Machi 17 mwakani imepangwa kuwa tarehe ya kurejesha upya mafunzo ya kijeshi katika Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), kwa mujibu wa sheria ambayo Serikali iliyafuta mwaka 1992.

Katika awamu hiyo, vijana 5,000 watakaohitimu kidato cha sita Februari mwakani, watajiunga katika mafunzo hayo katika kambi za Mlale mkoani Ruvuma, Bulombora na Kanembwa (Kigoma), Oljoro (Arusha) na Masange mkoani Tabora.

 

Akiwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka 2012/2013 bungeni wiki iliyopita, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha, alisema mafunzo hayo pia yatawahusisha wabunge wote vijana wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

 

“Mheshimiwa Spika, nafurahi kuliarifu bunge lako tukufu kuwa wizara yangu imelifanyia kazi ombi hilo (la kurejesha upya mafunzo ya JKT kwa mujibu wa sheria), na kuandaa utaratibu wa mafunzo maalumu ya wiki tatu kwa waheshimiwa wabunge vijana,” alisema na kuwataka wahusika waorodheshe majina yao kwa ajili ya kufanyiwa maandalizi.

 

Nilipata mafunzo hayo ya kijeshi mara mbili kwa sababu nimetumikia majeshi mawili tofauti, hivyo nina ujuzi na uzoefu wa kutosha kuhusu jambo hilo na ndiyo maana ninapata wasiwasi na Nahodha.

 

Kwanza nilipata mafunzo ya awali katika Kambi ya 822 KJ, Masange, nje kidogo ya mji wa Tabora yaliyodumu kwa miezi sita, yale ambayo nilipohitimu nilipelekwa 821 KJ, Buhemba na kisha Rwamkoma, jirani kabisa na Kijiji cha Butiama, Musoma (sasa wilaya mpya ya Butiama) Mara, nilikokaa kwa miezi mitatu na kuhamishiwa 831 KJ, Mgulani jijini Dar es Salaam.

 

Baada ya kumaliza huko mwaka mzima nikiwa tayari nimepata mafunzo kikamilifu, bado nilipokwenda Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kila jambo likaanza upya.

 

Nilipata mafunzo mapya ya awali (ukuruta) kwa miezi sita mingine, safari hii nikiwa RTS Kunduchi, kilomita chache kutoka katikati ya jiji la Dar es Salaam, kisha nikahamishiwa Brigedi ya Tatu ya Vikosi vya Mizinga (3 KVM) – wakati huo – katika Kambi ya Jenerali Twalipo iliyopo mkabala na Uwanja wa Uhuru, Temeke.

 

Lakini badala ya kupelekwa huko, mimi na wenzangu tuliachwa palepale Kunduchi, tukapelekwa 342 KJ na kuchukua mafunzo magumu ya mizinga ya masafa marefu kwa miezi mitatu.

 

Kutoka huko nilianza kuhamishiwa vikosi mbalimbali jijini Dar es Salaam kama 34 KJ, 36 KJ, Makao Makuu ya Brigedi ya Chui, 310 KJ na kadhalika, na pia nilikwenda kozi ya uhandisi wa medani (field engineering), Chuo cha 121 KJ katika Kambi ya Sangasanga mkoani Morogoro, mbali na mafunzo mengine.

 

Nimelazimika kutaja baadhi ya mambo ili kuthibitisha uanajeshi nilionao. Nimejifunza kwata nikianzia JKT, utumiaji wa bunduki tofauti, mizinga ya masafa marefu, utegaji na uteguaji wa mabomu ardhini.

 

Wakati nilipokuwa kuruta katika kambi ya JKT kule Masange, Tabora, tulikuwa tukiamshwa saa 11 alfajiri kila siku na kukimbizwa mchakamchaka kwa kilomita angalau 10, tukarudi na kufanya usafi, na pia nimepata suluba zote za kijeshi na hivyo ninayajua vizuri mafunzo hayo yote.

 

Baadhi ya makamanda waliokuwa wakufunzi wetu huko ni Kapteni Juma Muhombolage, Luteni Mgonja, Luteni Usu Msengi, Sajenti Charles Sijale, Koplo Kikolokozi na Makoplo Usu Kazyoba, Elizabeth, Shilinde na Mwakajinga, angalau baadhi yao.

 

Lakini nilipokwenda JWTZ ulikuwa wakati mgumu kupindukia. Katika miezi yote sita ya mafunzo ya awali, mimi na makuruta wenzangu tulikuwa tukiruhusiwa kulala angalau kwa dakika 10 tu na kuamshwa, wastani ambao ni wa saa 30.4 tu katika kipindi hicho chote!

 

Siku zote tulikuwa tukiamshwa kati ya saa 8-9 usiku, muda ambao pia ndiyo tuliokuwa tunaruhusiwa ili kwenda kulala, lakini tukalalia vitanda vyetu kwa dakika 5-10 tu hivi na kuamshwa hadi tena kesho yake usiku saa kama hizo.

 

Kuanzia hapo hadi kunapokucha na mchana kutwa tulikuwa ni watu wa shughuli. Hatulali wala kupumzika, hatupati uhuru wowote wala hatuli tukashiba. Tulikuwa hatupewi hata muda wa kuoga, kufua sare zetu za mafunzo ambazo ni pamoja na bukta, fulana, shuka, soksi, blanketi, kofia na vifaa vingine.

 

Kubwa zaidi katika maisha yetu yote ya ukurata ni ukweli kuwa hakuna hata mmoja wetu aliyewahi kuvua nguo zake wakati wa kulala katika miezi sita yote.

 

Kila tuliporuhusiwa kulala, wote tulikwenda kujitupa vitandani bila kuvua bukta zetu, fulana zetu, soksi zetu na buti zetu kwa sababu hata sekunde moja tu ya kupoteza kufanya hivyo ilikuwa na thamani kubwa kiasi kwamba hakuna yeyote aliyekuwa tayari asiitumie kulala.

 

Pamoja na kupewa pia chandarua kila kuruta na kuifunga vizuri katika kitanda chake, kwa miezi yote sita ya mafunzo hayo ya awali hakuna aliyewahi kuifunga kutokana na sababu moja tu; ni afande gani angemngoja – iwe hata kwa dakika moja – eti akifunga neti yake tukiamshwa ile saa 8-9 kila usiku? Lakini pia, ni kuruti gani aliyekuwa tayari kupoteza hata sekunde moja ili aifungue na hivyo achelewe kulala?

 

Katika mafunzo hayo pia nawakumbuka makamanda wetu kama Meja Njogopa, Luteni Usu Komba, Afisa Mteule Daraja la Pili Mpalasinge na Makoplo Isaack Malyamungu (ambaye sasa ni marehemu), Kisura Chuma, Chacha na Katyetye. Kila afande ana sifa zake ikiwamo kutojadiliana chochote na kuruta yeyote ila kuonyeshana vitendo kwa maana ya ngondo tu!

 

Nikiwa katika JWTZ pia wakati wote ninapokwenda kozi kuanzia mizinga hadi uhandisi wa medani nilijifunza mambo mengi kutoka kwata kwa hatua zote, kufungua na kufunga silaha, kuzitumia kivita mbali na mazoezi lukuki ya kunijengea ukakamavu.

 

Nimekimbia mchakamchaka kwa umbali hadi wa nusu marathoni au sawa na kilomita 21, nimetembea usiku kucha barabarani na vichochoroni, nimepanda milimani, kushuka kwenye mabonde au miteremko ikiwamo mikali, nimelala kwenye majani, mahandaki na kukimbia huku na kule sehemu mbalimbali zikiwamo zinazotisha.

 

Mbali na mafunzo hayo wakati wa ukuruta pia nimetambaa juu ya kamba zilizofungwa kati ya nguzo mbili zilizopo umbali wa hadi mita 20 huku chini kukiwa na shimo refu na hatari. Nimetambaa chini ya nyaya za namna zote, maji machafu, kugaragara kwenye matope na hata kusimama kwenye mvua ili kutumikia adhabu au mazoezi ya ukakamavu wa mwili na viungo vyake.

 

Kila nikijiuliza kuwa eti wabunge wanapelekwa katika mafunzo ya JKT kwa wiki tatu, zile ambazo ni sawa na siku 21 tu, ninabaki kutafakari endapo wanakwenda jeshini kikwelikweli au kuwadanganya wananchi. Nashindwa kuelewa iwapo wanafanya hivyo kwa mujibu wa sheria au ni sehemu ya utani kwa watu wengine.

 

Endapo wanakwenda kuwatambia wakufunzi waliopo huko kuwa wao ni “waheshimiwa wabunge”, hapo nitamwelewa Nahodha, lakini sikubaliani kabisa na madai eti kwamba wanapelekwa huko ili kupata mafunzo ya kijeshi. Pengine wanachofuata huko ni semina za JKT!

 

Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa Simu Na. 0659 220 220 na 0762 633 244

2446 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!