za nje ni pamoja na Bunge, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikano wa Kimataifa, Wizara ya Fedha, Ofisi ya Waziri Mkuu, Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali (NAOT), Wizara ya Mambo ya Ndani, n.k.

“Hizi fedha zingeweza kutumika vizuri kuboresha huduma za wananchi wa maisha ya chini, kama afya, maji, elimu, umeme n.k. Mfano; fedha hizi zingetosha kutengeneza kilometa 400 za barabara za lami, tujiulize zingeweza kutengeneza zahanati ngapi? Nyumba za walimu ngapi? Madawati mangapi? n.k. Hivyo tunapodhibiti safari za nje tunawaomba Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote mtuelewe na mtuunge mkono.

“Pili, tutahakikisha tunadhibiti safari na ziara za mafunzo nje ya nchi zinazogharamiwa na serikali ambayo yanapatikana hapa nchini.

“Tatu, tutadhibiti warsha, semina, makongamano, na matamasha ambayo kwa kweli yanatumia fedha nyingi tu za serikali lakini hayana tija na wala hayaongezi ufanisi katika utekelezaji na usimamizi wa sera na mipango ya Serikali.”

 

Utumbuaji kwenye sherehe

Sehemu nyingine ambayo uongozi wa Rais Kikwete umeliumiza Taifa ni kwenye sherehe na mambo yasiyo ya lazima.

Rais Kikwete alitumia Sh bilioni 50 kwa ajili ya maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru wa Tanganyika, huku fedha nyingi zikiishia kwenye uchapishaji khanga, fulana, kofia, wheel cover, posho, usafiri wa ndege na magari, vikundi vya ngoma, vinywaji na vyakula.

Kiasi hicho cha fedha kingeweza kujenga barabara ya lami yenye urefu usiopungua kilometa 50.

Matumizi mabaya ya fedha za umma yaliyosimamiwa na Kikwete, yamedhihirika mwezi huu baada ya Rais Magufuli, kubadili stali ya kusherehekea Uhuru wa Tanganyika kwa kufuta gwaride, ngoma na mbwembwe nyingine zisizo za lazima.

2164 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!