JK amchoka Nyalandu

*Atinga Marekani na msanii wa ‘Bongo Movie’

*Wabunge wamsubiri kumsulubu Novemba

*Safari, hoteli ghali zatafuna mamilioni ya shilingi

*Ofisi zake za wizarani ‘zakaribia kuota majani’

 

Na Mwandishi Wetu

 

Rais Jakaya Kikwete ameanza kuchoshwa na vituko vya Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, JAMHURI limethibitishiwa.

Habari za uhakika zinasema Rais Jakaya Kikwete sasa hana mpango mwingine isipokuwa kuchukua ‘uamuzi mgumu’ dhidi ya waziri huyo, anayekabiliwa na kashfa nyingi.

Miongoni mwa mambo ambayo rais anatajwa kukasirishwa nayo ni kitendo cha Nyaladu kutelekeza wizara pamoja na vikao vya Bunge Maalum la Katiba; na badala yake kuhamishia shughuli zake jijini Arusha, Marekani na Ulaya.

Nyalandu amekuwa akisafiri ndani na nje ya nchi huku gharama zote zikibebwa na taasisi zilizo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii. Ana vyumba maalum katika hoteli kadhaa za kitalii kwenye majiji ya Arusha na Dar es Salaam.

Inaelezwa kwamba imekuwa nadra mno kuonekana ofisini kwake Dar es Salaam; na hata anapotaka kuzungumza na waandishi wa habari, amekuwa akitumia hoteli za kitalii kwa gharama kubwa.

Chanzo cha habari kutoka kwenye msafara wa Rais Kikwete nchini Marekani, kimesema kiongozi huyo mkuu amekasirishwa na hatua ya Nyalandu kwenda nchini humo ‘kinyemela’ na kuendelea na shughuli zisizokuwa kwenye ratiba ya rais.

Katika ziara hiyo, Nyalandu anatajwa kwenda na mmoja wa wasanii wa Bongo Movie anayetajwa kuwa rafiki yake wa karibu.

“Rais yupo Marekani, kukawa na shughuli inayohusu ujangili na utalii. Mshauri mmoja akapendekeza Nyalandu awepo ajibu hoja; ndipo Rais aliposhtuka na kuhoji iweje waziri huyo awe Marekani wakati wenzake wanapambana bungeni kupitisha Rasimu ya Katiba.

“Lakini rais alionesha kutofurahishwa na Nyalandu anavyoiacha ofisi pamoja na mparaganyiko mkubwa wa kiuongozi ulioikumba Wizara ya Maliasili na Utalii,” kimesema chanzo chetu.

Hasira za rais zinatajwa kumfanya Nyalandu afunge safari haraka ya kurejea nchini mwishoni mwa wiki iliyopita. Lakini chanzo chetu cha habari kinasema Nyalandu amekuwa hana wasiwasi wowote wa kupoteza nafasi yake kutokana na kujiamini kwake kuwa yuko karibu mno na baadhi ya mawaziri waandamizi pamoja na Rais Kikwete mwenyewe.

Wakati hayo yakitajwa upande wa Rais Kikwete, kuna habari zisizotiliwa shaka kuwa wabunge kadhaa kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) na wengine kutoka Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni wanajiandaa kuibana mamlaka ya uteuzi kuhakikisha Nyalandu anang’olewa.

“Haiwezekani kashfa zote hizi zikawa zinaandikwa, hazikanushwi na bado huyu mtu anaendelea kuwa waziri. Tunasubiri Bunge la Novemba tuibane mamlaka ya uteuzi imuondoe. Huyu mtu hafai kuwa waziri. Tunataka tujue hiki kiburi anakitoa wapi?” amesema mmoja wa wabunge aliyesema ameanza kuandaa hoja ya kumng’oa waziri huyo.

Pamoja na Nyalandu, Naibu wake, Mahamoud Mgimwa, naye yuko kwenye hatihati kutokana na kukumbwa na kashfa ya ugawaji vitalu vya miti.

Kwa siku kadhaa sasa, vyombo vya habari vimekuwa vikiandika kashfa hiyo, huku Mgimwa akitajwa kuwa miongoni mwa wahusika wakuu ambao, ama wamejichotea, au wamefanikisha kuwasaidia marafiki zao kujipatia vibali vya ukataji miti kwa ajili ya mbao.

Kwa Nyalandu, idadi ya kashfa zinazomkabili ni kubwa mno. Kashfa ya karibuni ni mpango wake wa kuigomea Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma iliyoamuru kuhamishwa kwa baadhi ya watumishi wa Maliasili na Utalii.

Waziri huyo aliandika dokezo akiwazuia watumishi hao, akiwamo Paulo Sarakikya, kwenda walikopangiwa. Hadi wiki iliyopita, Sarakikya hakuwapo katika kituo chake kipya cha kazi.

Bado wachunguzi wa mambo wanashindwa kubaini nguzo inayompa jeuri Nyalandu, lakini kuna habari kwamba wanapata nguvu kubwa kutoka kwa mawaziri wawili wanaotajwa kuwania urais.

Kashfa nyingine inayomtikisa Nyalandu ni ya kutoa Leseni ya Rais kuua wanyampori 704; ‘zawadi’ ambayo aliwapa marafiki zake Wamarekani wa familia moja. Gazeti JAMHURI lilifanya kazi kubwa ya kuandika habari hizo na hivyo kufanikisha kuokoa wanyama hao 700.

Pamoja na habari hiyo, JAMHURI ilichapisha picha zilizowaonesha watoto wadogo wakiwa na bunduki wakiwinda katika kitalu kinachomilikiwa kihalali na kampuni ya Green Miles Safaris (GMS). Kifungu cha 43(3) cha Sheria ya Wanyamapori Namba 5 ya mwaka 2009 kinazuia watoto chini ya miaka 18 kuwinda.

Waziri Nyalandu amekiuka kifungu kinachoweka ukomo wa idadi ya vitalu ambao ni vitalu vitano kwa kampuni. Ameruhusu TGTS kumilikishwa vitalu vinane pamoja na eneo la wazi na hivyo kukiuka kifungu cha 38(7) cha Sheria ya Wanyamapori Na. 5 ya mwaka 2009.

Kwa kawaida kitalu chochote kinapobaki wazi, sharti kitangazwe kwanza na waombaji washindanishwe katika mfumo na utaratibu ulio wa haki na uwazi [Kanuni ya Uwindaji wa Kitalii 18(1)]. Pia amevunja sheria hiyo kwa kuruhusu uwindaji wa kitalii kufanyika eneo la Makao, sehemu ambayo haijatengwa kama kitalu.

Kashfa nyingine kwa Nyalandu ni mpango wake wa kusafiri kwenda nchini Afrika Kusini na kufanya mazungumzo na kampuni ya African Parks Network (APN) kwa ajili ya kuikabidhi uendeshaji wa Hifadhi za Taifa, Mapori ya Akiba na Mapori Tengefu.

Kwenye mpango huo, alishirikiana na mmoja wa wakurugenzi katika Bodi ya APN, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, James Lembeli.

Kwa mara nyingine, gazeti hili lilifichua kashfa hiyo na kwa sasa bado wanatafuta mbinu nyingine za kuuendeleza.

Kwenye mlolongo wa kashfa hizo, Nyalandu alikuwa na mpango wa kufungua mpaka wa Bologonja unaotenganisha Tanzania na Kenya ili kuruhusu watalii kutoka Kenya kupita eneo hilo. Mpaka huo ulifungwa wakati wa uongozi wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, kwa kuzingatia maslahi mapana ya kiuchumi ya Taifa.

Kwa mara nyingine, JAMHURI ilifichua mpango huo na kuchapisha nyaraka mbalimbali na hatimaye kufanikiwa kuuzima.

Waziri Nyalandu anakabiliwa na kashfa ya kujihusisha na ujangili mkoani Singida. Nyaraka ambazo JAMHURI inazo zinaonesha kuwa Juni 11, 2012 Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Mwanyonye, Rehema Manji, alimwandikia Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida akilalamikia kutishiwa kwa bastola.

Anasema, “Napenda kutoa taarifa ya kuvunjiwa geti/kizuizi cha mazao na kutishiwa kwa silaha aina ya bastola na mtu ndani ya gari Na. T505 BKM usiku wa kuamkia leo tarehe 11/04/2012 yaani saa 6.00 usiku katika eneo la Kijiji cha Mwanyonye na Kinyeto.”

Aliongeza; “Pia tumefungua kesi Na. IR/SI/1570/2012, aidha tangu usiku huo hadi sasa geti liko wazi na magari ya mizigo yanapita bila kukatiwa risiti za ushuru.”

Siku hiyo hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Singida alipokea waraka wa Meneja wa Mkoa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Singida, ukisema; “Nakiri kupokea barua yako ya tarehe 11/04/2012 yenye kumb.SDC/K.2/1/PART ‘E’/45 kuhusiana na somo tajwa hapo juu. Napenda kukufahamisha kwamba mmiliki wa gari Na. T505 BKM ni Ndugu Lazaro Samwel Nyalandu mwenye namba ya utambulisho wa mlipa kodi (TIN: 105-059-701).”

Barua hiyo ilitiwa saini na Mnubi kwa niaba ya Meneja wa Mkoa wa TRA Mkoa wa Singida. Pamoja na tuhuma hizo za ujangili, rekodi hazioneshi kama Nyalandu alishawahi kuwajibishwa kwa jambo hilo.