Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba amesema Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali kuhakikisha upatikanaji wa mafuta nchini unaendelea kuwa wa uhakika na bidhaa hiyo haiadimiki.
Akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Janeth Mahawanga Bungeni jijini Dodoma, aliyetaka kujua hatua zilizochukuliwa na Serikali katika kukabiliana na athari za migogoro ya kimataifa na kidunia zilizopelekea changamoto ya mafuta nchini.
“Hatua ya kwanza ambayo Serikali imechukua ni kuhakikisha bidhaa hii haiadimiki. Zipo nchi ambazo tayari matatizo yameshajitokeza ya bidhaa hiyo kuadimika, hata kama una fedha hupati mafuta,” amesema Dkt. Nchemba.
Waziri Mkuu amesema Serikali imeanza taratibu za kuweka ruzuku ili kupunguza makali ya athari zinazotokana na hali inayoendelea Mashariki ya Kati.
Aidha, amesema Serikali imekaa na kuwasikiliza wadau mbalimbali, wakiwemo wadau wa usafirishaji, kwa lengo la kujadiliana namna ya kudhibiti ongezeko la gharama za usafirishaji.
“Tulikubaliana na wasafirishaji kupunguza baadhi ya gharama zinazotokana na hatua zinazochukuliwa na Serikali ambazo kimsingi si za lazima. Mfano, ulikuwepo uratibu wa mabasi yote ya mikoani kupita kila stendi, tumesema hakuna ulazima wa basi kupita kila stendi,” amesema Waziri Mkuu.




