Katika toleo lililopita tuliishia katika aya isemayo: “Tumuachie Mungu, Paul ni mtu anayejitambua, kama yuko hai atakuja,’’ alisema baba yake Paul, japokuwa kauli hiyo  ilikuwa  na hisia ya kukata tamaa ndani yake, akihisi mwanae pengine alikuwa amekufa au ametekwa na watu wenye nia mbaya. Endelea…

“Kaka atakuwa amepatwa na nini siku hizo zote?’’ alisikitika mdogo wake Paul huku machozi yakimlengalenga machoni. “Hakuna namna,’’ aliendelea kutoa majibu baba yake yaliyokuwa yamegubikwa simanzi.

Matumaini ya Paul kusoma katika chuo kikubwa na chenye hadhi ilikuwa ni baada ya masomo apate kazi na kuisaidia familia yake. 

Haikuwa kwake tu, bali hata kwa baba yake, alijua Paul angekuja kuiinua familia kutoka katika umaskini waliokuwa nao. 

“Ng’ombe wa maskini hazai,” ulikuwa msemo wa Paul mara nyingi alipokuwa akikaa mwenyewe na kujisemea.

Punde akafika rafiki yake Paul aliyesoma naye kidato cha sita, Shule ya Sekondari ya Tosamaganga iliyopo Mkoa wa Iringa nchini Tanzania.

Alikuwa anaonekana kukata tamaa katika maisha yake. “Baba shikamoo!!!’’ alimsalimia baba yake Paul. Charles alikuwa mtaaluma katika uchumi. “Bado haujafanikiwa kupata kazi?’’ aliuliza baba yake Paul.

 Charles alijibu na kusema ukweli pasipo kuficha: “Bado, ila kwa sasa ninakata mkaa na kuuza mjini.’’ Kauli  hiyo iliwashangaza baba na mdogo wake Paul.

 “Usomi wote huo mnaishia kuuza mkaa!’’ Ilimshangaza baba yake Paul. “Kwanini inakuwa hivyo?’’ aliuliza mdogo wake Paul. 

Charles alijibu kwa unyonge: “Kazi ni ngumu kupata. Ajira hazipo.’’ Baba yake Paul na mdogo wake ilikuwa vigumu kwao kuelewa.

****

Paul alitembea kwa miguu mitaani, alikuwa hana woga, kwa kuwa ilikuwa vigumu kutambua kama si raia wa Kenya. Jinsi alivyokuwa akivaa ilikuwa vigumu kumtambua kuwa aliishi maisha ya kubahatisha.

“Mungu nifanikishe niweze kupata kazi,’’ aliwaza Paul akiwa anatembea. Aliingiwa kumbukumbu namna alivyokuwa chuo kikuu.

“Nikimaliza chuo kazi itapatikana tu ili niwasaidie nyumbani,’’ alijisemea mwenyewe. Paul alikuwa na rafiki yake aitwaye Ramso, naye aliendelea kuongea:

 “Hatuwezi kukosa kazi ilhali tuna shahada.’’ Alipokuwa akizungumza na rafiki yake Ramso walikuwa wameketi kwenye vimbweta chuoni, wakiwa wameshikilia kompyuta mpakato huku pembeni wakiwa na vinywaji baridi. Paul aliendelea kufikiria namna maisha ya chuo yalivyo mfanya kuwa na matarajio makubwa.

 “Kumbe sikujua kama mitaani pako tofauti,’’ aliendelea kuzungumza mwenyewe huku akitembea na kujikuna kichwa kutokana na msongo wa mawazo aliyokuwa nayo.

Philemon naye alikuwa mitaani akisaka makopo. Aliamua kujitoa pamoja na kuishi katika banda lakini alikuwa ni mtu mwenye matumaini. “Rafiki wewe ni Mkikuyu?’’ aliulizwa na muokota makopo mwenzake aliyekuwa amekutana naye.

“Hapana, mimi ni Mtanzania,’’ alisema ukweli Philemon.

Philemon alizaliwa Mkoa wa Mbeya, asili ya kabila lake alikuwa Mnyakyusa wa Kyela, wazazi wake walikuwa wakulima wa mpunga, wakiwa hawana elimu yoyote,  hawakubahatika kupelekwa shuleni na wazazi wao.

“Hapa Nairobi unaishi wapi?’’ alimuuliza huku akimtazama usoni. “Ninaishi Kariobangi,’’ Philemon alisema. Yule Mkenya hakuwa na kiwango kikubwa cha elimu ila alikuwa mtu mwenye maarifa mengi.

“Kwanini uliamua kuja Kenya?’’ alimuuliza Philemon. Waliongea huku kila mmoja akiokota makopo jalalani.

 “Ni namna tu ya kutafuta maisha, muda mwingine unaweza kuwa mkimbizi ndani ya taifa lako,’’ maneno hayo yaliyomtoka Philemon na kuonekana kumgusa yule kijana Mkenya ambaye maisha yake yalikuwa magumu. Alikuwa na elimu ya udereva, alitafuta kazi lakini hakupata. 

“Ni kweli rafiki yangu,’’ alisema yule Mkenya huku akimpa mkono, kichwani alivaa kofia chafu. Mbele yao walipita mabinti wazuri, nywele zao zikiwa zinavutia, mikononi walishika bahasha za kaki. 

“Tazama wale pia wamo ndani ya taifa lao la Kenya lakini ni kama wakimbizi,’’ alisema Philemon, maneno yaliyomvutia kijana yule Mkenya, mzaliwa wa Kisumu.

Walipomaliza kuokota chupa za maji, kazi ambayo ilichukuliwa na watu wa Kenya kama kazi dhaifu na isiyo rasmi, wakaenda pembeni kuendelea na mazungumzo.

 “Mimi nimehangaika hapa Kenya lakini bado sijafanikiwa, wewe utaweza?’’ Yule Mkenya alimuuliza Philemon.

 Philemon alijibu kwa kujiamini: “Naweza, maana maisha haya ni fursa mtu anazokutana nazo.’’ Philemon alisema lakini akilini mwake akiwaza ataishi vipi na atapataje fedha za kulipa kodi ya banda walimokuwa wakiishi.

 “Ni sawa, ngoja mimi niwahi kiwandani,’’ alizungumza yule kijana Mkenya huku akitengeneza sandarusi lake vema.

Itaendelea …

795 Total Views 4 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!