Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Mwandishi wa vitabu na mshairi Aisha Kingu ambaye pia ni Wakili Msomi, anatarajia kuzindua kitabu chake cha sita kiitwacho ‘Sing Gratitude’, kinacholenga kuhamasisha jamii kujenga utamaduni wa shukrani unaochochea mabadiliko chanya katika maisha jamii.

“Kitabu hiki kinalenga watu wa rika zote na kada mbalimbali, kuanzia vijana hadi wazee. Ni kwa ajili ya yeyote anayetaka kujifunza sanaa ya kuishi kwa furaha na kutosheka kupitia nguvu ya shukrani katika nyanja za kiuchumi, kijamii na kiroho,” alisema Wakili huyo Msomi.

Aisha, ambaye ameendelea kujizolea umaarufu kupitia kazi zake za ushairi kwa lugha ya Kiingereza, amesema anaamini sanaa ya uandishi ni nyenzo muhimu ya kuelimisha jamii pamoja na kuwahamasisha vijana kupenda kusoma, kuandika na kutumia vipaji vyao kwa maendeleo ya taifa.

“Uzinduzi wa kitabu hiki utafanywa na Mhe. Jaji Mkuu George Mcheche Masaju Katika Ukumbi wa Mlimani City Jumapili wiki hii (10 Mei, 2026) Amesema Bi. Aisha katika mkutano wake na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo.

Bi. Aisha amesema kupitia kitabu hicho wasomaji watapata nafasi ya kutafakari maisha yao kwa mtazamo chanya na kujifunza namna ambavyo shukrani inaweza kuwa chanzo cha furaha, matumaini na mafanikio.
Mbali na kitabu hicho kipya, Aisha tayari ameandika vitabu vingine vitano ambavyo ni Poetry Rebirth, Dear Paula, A Day with a Quote, pamoja na vitabu viwili vya United Nations 17 Sustainable Development Goals in English and Swahili, ambavyo vimepokelewa vizuri na wasomaji ndani na nje ya nchi.

Bi. Aisha ambaye ni kijana amejijengea utamaduni wa kusoma na kuandika tangu akiwa shuleni, huku akiwataka vijana kutumia sanaa na maarifa yao kuleta mchango chanya katika jamii.

“Vijana wanapaswa kujenga tabia ya kusoma, kuandika na kushiriki kutoa mawazo yenye kujenga jamii kupitia sanaa ya uandishi,” alisisitiza.

Akizungumzia zaidi kuhusu Sanaa ya uandishi na vitabu vyake, Bi Aisha amesema wazazi wake wamekuwa mstari wa mbele kumuunga mkono katika jitihada zake za kuandika vitabu vinavyolenga kutoa elimu na maarifa kwa jamii.