Home Habari Mpya Messi na ukurasa wa mwisho Camp Nou

Messi na ukurasa wa mwisho Camp Nou

by Jamhuri

DAR ES SALAAM

Na Mwandishi Wetu

Kila zama na kitabu chake. Kila nabii na kitabu chake. Hii ni misemo maarufu katika jamii na hutumika mara kwa mara.

Messi naye ana kitabu chake katika Klabu ya Barcelona na soka kwa ujumla wake. Na sasa ukurasa wa mwisho wa kitabu cha Lionel Messi na Barcelona umefungwa wiki iliyopita kule Catalunya.

Ni majonzi. Majonzi. Majonzi kwa mashabiki wa klabu hiyo na wapenzi wa soka duniani.

Kwa kusema ukweli zama za Messi pale Barcelona zimemalizika kikatili sana. Kitabu kimefungwa. Katika ukurasa huu kama wiki tatu hivi zilizopita, nilitabiri kutokea kwa hali hili. Ilikuwa ikionekana wazi kwa wafuatiliaji wa masuala ya soka.

Wazungu hawana maisha ya shukrani kama tulivyo sisi Waafrika. Wao ni biashara, fedha na faida tu.

Mwisho wa Messi na Barcelona umekuwa mwepesi sana. Chama cha Soka cha Hispania kinatupa mzigo wa lawama kwa klabu na uongozi wa Barcelona wakati Barcelona wenyewe wanatupa mzigo wa lawama kwa chama hicho cha soka.

Ni lawama kila upande! Kila mmoja anamlaumu mwenzake.

Kila mmoja anasema na atasema la kwake analoliamini, lakini kwa ufupi tu umri wa Messi umeshakimbia, halafu hana maajabu mengi katika miguu yake.

Hii ndiyo sababu hasa, lakini wakubwa wameshindwa kutuambia au kuisema hadharani.

Kuwa na Messi huyu mwenye umri wa miaka 34 ni gharama kubwa kikosini mwako. Wazungu umri ukishasogea hawajipi sana muda wa kutazama yaliyopita. Wanakuacha ulivyo na wao wanasonga mbele.

Messi ni muungwana. Aliupunguza hadi mshahara wake ili aendelee kusalia katika timu aliyoipenda tangu akiwa mtoto, lakini bado haijatosha.

Kwa macho makavu kabisa ameambiwa atafute ‘changamoto’ nyingine mpya nje ya Barcelona.

Unadhani Messi wa miaka 30 kushuka chini angeonekana mzigo kwa Barcelona kama ilivyo sasa? Huu ni mwisho wa zama zake. Hakuna kitakachobadilika zaidi ya kuwaaga watu aliokuwa nao tangu alipokuwa mvulana mdogo mpaka sasa baba mwenye mke na watoto.

Inachekesha na kufikirisha kwa namna fulani ukimsikia Rais wa Barcelona, Joan Laporta, alipokuwa akizungumza juu ya jambo hili.

Anasema: “Kila kitu kinachohusiana na kuondoka kwa Messi wakuwajibishwa ni kanuni za Bodi ya La Liga. Hata kama tungekubaliana naye, tusingeweza kurasimisha usajili wake kutokana na kanuni hizo kutubana.”

Huyu ndiye Laporta ambaye moja ya ahadi zake alipokuwa anaomba kura kwa wanachama wa Barcelona hivi karibuni ni kusema atahakikisha Messi anaendelea kubaki Barcelona.

Laporta anaendelea kusema: “Tulikubaliana naye mkataba wa miaka mitano na tulikuwa tunakwenda kumlipa miaka miwili ya mshahara wake. Messi alikubaliana na jambo hilo. Tuliamini tulifuata kanuni za shirikisho, lakini La Liga hawakuruhusu jambo hilo.

“Tumehamasika zaidi ya tulivyokuwa huko nyuma. Barcelona itaendelea kung’ara kwenye ulimwengu wa soka hata bila ya uwepo wa Messi, ninaamini kizazi kipya cha bila ya Messi kitafanikiwa sana.

“Siku mbili nyuma, tuligundua tusingeweza tena kuongeza mkataba naye kutokana na vikwazo vya kanuni, tulifanya kikao chetu cha mwisho na Messi na baba yake (ambaye ndiye wakala wake). Messi alitaka kubaki.

“Kwa mujibu wa hesabu zetu, tuna uwezo wa kuruhusu ujio wa Eric García, Memphis Depay na Sergio Kun Agüero kwenye kikosi chetu. Naamini hatuna tatizo kwenye hilo.

“Kanuni katika tasnia ya soka zinahitaji bajeti ya mishahara kwa timu zote ziwe kati ya asilimia 65 hadi 70 ya mapato. Mpaka dakika hii bajeti yetu ya mshahara ni asilimia 95 ya pato letu.”

Kila la heri Messi kokote utakakokwenda. Historia ya soka itakuenzi daima.

You may also like