Wafanyakazi na Wahadhiri wa Chuo Kikuu Cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere (MNMA), wameingia katika mgogoro na uongozi wa taasisi kwa kushindwa kuwalipa zaidi ya Sh. milioni 700 ikiwa ni malimbikizo ya mishahara na posho.

Pamoja na Serikali kupinga kwa nguvu zote taasisi zake kuepuka kuzalisha madeni yasiyokuwa ya lazima, Chuo hicho kimeendelea kuajiri wafanyakazi bila kuzingatia taratibu za ajira na kushindwa kuwalipa mishahara.

Mei mwaka huu, chuo hicho kiliajiri walimu wapya 98 na watumishi wengine wa kada mbalimbali wapatao saba na kufanya jumla waajiriwa wapya kuwa 105, lakini hawajawahi kulipwa mishahara mipya hadi mwezi huu.

Imeelezwa kwamba kutokulipwa mishahara kwa watumishi hao kumetokana na Mkuu wa Chuo hicho kutoa ajira bila kupata kibali kutoka kwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Utumishi, ambaye ndiye mwenye mamlaka ya kutoa vibali vya ajira serikalini.

Watumishi hao, wengi wao wakiwa wametoka katika taasisi zingine na kuajiriwa katika chuo hicho kwa njia ya uhamisho wamekuwa wakilipwa mishahara midogo ambayo hutofautiana kwa viwango kuanzia Sh. milioni moja na kuendelea na kufikia kiasi cha deni hilo la Sh. milioni 700.

Hata hivyo, watumishi hao wamelieleza JAMHURI, kwamba jitihada za kufuatilia vibali Ofisi ya Katibu Mkuu, Utumishi zimefanyika mara nyingi bila mafanikio kwa madai kwamba Mkuu Wa Chuo ndiye aliyefanya makosa  kwa kujitwalia mamlaka yasiyomuhusu kwa kutoa ajira bila kupata kibali serikalini.

Wanasema uwezekano wakupata mishahara hiyo hadi mwaka mpya wa fedha wa 2016/17 wakati vibali vya wahadhiri hawa vinakwisha muda wake Julai 2016.

Kutokana na kasi ndogo ya kushughulikia madai yao wanasema wamekumbwa na hofu kwamba vibali vyao vitakwisha bila haki zao kupatiwa ufumbuzi na pengine uongozi wa chuo hauna nia ya dhati ya kuwaondolea kero hiyo.

Makamu Mkuu Wa Chuo hicho, Dk. Thomas Ndaluka alipohojiwa na JAMHURI kuhusu deni hilo na kutoa ajira kwa wafanyakazi bila kuzingatia taratibu zilizowekwa na serikali hakutaka kulizungumzia suala hilo huku akidai yeye siyo Ndaluka.

Pia alipotumiwa ujumbe mfupi wa maneno (sms) siku ya Jumamosi, Desemba 19 mwaka huu saa 10:57 jioni kwamba licha ya kukana kwamba yeye sio Ndaluka wakati taarifa za uhakika zikionesha namba za simu hiyo ni zake, hakuweza kutoa jibu lolote na muda mfupi simu yake haikupatikana tena.

Imeelezwa kwamba kwa muda mrefu uongozi wa chuo hicho umekuwa ukitoa taarifa za uongo wizarani kuhusu mapendekezo ya majina ya wanataaluma na wafanyakazi  ambao sio wawakilishi halali.

Wanasema vitendo vya uongozi wa chuo kutozingatia taratibu zinazowekwa na serikali visipodhibitiwa mapema vinaweza kuendelea kuzalisha madeni zaidi serikalini na hivyo wanaiomba serikali kukitupia macho chuo hicho.

Chuo hicho kilichoanzishwa Julai 29, 1961 na lengo kubwa likiwa kuwaandaa Waafrika kushika madaraka baada ya kung’oka wakoloni wa Kiingereza kikiitwa Kivukoni.

Kuasisiwa kwa chuo hicho lilikuwa wazo la Rais wa kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliyejipambanua kwa kuchukia vitendo vya ufisadi na watumishi wazembe wasiozingatia maadili ya kazi zao.

katika harakati za kupatikana uhuru wa Tanganyika, Mwalimu Nyerere alibuni wazo hilo la kuwa na chuo kitakachowafunza viongozi maadili ya umma na namna bora ya kutoa huduma kwa kuanza na makada wa chama cha Tanganyika National Union (TANU).

By Jamhuri