TABORA

Na Moshy Kiyungi

Unenguaji ni chachu na kivutio katika muziki wa dansi na hata muziki wa Injili.

Huenda mwaka 1973 ndiyo ilikuwa mara ya kwanza Tanzania kushuhudia umahiri wa unenguaji jukwaani.

Wakati huo TP OK Jazz ya DRC chini ya Franco Lwambo Lwanzo Makiadi ilifanya onyesha kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam na baadaye Arusha, maonyesho ambayo wanenguaji walichangamsha vema umati.

Mwaka 1977, Mbilia Bell, akiwa na umri wa miaka 17, aliacha shule na kujiunga na kundi la Abeti Masikini kuwa ‘mcheza show’ (mnenguaji).

Fally Ipupa naye alipitia unenguaji kabla ya kuwa mtunzi na mwimbaji maarufu hadi kumiliki bendi ambayo takriban wanamuziki wake wote wana uwezo mkubwa wa kunengua!

Bileku Mpasi alichukuliwa na Kabasele Yampanya ‘Pepe Kalle’ kama mnenguaji wa Empire Bakuba, akiwaongoza wanenguaji ‘mbilikimo’, Emollo na Jolly Bebe.

Baada ya kifo cha Pepe Kalle, Bileku aliunda bendi ya Orchestra Big One, akiwa na wanenguaji Jolly Bebe na Djuma Fatembo.

Tanzania wapo wanenguaji kama Super Nyamwela aliyeanza kazi hiyo tangu akiwa shule ya msingi, akifanya maonyesho katika Baa ya Macheni, Magomeni Mapipa.

Leo tunamtazama Jolly Bebe, mnenguaji maarufu aliyezaliwa Matadi, DRC akiwa mtoto wa nne kati ya sita, akibatizwa kwa jina la Josephine.

“Mimi si mbilikimo, hapana. Ndugu zangu wote wana kimo cha kawaida. Isipokuwa nikiwa mtoto, niliugua maradhi yaliyoathiri ukuaji wangu,” anasema Jolly.

Kwa maana hiyo anasema hali aliyonayo ni ulemavu na kwamba akiwa shuleni alichekwa sana na kukasirika.

“Walionicheka walijuta kwa kuwa nilianzisha ugomvi mkubwa. Hakuna wa kuamua,” anasema Jolly Bebe akishukuru Mungu kwa kumpa akili na viungo vingine kama binadamu mwingine yeyote, hivyo kuweza kujitegemea.

Anasema akiwa mtoto alikuwa kipenzi kwa familia, lakini kuna siku alicharazwa bakora na baba yake baada ya kutoroka nyumbani usiku kwenda kushuhudia mpambano wa mieleka, mchezo anaoupenda sana.

“Siku ile baba hakulala. Akasubiri hadi niliporudi nyumbani. Mwenyewe nikaingia kwa kunyata, kumbe baba yupo sebuleni! Akanidaka na kunipa kichapo ambacho siwezi kukisahau,” anasema.

Mapenzi yake kwa muziki yalianza alipojiunga na kundi la mieleka la ‘Catch’, ambapo kundi la wasanii lilitumika kuishangilia na kuihamasisha timu ya mieleka pembeni mwa ulingo.

Ni katika safari za kundi hilo kutoka Matadi kwenda Kinshasa ndipo alikokutana na Pepe Kalle, shabiki mwenzake wa masumbwi na mieleka. 

“Aliniona wakati tukiwahamasisha wapiganaji wetu. Nilikuwa ninafanya vimbwanga si mchezo. Akavutiwa nami,” anasimulia namna alivyokutana na Pepe Kalle.

Anasema: “Miezi kadhaa baadaye tukiwa safarini kwenda Kongo Brazzaville, tukiwa bandarini tukisubiri kuvuka, kumbe Pepe Kalle na Empire Bakuba nao walikuwapo.”

Anasema awali hakuwa akimfahamu Pepe Kalle hadi alipoitwa kwa ajili ya mazungumzo na kuombwa ajiunge nao ili afanye kazi na Emollo.

Lakini waliporejea Matadi, hakumsikia tena Pepe Kalle, akaamua kwenda Kinshasa kumtafuta na kumkumbusha mazungumzo yao.

Akaondoka nyumbani bila kuaga, akiwa Kinshasa, akafikia kwa rafiki yake, Marie Claire. Kazi ya kutafuta anakoishi Pepe Kalle ikaanza mara moja.

“Kwa kawaida nilikuwa ninakasirika sana watoto wakinifuata kushangaa ufupi wangu, lakini siku hiyo nikawa nina furahi sana. Nikaona kama jambo la kawaida tu,” anasema Jolly.

Nyumbani kwa Pepe Kalle, walimkuta mkewe, Mama Paulina, akawaambia kuwa mzee amekwenda Ulaya kwenye shughuli za muziki, akamuomba amuachie mawasiliano.

Akiwa bado Kinshasa nyumbani kwa Marie Claire, siku moja wakaona taarifa kwenye runinga kwamba Pepe Kalle yupo jijini humo.

“Mara moja tukaenda nyumbani kwake na kumkuta akiwa na Papy Tax na Djuna Mumbafu ‘Bileku Mpasi’.

“Pepe Kalle aliponiona alifurahi sana. Akamuagiza mmoja wa maofisa wake anipige picha kwa ajili ya pasipoti.

“Nikawa nimejiunga nao na ndani ya mwezi mmoja tu tayari tulishafanya maonyesho Abidjan, Ivory Coast na kwingine kwingi,” anasema.

Jolly Bebe akawa nyota wa kimataifa. Anasema akajiona ameikamata dunia na wala hajui amepanda ndege mara ngapi!

“Paris nilifika kwa mara ya kwanza mwaka 1992. Onyesho lilifana na nilituzwa zawadi nyingi mno,” anakumbuka.

Anamtaja Pepe Kalle kama bosi mchapakazi siyetaka mchezo; kwamba hukasirika mtu akichelewa mazoezini.

Anasema ingawa amewahi kusikia watu wakidai Pepe Kalle alikuwa akiwatumia yeye na Emollo kwa ushirikina, hajawahi kuona masuala ya kishirikina kwa bosi wake au ndani ya Empire Bakuba.

“Mengi yalizungumzwa kuhusu Pepe Kalle na ushirikina, yote hayana msingi. Ukweli ni kwamba alikuwa mtu wa mikakati na uwepo wangu na Emollo pale Empire Bakuba, uliimarisha sana kikosi na kuvuta mashabiki wengi,” anasema.

Akizungumzia kifo cha Emollo nchini Botswana, anasema baada ya onyesho moja lililohudhuriwa na watu wengi, Emollo alisema hajisikii vizuri akaomba apelekwe hospitalini.

“Akapelekwa lakini muda mfupi tu, tukaambiwa amefariki dunia. Kifo chake kiliniletea huzuni kubwa. Kwanza, hakuwa anaumwa; halafu tupo ugenini!

“Nikatamani hata mimi nife tu. Tulikuwa tumezoeana sana na kushirikiana katika unenguaji. Lakini pamoja na kuwa mimi ni mfupi, Emollo alizidi. Ili apande mgongoni wakati wa shoo, nililazimika kuchuchumaa,” anasema kwa kicheko cha utani.

Jolly anawashauri mabinti wanaojishughulisha na unenguaji kufahamu kwamba hiyo ni kazi kama nyingine, muhimu ni kujiheshimu.

“Ukijiheshimu na wengine watakuheshimu. Tutunze maadili ya Kiafrika kwa nguvu zote,” anasema.

Josephine ‘Jolly Bebe’ ni mama wa familia ya mume na watoto kadhaa na bado yupo jukwaani akiendelea na kazi ingawa umri unasogea mbele.

Kwa sasa yupo na Orchestra Big One, bendi inayomilikiwa na Bileku Mpasi.

Makala hii imeandaliwa kwa msaada wa vyanzo mbalimbali.

Mwandaaji anapatikana kwa namba: 0713331200, 0784331200, 0736331200 na

0767331200.

510 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!