jakaya kikwete
jakaya kikwete
Kila kiongozi katika nchi yoyote ile duniani – iwe inafuata utawala wa kidemokrasia au wa mabavu – anapoondoka madarakani anakuwa na historia ya kukumbukwa kwa vyovyote vile kwa mabaya au mema aliyowatendea watu wake.

Hapa si kwa viongozi wakuu wa nchi tu bali kwa kila mmoja kulingana na utendaji wake wa kazi, akiwaongoza wengine katika majukumu mbalimbali ya kijamii na kitaifa.

Kiongozi wa familia (baba) naye hukumbukwa kwa uzuri na pia kwa ubaya wake na familia yake bila kujali yuko hai au ameshafariki. Historia yake itakuwa inaishi miongoni mwa jamii.

Siwezi kumsahau mwalimu wangu wa somo la hisabati na historia aliyenifundisha nikiwa Shule ya Msingi Maendeleo ya Jijini Mbeya, Mzee Mwangomile. Tulimwita babu, kwani alistahili kuitwa hivyo kutokana na umri wake na vilevile aliwafundisha hata baadhi ya wazazi wetu kabla ya Tanganyika kupata uhuru.

Mwalimu huyu alikuwa jasiri, mkakamavu asiyekubali uzembe wala mgawanyiko wowote wa kitabaka kati ya wanafunzi na walimu.

Siku moja kwenye miaka ya 1980 wakati wanafunzi tulipokuwa tunalima katika shamba la shule, wakati mvua inanyesha na walimu wakiwa wametusimamia wakiwa wamejifunika miavuli waliyokuwa nayo, nakumbuka  alitoa amri kwa walimu tuliokuwa nao shambani: 

“Hakuna mwalimu yeyote kujifunika mwavuli, hawa tunaowasimamia si wanyama.” Walimu wale walitii amri ile, tukaendelea na kilimo huku wote tukinyeshewa na mvua.

Kila shule aliyopelekwa aliweza kukabiliana na wanafunzi jeuri, walimu wavivu wasiotaka kufundisha, na wazazi wazembe waliokubaliana na utoro wa watoto wao. Shule alizoziongoza zilikuwa mfano wa kuigwa na shule nyingine kwa usafi na nidhamu ya hali ya juu kwa wanafunzi na ufaulu. 

Huyu amejiwekea kumbukumbu yake kutokana na utendaji wake. Wapo watu wengine waliojiwekea historia inayoakisi maisha yao kwa ubaya au uzuri wa utendaji wao. 

Leo tuzungumzie hili la viongozi wetu wakuu waliomaliza vipindi vyao vya uongozi na Rais Jakaya Kikwete anayemaliza muda wake mwaka huu.

Kwa upande wake, Mwalimu Julius Nyerere amejijengea heshima kubwa kwa Tanzania na katika jumuiya za kimataifa kwa kuwaunganisha Waafrika kwa pamoja na kuleta uhuru, umoja, utu na uzalendo wa kweli kwa Watanzania.

Mwalimu alikuwa mzalendo wa kweli ambaye hakukubali unyonge katika kukabiliana na mabepari, wala kuwa dalali wa kuuza rasilimali za nchi kwa wageni kama ilivyojitokeza kwa waliomfuata hasa Serikali ya Awamu ya Tatu na ya Nne.

Aliipenda nchi na Watanzania wote bila kuwa na ubaguzi wa namna yoyote ile, ndiyo maana watoto wake waliishi maisha sawa na wananchi wengine. Lakini ametofautiana na familia za watawala waliomfuata ambao wanakumbukwa kwa ubinafsi na matukio ya ufisadi.

Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, ameendelea kukumbukwa na wananchi kwa kuimarisha uchumi wa nchi katika kipindi chake cha uongozi mwaka 1995-2005, ambako alifanya jitihada za dhati kuhakikisha mfumuko wa bei unadhibitiwa na makali ya maisha yanapungua.

Rais Mkapa aliweka mikakati ya kweli kuhakikisha kila mwananchi anamudu mlo angalau mara tatu kwa siku. Na hilo tuliliona na atakumbukwa kwa hilo. Lakini hatuachi kumkumbuka kwa upande mwingine wa kuleta ulanguzi ndani ya Ikulu kwa kuanzisha kampuni akiwa mpangaji na kujimilikisha mgodi wa makaa ya mawe wa Kiwira mkoani Mbeya.

Watanzania tumezoea kumkumbuka mtu kwa mema yake baada kufariki kwake tu, na hili limechangia tuishi maisha ya unafiki wa kuwapamba watu hata kama hawastahili sifa hizo.

Rais Kikwete anayemaliza muda wake mwaka huu, atakumbukwa kwa mengi aliyowatendea Watanzania. Amekuwa mwepesi kushiriki katika matukio yanayowapata wananchi wake wa ngazi zote – iwe ugonjwa au msiba – tofauti na waliomtangulia licha ya Serikali yake kukumbwa na ufisadi wa kila namna.

Anawaacha Watanzania wakisubiri matumaini ya ‘maisha bora,’ ambayo yamekuwa njozi za mchana, huku makali ya maisha yakiongezeka kila kukicha. Kete moja ambayo ingempa kumbukumbu ya kudumu ni Katiba Mpya sawa na maoni yaliyotolewa na wananchi.

Angekumbukwa kwa Katiba mpya isiyochakachuliwa, kwa sasa sioni atakumbukwa kwa wema upi zaidi ya huo. Amesikiliza hila za CCM ambazo hazitaki mabadiliko, kwa kutumia Katiba mbovu kama mtaji wa kuendelea kuwatawala Watanzania.

Kwa kushinikiza Bunge la Katiba kujadili na kutengeneza Katiba ya CCM iliyoota mbawa baada ya kulaaniwa kila kona na Watanzania, amepoteza nafasi muhimu ya kukumbukwa kwa wema. Sasa Kikwete tutamkumbuka kwa lipi anapoondoka madarakani baada ya rais wa awamu ya tano kupatikana Oktoba 25, mwaka huu?

1435 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!