Juma Nyosso Akamatwa na Polisi

Jeshi la Polisi Mkoani Kagera limethibitisha kumshikilia mlinzi wa Kagera Sugar Juma Said Nyosso kwa kosa la kumpiga shabiki anayeaminika kuwa ni wa Simba baada ya mchezo wa ligi kuu dhidi ya Simba uliopigwa mjini Bukoba.

Tukio hilo limetokea baada ya mechi kumalizika na wachezaji wa Kagera Sugar walikuwa wanakwenda katika vyumba vya kubadilishia nguo na mashabiki wakawa wanashangilia kwa kutoa maneno makali kitendo ambacho kilimfanya Nyosso akose uvumilivu na kumpiga shabiki huyo.

Baada ya kupigwa ngumi shabiki huyo alianguka chini na kuonekana kama amepoteza fahamu ndipo Polisi walifika na kumkamata Nyosso na kuondoka naye.Aidha shabiki huyo alichukuliwa na gari ya wagonjwa na kumkimbiza hospitali kwaajili ya kupata huduma zaidi ikiwemo matibabu.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Kagera Augustine Orom amesema bado wanaendelea na uchunguzi zaidi wa tukio hilo na wakikamilisha watatoa taarifa kamili.