King Kiki naye yupo kitandani

Kikumbi Mwanza Mpango, maarufu kwa jina la King Kiki au Bwana Mukubwa, kwa sasa haonekani majukwaani kutokana na maradhi ya uti wa mgongo yanayomsumbua kwa muda mrefu.

Taarifa hii inakuja wakati mkongwe mwingine wa muziki wa dansi nchini, Hassan Bitchuka, naye akiwa kitandani kwa maradhi.

Wote hawa wanahitaji msaada kutoka kwa Watanzania wenye mapenzi mema.

King Kiki hawezi kusimama wala kufanya lolote bila msaada, anatumia ‘wheel chair’, ni thawabu kwa mashabiki kwenda kumfariji na kumtia moyo azipokee changamoto za matibabu.

Tayari viongozi wakuu nchini, Rais Dk. John Magufuli na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, wamekwisha kumjulia hali, ama kwa njia ya simu au kwa kumtembelea nyumbani kwake Mtoni kwa Azizi Ali, jijini Dar es Salaam.

“Ni faraja sana kwangu na kwa wanaoniuguza. Waziri Mkuu ameniahidi kuwa serikali itagharamia matibabu yangu,” anasema King Kiki.

Januari 1, mwaka huu, Kiki ametimiza umri wa miaka  74 ya kuzaliwa. Hakika ni mkongwe.

Katika maisha yake yote kazi aliyoifanya tena kwa umahiri mkubwa ni muziki tu. Kazi hii imemnpa heshima na umaarufu mkubwa ndani na nje ya nchi.

Aliingia nchini akitokea Zaire (DRC) mwanzoni mwa miaka ya 1970 akiwa na Orchestra Fouvette na tangu wakati huo amekuwa mkuzi, mwalimu na mlezi wa vipaji vingi vya muziki.

Kiki alizaliwa Januari 1, 1947,  Lubumbashi, DRC.

“Mimi ni mtoto wa tano kwa wazazi wangu Katambo Wabando Paulino na mama yangu ni Mwanza Jumban,” anasema Kiki.  

Akiwa shuleni, darasa la tano, Kiki na wenzake watatu walianzisha kikundi cha muziki wa dansi; wakiimba na kucheza kiasi cha kukubaliwa na uongozi wa shule na kualikwa katika kila sherehe shuleni kwao.

Sifa zao zikazagaa mitaani hasa kutokana na umri wao na ukubwa wa ‘kazi’ waliyokuwa wakiifanya.

“Hata wakazi wa jirani na shuleni kwetu walikuwa wanatualika kwenye shughuli zao ingawa ilikuwa ni bure,” anasema King Kiki.

Mbali na muziki, Kiki alikuwa kichwa darasani, akishika nafasi za juu kwenye mitihani yote.

Akiwa na umri wa miaka sita tu, Kiki alibahatika kuhudhuria onyesho la mkongwe wa muziki wa Afrika Kusini, Miriam Makeba, na kwa hakika mama huyu ndiye aliyemvutia kuupenda muziki.

“Kumbukumbu ya Miriam haikunitoka tena akilini,” anasema Kiki aliyepelekwa kwenye onyesho hilo na kaka yake.

“Nimezunguka nchi nyingi kufanya muziki, nimeona shoo nyingi za kimataifa lakini hakuna aliyevunja rekodi ya kile nilichokiona kwa Miriam Makeba,” anasema.

Akiwa bado masomoni, mwaka 1958 alianzisha kikundi cha Bantu Negro kilichoubadili muziki wa Afrika Kusini kuwa muziki wa rhumba.

Aliachana na masomo mwaka 1962 na kujiunga na Norvella Jazz, bendi iliyomfikisha Kasai (Mbudji Mai) na kupaunua uzoefu wake kwa kukutana na wanamuziki mahiri kutoka Kinshasa.

Hata hivyo, wazazi wake hawakupenda awe mwanamuziki, hivyo kuwa kizingiti kikubwa katika safari yake ya sanaa.

“Hata kaka yangu alikuwa akinifunga kamba nyuma ya baiskeli na kuniburuza umbali mrefu kama adhabu ya kutokwenda shule. Lakini yote hayo hayakusaidia,” anasema.

Kiki na mwanamuziki mwingine maarufu nchini, Fred Ndala Kasheba, walikutana kwa mara ya kwanza huko Katanga, DRC mwaka 1968 katika bendi ya Orchestra Fouvette.

Ni bendi hiyo ndiyo iliyowaleta wakubwa hao nchini kwa mara ya kwanza miaka ya 1970 mwanzoni.

Kiki alihamia rasmi Tanzania mwaka 1977 baada ya kufuatwa na Chibangu Katayi ‘Mzee Paul’ na kujiunga na bendi ya Maquis du Zaire ya jijini Dar es Salaam.

Kutoka DRC, Kiki aliongozana na Nkashama Kanku Kelly, Mutombo Sozy na mpiga besi gitaa maarufu wa Maquis, Ilunga Banza ‘Mchafu’; bila kumsahau mnenguaji, Ngalula Tshiandanda.

Kiki ndiye muasisi wa mtindo maarufu wa Kamanyola ulioacha urithi wa jina la kituo kimojawapo cha daladala katika Barabara ya Shekilango, Sinza.

“Kamanyola ni mji huko DRC. Nilibuni mtindo wa uchezaji wa taratibu na kuuita ‘Kamanyola bila jasho’, kwamba unacheza kwa kujidai,” anasema Kiki.

Miongoni mwa vibao maarufu vilivyotungwa na King Kiki ni ‘Nimepigwa Ngwala’, ‘Kiongo’, ‘Kyembe’, ‘Sababu ya Nini’ na ‘Krisimasi Bonane’.

Wanamuziki alioshirikiana nao wakati huo ni akina Mbuya Makonga ‘Adios’, Mutombo Lufungula ‘Audax’, Mukumbule Lolembo ‘Parashi’, Kasongo Mpinda ‘Clyton’, Mbombo wa Mbomboka, Tshimanga Kalala Assosa, Kiniki Kieto, Masiya Radi ‘Dikuba Kuba’, Issa Nundu na Tabia Mwanjelwa.

Baadaye Kiki akajiunga na Orchestra Safari Sound (OSS) iliyokuwa na makao yake Kimara Resort na kukutana na akina Skassy Kasambula, Monga Stani Liki, Mobali Jumbe, Kalala Mbwembwe, Tshibanda Sony na Kabeya Badu.

Huko akaibuka na mtindo wa ‘Masantula Ngoma ya Mpwita’ na kushiriki kuimba na kutunga nyimbo kama ‘Mimi Msafiri’, ‘Mama Kabibi’ na nyingine nyingi, kabla ya kuanzisha bendi yake ya King Kiki Double O, iliyokuwa ikitumia mtindo wa ‘Embalasasa’.

Mwaka 1994 akaungana na Kasheba kuunda bendi ya Zaita Musica iliyopata umaarufu kwa wimbo wa ‘Kesi ya Kanga’ na ni hapo ndipo mtindo wa ‘Kitambaa Cheupe’ ulipozaliwa.

Mtindo huu umeipa umaarufu mkubwa bendi ya La Capitale (Wazee Sugu) aliyoiunda mwaka 2003, baada ya kifo cha Kasheba.

Mwaka 1977, Kiki alipata uraia wa Tanzania baada ya kuishi nchini kwa miaka mingi.

Alisema kuwa huenda bendi hiyo ndiyo atakayozeekea nayo, usemi huo yawezekana ukatimia kufuatia maradhi yanayomsumbua hivi sasa.

Bwana Mukubwa Kikumbi Mwanza Mpango ‘King Kiki’ ni baba wa watoto kadhaa, huku binti mmoja pekee ndiye aliyefuata nyayo zake.

Mbali na Kiki na Bitchuka, wakongwe wengine wa muziki ambao afya zao zimedorora kwa sasa ni Salim Zahoro, Hussein Jumbe na Rashidi Pembe.

Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa simu namba: 0784331200, 0736331200, 0713331200 na 0767331200.