JOSE CHAMELEONE

Mwanamuziki tajiri Uganda

Jose Chameleone yaelezwa kuwa ndiye mwanamuziki anayeongoza kwa utajiri nchini Uganda, akikadiriwa kuwa na utajiri unaofikia Sh bilioni 1.5 za Tanzania.

Aidha, anamiliki majengo ya thamani kubwa ya kukodisha (apartments), ziitwazo Daniella Villas, jijini Kampala na studio yake iitwayo Leon Island.

Mwanamuziki huyo ametajwa na takwimu za kifedha kuwa ana utajiri wa zaidi ya dola za Marekani milioni 5.

Katika orodha ya mali zake, pia anamiliki ufukwe uitwao Coco Beach, uliopo Barabara ya Entebbe nchini humo.

Jose Mayanja Chameleone, pia ana mikataba minono na kampuni zinazomtumia kutangaza bidhaa na huduma zake.

Moja kati ya mikataba yake iliyowahi kumtajirisha ni ile ya MTN na simu za Android.

Jose Chameleone ni jina la kisanii. Alipozaliwa mwaka 1976, wazazi wake walimpa jina la Joseph Mayanja, ambalo si geni miongoni mwa wapenzi na mashabiki wa muziki wa ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Chameleone alianza muziki mwaka 1996, kipindi hicho akiwa ‘DJ’ katika Ukumbi wa usiku wa Missouri uliopo Kampala.

Moja kati ya nyimbo zake za kwanza ulikuwa wa ‘Bageya’, aliomshirikisha msanii kutoka Kenya, Redsan.

Albamu yake ya kwanza ilitolewa nchini Kenya mwaka 1999. Tangu wakati huo aliachia albamu kadhaa zikiwa ni pamoja na ‘Bageya’ mwaka 2000, ‘Mama Mia’  mwaka 2001, ‘Njo Karibu’ mwaka 2002, ‘The Golden Voice’ mwaka  2003, ‘Mambo Bado’ mwaka 2004 na ‘Kipepo’ mwaka  2005.

Aidha, alishirikiana kufanya kazi na mwanamuziki mwenzake Bebe Cool, lakini baadaye waliibuka kuwa na upinzani mbaya.

Mtindo wa muziki anaocheza Chameleone ni mchanganyiko wa utamaduni wa Kiganda, rhumba ya Kati ya Afrika, Zouk na ragga.

Jose Chameleone ni mwanachama wa Jamii ya Mwanamuziki, muungano wa wanamuziki ambao hutumia umaarufu na mali zao kusaidia kuondoa umaskini na kujenga kampeni za mwamko wa virusi vya ukimwi.

Amezitembelea nchi nyingi za ng’ambo kufanya maonyesho, zikiwemo Marekani, Uingereza, Sweden na nyingine nyingi.

Aidha, alifanya ‘kufuru’ baada ya kuachia vibao vya ‘Jamila’, ‘Bei Kali’, ‘Mama Rhoda’ na nyingine nyingi vilivyo muongezea umaarufu.

Ngoma zake zingine ambazo zimewahi kutikisa kwenye soko la muziki barani Afrika ni ‘Wale Wale’, ‘Nkoleki’, ‘Vale Vale’, ‘Dorotia’, ‘Tubonge’, ‘Agatako’ na ‘Pam Pam’.