Imedaiwa kwamba kuporomoka kwa muziki wa dansi kumesababishwa na baadhi ya vituo vya redio zilizomo humu nchini kutokupiga muziki huo mara kwa mara.

Madai hayo yametolewa na mwimbaji nguli, Khadija Mnoga ‘Kimobitel’, ambaye ametamka kuwa nyimbo za bendi za zamani zina ujumbe wenye manufaa kwa jamii, wala haupotei.

Amezitaja baadhi ya bendi ambazo bado zipo kama Mlimani Park na Msondo Ngoma Classic, ambazo amesema kuwa zinafanya muziki wa dansi hadi leo na baadhi nyimbo zao hurindima katika vituo vichache vya redio.

Khadija amesema baadhi ya vituo hivyo vya redio vimeunyima nafasi muziki wa dansi tofauti na ilivyokuwa zamani na hicho ndicho chanzo cha kushuka kwa soko lao.

“Hakuna mchawi katika muziki wa dansi, bali baadhi ya vituo vya redio vilivyopo hapa nchini kwa makusudi  vimeamua kutozipa ‘air time’ ya kutosha nyimbo hizo,” anasema Khadija.

Wasifu wake

Khadija Mnoga alizaliwa Mwananyamala jijini Dar es Salaam, na kuanza elimu ya msingi katika Shule ya Mwongozo iliyoko Kinondoni jijini humo, ambako alimaliza mwaka 1995.

Khadija alijiunga na msomo ya sekondari katika Shule ya Navy Kigamboni. Alipokuwa shuleni hapo alikuwa mpenzi sana wa michezo na wala hakuwa na muonekano wowote wa kuwa na kipaji cha muziki.

Lakini mwishoni mwa miaka ya 1990, akajiunga na kikundi cha Chipukizi Mwananyamala cha CCM, ambako walianzisha kwaya. Hapo ndipo kwa mara ya kwanza alijijua kuwa anao uwezo wa kuimba, alipoona watu wanaanza kumsifu.

Diwani mmoja wa wakati huo, Ndege, ambaye ni marehemu hivi sasa, alikinunulia kikundi hicho sare kwa wanakwaya wote. Kikundi hicho kikawa rasmi, kikialikwa kwenye mikutano ya Chama Cha Mapinduzi.

Khadija Monoga kwa mara ya kwanza akaanza kufaidi kwa kutuzwa kitita cha pesa hata ikafikia Sh laki moja katika onyesho. Wenziwe katika vikundi hivyo vya chipukizi wakaanza kupandikiza mbegu ya kuanza kutamani kuimba kwenye jukwaa kubwa.  Khadija mwenyewe akaenda  kumwambia mama yake kuwa anajiona ana uwezo wa kuimba kwenye bendi.

“Mama hakuniunga mkono, pia hakunikataza, aliniangalia tu akacheka.” anasema Khadija. Jambo ambalo liko wazi, Khadija alikuwa na ndoto kamili za nini anataka kufanya katika maisha yake.

Kwanza, alikuwa amepanga kuwa hataanza kupiga muziki mpaka atakapopata mtoto, kwani aliamini atakuwa ‘busy’ sana na kujikuta anazeeka bila mtoto.

Kama alivyopanga, alipata mtoto wake wa kwanza lakini mtoto huyo alipomaliza kunyonya tu, kama bahati, mtu mmoja ambaye alikuwa mpiga ngoma wakati wako kwenye vikundi vya chipukizi, alimfuata na kumwambia kuna bendi inahitaji mwimbaji wa kike.

Alimkabidhi mama yake mtoto na kwenda kwenye mazoezi ya bendi kwa mara ya kwanza katika maisha yake bila hata kujua ni bendi gani anayokwenda.

Alifika kwenye nyumba moja karibu na taa za Jangwani na kukuta bendi ya Shikamoo Jazz, ndiyo iliyokuwa inahitaji mwimbaji wa kike.

Bendi ya Shikamoo ni bendi iliyoanzishwa mwaka 1994 kwa kukusanya wanamuziki wakongwe waliokuwa wamestaafu. Hivyo Khadija alianza muziki akiwa na walimu kama mzee Salim Zahoro, aliyetokea katika bendi ya Kiko Kids, Kapt. John Simon aliyekuwa katika bendi ya NUTA Jazz na mzee Majengo Bakari.

Wote walikuwa wakifanya mazoezi maeneo ya Buguruni nyumbani kwa mzee Waziri Nyange, aliyekuwa mpiga solo wa zamani katika bendi ya  Cuban Marimba  iliyokuwa ikiongozwa na Salum Abdallah.

Mwenyewe anasema walipoanza kumuimbisha wimbo kama ‘Wangu Ngaiye’, alidhani wametunga wao kwani hakuwa anazijua kabisa.

Baba yake Khadija alikuwa ni sheikh, aliiweka familia yake katika misingi ya dini yake ya Kiislamu, hivyo haikuwapo nafasi ya kusikia nyimbo hizo akiwa nyumbani.

Mababu hao walimlea vizuri sana Khadija, kwani pamoja na kujua kuwa hajawahi kupanda kwenye jukwaa waligundua ana kipaji, hivyo kumpa nauli kila siku ya kuja kwenye mazoezi na pesa kidogo ya kujikimu.

Wakati akiendelea na mazoezi, mpiga besi wa kundi la Young Star Taarab, Wana Segere, alibahatika kumsikia akiimba na moja kwa moja akaenda kuwaeleza wenzie kuwa kuna binti mmoja mdogo lakini muimbaji mzuri ila yuko kwenye kundi la wazee, Segere, wakaamua kufanya kila njia kumtoa kwa wazee na kumuingiza katika kundi lao.

Walimkaribisha awatembelee baada ya mazoezi yake, na Khadija alipokwenda huko akaambiwa kuwa kikundi hicho pia huimba nyimbo za taarabu, Khadija ambaye pia ana asili ya Zanzibar, alijisikia nyumbani zaidi katika muziki wa taarabu maana huo hata kwa baba yake ulikuwa  unasikika. 

Khadija alipofika hapo, haraka vyombo vilipangwa na wapigaji wakawa tayari, na akaulizwa anaweza kuimba wimbo gani wa taarabu, akawaambia kuwa yeye hajawahi hata kuwa jukwaani, lakini akaimba wimbo mmoja uliokuwa maarufu sana Zanzibar wakati huo uliokuwa na maneno haya: “Nafanya kwa raha zangu kwetu sigombwi, na nikigombwa napewa pipi, napewa pesa, na mobitel”.

Siku hiyo hiyo wakamkubali na wakamwambia usiku uleule atalazimika kupanda jukwaani kuanza kazi na kuimba wimbo huo mmoja. Kutokana na kuwa na wimbo  huo mmoja tu wa ‘Mobitel’ na hapo ndipo alipopatia jina la Kimobitel.

Kimobitel alisifika sana miaka ya nyuma akitamba katika bendi za African Stars ‘Twanga Pepeta’, Mchinga Sound, Double M. Sound na African Revolution ‘Wana Tam Tam’.

Kibao cha ‘Mgumba’ kilichotungwa na Muumin Mwinjuma wakiwa katika bendi ya African Revolution, Khadija Mnoga aliutendea haki kwa kuimba kwa hisia kali  wimbo huo na kumfanya kuwa mmoja kati ya waimbaji bora wa kike katika muziki wa dansi nchini.

Kimobite mweye asili ya Zanzibar, akifafanua kutokusikika katika muziki huo, amesema kuwa yupo katika bendi ya Sayari Stars, akiwa sambamba na wanamuziki waliowahi kutamba kama Rogart Hegga ‘Katapila’, Badi Bakule na wanamuziki wengine wengi.

“Mimi nipo jamani, wala sijapotea, kwa sasa nipo na bendi ya Sayari Stars pamoja na wanamuziki wenzangu Rogart Hegga ‘Katapila’, Badi Bakule, Emma Chokolate na wengine wengi tu. Bendi yetu imeweka makazi yake Manzese Tip Top, jijini Dar es Salaam,” anasema Kimobitel.

Hivi karibuni Khadija Mnoga alionekana kwenye Tamasha la 38  la Kimataifa la Sanaa na Utamaduni (TaS-UBa), lilliofanyika mjini Bagamoyo, akishirikiana na  bendi ya John Kitime JKF, inayomilikiwa na gwiji wa muziki wa dansi nchini, John Kitime.

Kitime ameunda bendi hiyo baada ya kupiga muziki katika bendi nyingi humu nchini, baadhi yake ni kama Super Matimila, Vijana Jazz na The Kilimajaro ‘Wana Njenje’ ambako amepiga muziki katika bendi ya Njenje kwa kipindi kirefu.

Makala hii imeandaliwa kwa msaada wa vyanzo mbalimbali.

Mwandaaji anapatikana kwa namba: 078433120, 0767331200 na 0713331200. 

By Jamhuri