pg 1Sakata la sukari likiwa halijatulia, wafanyabiashara wakubwa wanatajwa kujipanga kumtikisa Rais John Magufuli, kwa kuhakikisha mafuta ya kula yanaadimika nchini.

Tofauti na kwenye sukari, uhaba wa mafuta umepangwa mahsusi ili kujenga ushawishi wa wao kuendelea kuingiza mafuta ya kula ya mawese bila kulipia ushuru.

Habari za uhakika zinaonesha kuwa tayari viongozi waandamizi katika wizara tatu ‘wameshawekwa sawa’ ili kuhakikisha ushuru hauwekwi kwenye mafuta hayo.

Wizara zinazotajwa kusuka mpango huo ni za Kilimo, Mifugo na Uvuvi; Viwanda, Biashara na Uwekezaji; na Wizara ya Fedha na Mipango.

Ingawa Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mwigulu Nchemba, hahusishwi moja kwa moja, kauli yake ya wiki iliyopita bungeni kuwa nchi haijitoshelezi kwa mafuta ya kula kwa hiyo yataendelea kuagizwa kutoka nje, inajielekeza kwenye mkakati wa kuwahakikishia wafanyabiashara mwanya wa kuendelea na biashara hiyo.

Uchunguzi uliofanywa na JAMHURI umebaini wafanyabiashara wanaoongoza vita hii ya kukwamisha ushuru kwenye mawese, wengi wao ni wale wale wanaoagiza sukari kutoka nje ambao baadhi yao wameitikisa nchi kwa kusababisha uhaba wa bidhaa hiyo.

Katika vikao vyao, wafanyabiashara hao wamejipanga vilivyo kukwamisha ushuru kwenye mafuta hayo, kwa kiwango cha asilimia 10 kama ilivyokuwa ikitarajiwa.

Badala yake wameishauri Serikali kupitia watetezi wao, igeukie Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ili ikiwezekana ndiyo iondolewe kwa wenye viwanda vya kusindika mafuta yanayotokana na mawese hapa nchini. Mkakati huo umebuniwa kama kiinimacho ili ionekane wakulima na wenye viwanda watafaidi, jambo ambalo ni kinyume cha uhalisia wa mambo.

Kadiri sekeseke hili linavyoendelea, kuna dalili za wafanyabiashara kushinda vita hii na hivyo kuiona Bajeti ya Serikali ya Mwaka 2016/2017 ikipita bila kuwekwa ushuru kwenye mafuta ya mawese.

“Wameshaweka mazingira kuonesha kuwa mafuta ya kula nchini ni shida. Tayari kuna mawaziri wamejitokeza kutetea kile wanachosema uhaba wa mafuta ya kula upo nchini na kwa maana hiyo wanataka yaendelee kuagizwa. Lakini wanakolenga si kuruhusu au kuzuia mafuta, bali ni kuhakikisha ushuru hauwekwi kwenye mafuta ya mawese. Vita hii ni kubwa pengine kuliko ile ya sukari,” kimesema chanzo chetu na kuongeza:

“Unaondoa VAT ili iweje! Hii haina nafuu kwa mlaji wala kwa mkulima. Hii inamsaidia mwenye kiwanda.” 

Kuanzia wiki iliyopita, wafanyabiashara hao wamehakikisha wanapandisha bei ya mafuta ya kula kama njia ya kuitisha Serikali ya Rais Magufuli, ili isithubutu kuweka ushuru au kuweka utaratibu kama ule wa kuingiza sukari nchini kwa vibali maalumu vinavyoratibiwa na Serikali.

“Kwenye soko la mafuta la dunia, bei ya mafuta ya mawese imeshuka lakini hapa nchini inapanda. Hujiulizi kuna nini hapo? Bei imeshuka kwa asilimia hadi mbili,” kimesema chanzo chetu na kuongeza:

“Ushuru uwekwe ili kuwalinda wakulima wetu wa ndani, na fedha zitakazopatikana kwa njia hiyo zisaidie kuboresha kilimo cha nafaka za mafuta; zisaidie kutoa mikopo kwa wakulima – hasa vijana. Rais anaposema Tanzania ya viwanda, hivyo viwanda vitakuja kwa njia gani kama bado mafuta ya kula yanaingizwa bila kulipiwa hata senti moja?

“Ajira iko mashambani na katika viwanda vya ndani. Hawa wanaoingiza mafuta viwanda vyao vina teknolojia ya kisasa. Kiwanda kizima kikubwa kinaajiri watu 20 hadi 30; lakini viwanda vyetu vya kawaida vinaajiri watu wengi zaidi, na isitoshe, mahitaji ya mafuta yakiwa yapo, wakulima watalima zaidi, watauza zaidi na wataajiriwa zaidi katika viwanda huko vijijini.”

Kwa sasa Tanzania inaagiza wastani wa tani 300,000 za mafuta ya mawese kwa mwaka. Takwimu zinaonesha kwa miaka mitatu (2013-2015) Tanzania ilitumia dola milioni 604 za Marekani kuagiza mafuta ya kula; sehemu kubwa ikiwa mafuta ya mawese kutoka Indonesia na Malaysia. Mbegu ya mawese yanayolimwa katika mataifa hayo ilitolewa mkoani Kigoma.

 

Mkulo alivyowabeba wafanyabiashara

Ushuru kwenye mafuta ya kula ya mawese ulifutwa na aliyekuwa Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo, kupitia hotuba yake aliyowasilisha bungeni ya Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha wa 2009/2010.

Uamuzi wa Mkulo ulikuwa tofauti na mtangulizi wake, Zakia Meghji, aliyehakikisha anaweka ushuru kama njia ya kulinda viwanda vya ndani na wakulima.

Wakati fulani Meghji alinukuliwa akilalamikia shinikizo kubwa la wafanyabiashara waliokuwa tayari kufanya waliloweza ili ushuru huo usiwepo; lakini akaweza kukwepa vishawishi na kuliwezesha Taifa kupata fedha nyingi kupitia ushuru huo.

Mkulo kwenye hotuba yake wakati akifuta ushuru, alisema: “Tanzania kuondoa ushuru wa Forodha wa asilimia 10 unaotozwa kwenye mafuta ghafi ya kula ya mawese (crude palm oil) na kutoza asilimia sifuri kama ilivyo kwa nchi nyingine wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

“Hatua hii inalenga kuviweka viwanda vya mafuta vya hapa nchini katika nafasi nzuri ya kiushindani na vile vya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.”

Wakati Mkulo akitumia mbinu hiyo kuhalalisha kufutwa kwa ushuru, imebainika kuwa hakuna ushindani wowote wa viwanda vya mafuta katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.

 

Mizengwe uzalishaji mafuta ya mawese

Utamu uliomo kwenye biashara ya mafuta ya mawese na vita ya kuhakikisha yanaendelea kuingizwa nchini bila kulipiwa ushuru, umethibitishwa kwenye ripoti ya Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Kwenye ripori yake ya Mashirika ya Umma ya 2014/2015, CAG amebaini kuwapo kwa mizengwe mingi inayokwamisha uanzishwaji wa mashamba na viwanda vya mawese hapa nchini.

Ingawa hakutaja sababu za urasimu, duru za uchunguzi zinaonesha kuwa mkwamo huo unasababishwa na mtandao wa wafanyabiashara waagizaji wa mafuta ya mawese wanaoshirikiana na wakulima na wasafirishaji wakuu wa mafuta hayo – mataifa ya Indonesia na Malaysia. 

Mradi unaokwamisha uzalishaji mafuta ya mawese, unahusisha ubia kati ya Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) na Kampuni ya Nava Bharat Singapore Pty Ltd. Ununuzi wa ardhi ya ukubwa wa hekta 10,000 ulitarajiwa kufanywa na NDC. 

Ujenzi wa kiwanda cha kuzalisha mafuta ya mawese na uzalishaji wa megawati 10 za umeme wa mimea, ulitazamiwa kufanywa na mbia binafsi, ambako kwa ujumla wake upatikanaji wa lita milioni 58 za mafuta ya mawese zilitarajiwa baada ya mradi kuanza uzalishaji.

Hata hivyo, hadi ukaguzi wa CAG unakamilika, mradi ulikuwa haujaanza kufanya kazi kwa sababu ya urasimu wa taratibu za Serikali, zilizosababisha uchelewaji wa karibu miaka mitatu wa mradi huo. 

CAG anasema: “Barua ya Desemba 6, 2015 yenye kumbukumbu namba KSW/130/Vol III/1 kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe kwenda Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi iliyohusu ombi la kuhamisha ardhi yenye ukubwa wa hekta 4,000 (kati ya hekta 10,000 zinazohitajika) katika eneo la Kijiji cha Kimala Misale kwenda Shirika la Maendeleo la Taifa ilichukua mwaka mzima kwa barua hii kujibiwa, kwa mradi husika kukubaliwa na maombi hayo kupelekwa rasmi kwa Ofisi ya Rais kwa barua yenye kumbukumbu namba LD/314579/21 kwa uthibitisho wa mwisho.

“Sambamba na hilo, Shirika (NDC) lilipokea barua yenye kumbukumbu Na. CEA 110/302/V/01/32 ya Desemba 29, 2015 kutoka Ofisi ya Rais ikilitaarifu kwamba barua imetumwa Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe ili kupata taarifa sahihi kabla ardhi haijamilikishwa kwa mmiliki mpya, kwa mujibu wa kifungu namba 114 (1) cha Sheria ya Ardhi na Vijiji inayoruhusu umilikishaji ardhi ya kijiji kwa matumizi ya umma.

“Karibu miaka mitatu imepita, lakini shirika bado halijapata uthibitisho wa umiliki wa ardhi ya ukubwa wa hekta 4,000 lililoomba hivyo kuongeza sintofahamu kwenye utekelezaji wa mradi. 

“Taratibu za uombaji wa ardhi ya nyongeza ya hekta 6,000 katika vijiji vya Dutumu na Madege haziwezi kuanza bila ombi lililopita la hekta 4,000 kufanyiwa kazi ikiwamo ulipwaji wa fidia kwa wamiliki husika.”

Mmoja wa maofisa wa Wizara ya Ardhi aliyezungumza kwa masharti ya kutotajwa jina, amesema urasimu huo unasababishwa na wafanyabiashara ambao hawaoni umuhimu wa kuwa na viwanda hapa nchini katika mazingira wanayoendelea kupata faida kubwa kwa kuingiza mafuta bila kulipa ushuru.

Pia anasema ni vita iliyopo kati ya wazalishaji walioko Indonesia na Malaysia kwa upande mmoja, dhidi ya mwekezaji kutoka Singapore anayetaka kushirikiana na NDC kuwekeza hapa nchini.

Anatoa mfano wa kilimo cha mawese kilivyokufa nchini Nigeria, akisema chanzo kikuu ni vita ya wakulima wa mataifa yanayolima mawese na wafanyabiashara dhidi ya wale walioamua kuwekeza kwenye kilimo na kufungua viwanda nchini Nigeria.

“Bila kuchukua hatua za makusudi, kilimo cha mawese hapa nchi kitakuwa ndoto na kwa hiyo hakuna viwanda vitakavyoanzishwa. Rais awe mkali, vita hii ni kubwa kama ya sukari au hata zaidi,” kimesema chanzo chetu.

2733 Total Views 2 Views Today
||||| 1 I Like It! |||||
Sambaza!