Ni mabadiliko kweli?

Watanzania hivi sasa tumo katika mtihani mgumu wa kujibu swali moja lenye vipengele vingi kuhusu mustakabali wa kuboresha maisha yetu na kudumisha Muungano wetu kwa upendo na amani.

Swali liliopo mbele yetu ni, Je, tunahitaji mabadiliko au kuking’oa tu Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilichopo madarakani ili tupate kuukabili mustakabali ujao? Ni hoja au ushabiki tu bila kupima mizania?

Nimesema kuna vipengele vingi kuhusiana na swali lenyewe. Inawezekana wewe au mimi hata yeye kila mmoja anaweza akawa na jibu lake tofauti na la kwako na la kwangu. Au wote tukawa na jibu moja lililo sahihi.

Ukweli utabaki palepale, tunataka mabadiliko. Kutaka mabadiliko ni jambo la kawaida kwa kila mtu. Bila mabadiliko mustakabali wetu katika maendeleo na maisha itakuwa shida kuonekana. Hapa tunaweza kuwa na swali ndani ya swali. Mabadiliko yepi tuyatakayo? 

Kwa sababu kuwa na barehe ni mabadiliko kutoka utotoni. Kufuja mali au fedha ni mabadiliko kutoka katika matumizi mazuri na makini. Vita ni mabadiliko kuoka kwenye amani. Mifano ipo mingi ya mabadiliko.

Mwaka 1995, Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alipigia chapuo dhana ‘mabadiliko’ na kuwatanabaisha viongozi nchini pamoja na kuwatetea wananchi, Watanzania kuwa wanataka mabadiliko.

Wanataka mabadiliko katika kupiga rushwa vita, kuondoa umaskini kwa wakulima na wafanyakazi, kukemea na kuzuia udini usitamalaki nchini, kuupuuza na kuuzuia ukabila kuwa ni kigezo kimoja wapo eti cha kujenga umoja, kupata ajira, cheo au madaraka ndani ya jamii.

Leo, imetimu miaka 20 (1995-2015). Hotuba ile kusikika katika masikio ya Watanzania. Kila Mtanzania ameielewa kwa maana yake na viongozi wetu wa vyama vya siasa na Serikali wameitafasiri  kwa maana zao!

Sikitiko kubwa liliopo ni mtoa hotuba au kauli hiyo, Baba waTaifa Mwalimu Nyerere hatunaye duniani na wala hakupata kuona kwa upana na kina chake, viongozi wetu wamepokeaje hotuba hiyo. Miaka minne (1995-1999) haikutosha kwake kupima utekelezaji na mafanikio yake!

Hivi sasa kila Mtanzania huenda akajiuliza, laiti Mwalimu Nyerere angekuwapo hali ya mabadiliko ingekuwaje? Mabadiliko tunayokusudia kuyapokea au yanayotakiwa na viongozi wetu ndiyo yale aliyeyasema na kuyataka Baba wa Taifa?

Kama jibu ni NDIYO. Nani hasa mfasiri au mudir makini wa hotuba ile hata sisi Watanzania tuweze kumfuata katika mabadiliko tuyatakayo? Kama jibu ni SIYO. Watanzania tufanye lipi tuweze kutii na kuenzi hotuba ile? 

Nadhani Watanzania tuna mila moja nzuri ya kutafakari kwa makini kauli za Baba wa Taifa ni vyema tukatumia mila hiyo kwa utuvu na makini wakati wa kuwasikiliza hao viongozi wanapojigamba wana muenzi na kumtafasiri Baba wa Taifa. Inthari iwekwe tulikotoka tulipo na kuendako. 

Jambo hilo ukweli linawezekana endapo wanaotaka kuongoza nchi hii wanabeba dhana za ukweli na haki, rushwa ni adui wa haki, yuko tayari kutumikia nchi hii na watu tuliyomo na kuahidi kuondoa  umasikini, ujinga na maradhi.

Dhana hizo zisiwe ni istilahi za kisiasa tu kutamkwa vinywani lakini rohoni na moyoni hazipo! Kwani hayo mabadiliko hayatakuwapo na badala yake ni fujo na vilio vya milele.

Kampeni zimeanza na ni wajibu na haki kwa Watanzania wapiga kura kupima na kuzingatia yasemwayo na wagombea majukwaani yanafanana na tabia, hulka na mwenendo wake kwa jamii. Tupime uasili wake katika utendaji tusipime uigaji wake katka utendaji.

Twendeni kwenye mikutano ya hadhara tukawasikilize na kuwachuja kabla ya kura zetu kufanya kazi tuikusudiayo ya MABADILIKO.