JWTZ wasogea mpakani

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Tanzania, Bernard Membe, ameionya Serikali ya Malawi kuhusu mgogoro wa mpaka, katika kile kinachoonekana kuwa Tanzania ipo tayari kuingia vitani endapo itapuuzwa. Wakati Membe akitoa msimamo huo mkali bungeni jana, kuna habari kwamba wanajeshi na vifaa vya kijeshi wameshapelekwa karibu na eneo la mgogoro ajili ya kuimarisha ulinzi.

Ulinzi huo unaofanywa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), unalenga kudhibiti vitendo vyote vya uchokozi vinavyofanywa na Serikali ya Malawi na kampuni zilizopewa vibali na nchi hiyo kufanya utafiti wa mafuta na gesi katika Ziwa Nyasa. Membe alitangaza msimamo wa Serikali ya Tanzania alipokuwa akiwasilisha bungeni Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kwa mwaka wa fedha wa 2012/2013, jana.

 

Wakati akitangaza uamuzi huo, ujumbe wa makamishna wa Tume ya Utumishi wa Bunge la Malawi ulikuwapo eneo la wageni wa Spika kumsikiliza Membe. Ujumbe huo uliongozwa na Naibu Spika wa Pili wa Bunge la nchi hiyo, Juliana Mpande. Wengine na vyeo vyao kwenye mabano ni Alfred Mwechumu (Kamishna), Akimu Mwanza (Kamishna), Watson Makala Ngozu (Kamishna), Profesa Eta Banda (Kamishna), Christina Chiwoko (Kamishna), Renard Mapemba (Naibu Katibu wa Bunge la Malawi), Leonard Mengezi (Mtumishi wa Bunge), Hervey Chugumula (Mtumishi wa Bunge) na Tamika Nyirenda ambaye pia ni Mtumishi wa Bunge la nchi hiyo.

 

Uzoefu wa Tanzania, tofauti na Malawi katika medani za kivita ni wa hali ya juu. Kwa kifupi tu, JWTZ imeshiriki Operesheni nyingi kwa mafanikio makubwa. Kuna Operesheni Kumekucha dhidi ya Wareno mwaka 1960; Operesheni TEGAMA – Msumbiji, dhidi ya majeshi ya Rhodesia na Afrika Kusini (1975-1980); Operesheni Safisha – Msumbiji, dhidi ya Mozambican National Resistance au Resistência Nacional Moçambicana (RENAMO) mwaka 1986-1988; Operesheni dhidi ya mamluki waliovamia Kisiwa cha Ushelisheli mwaka (1981-1982) na Operesheni Demokrasia Comoro (Machi 2008) iliyomwondoa Kanali Mohamed Bakar kutoka kisiwa cha Anjouan.


JWTZ inakumbukwa kwa kipigo ilichompa dikteta Idi Amin Dada wa Uganda na hata kumfanya aikimbie nchi hiyo katika vita iliyojulikana kama Vita ya Kagera, mwaka 1978. JWTZ imeshiriki katika Operesheni za kulinda amani chini ya Majeshi ya Umoja wa Mataifa. Mifano ya karibuni ni ya Liberia, Darfur na Lebanon. JWTZ ina hazina kubwa ya uzoefu kutokana na Operesheni hizo. Siri kubwa ya mafaniko ya JWTZ ni umoja, ujasiri, nidhamu na weledi.

HOTUBA YA MEMBE KUHUSU MPAKA WA TANZANIA NA MALAWI ALIYOITOA BUNGENI JANA AGOSTI 6, 2012.

Mheshimiwa Spika, tunalo tatizo la muda mrefu – suala la mpaka wetu Ziwa Nyasa au Ziwa Malawi kama linavyoitwa na wenzetu Malawi. Tatizo lenyewe, wenzetu wa Malawi wanadai kwamba mpaka wetu na wao kwenye Ziwa Nyasa unapita pwani, na kwa maana hiyo ziwa lote la Nyasa kutoka kwenye mpaka wa Mozambique (Msumbiji) hadi Malawi ni mali yao. Msingi wa madai yao ni kwamba mkataba uliowekwa saini kati ya Waingereza na Wajerumani mwaka 1890 uliweka mpaka kwenye pwani au ufukwe wa Ziwa Nyasa. Mkataba huo unajulikana kama Anglo-German Agreement au Heligoland.

 

Mheshimiwa Spika, Tanzania kwa upande wetu tunadai kwamba mpaka kati yetu na Malawi kwa Ziwa Nyasa unapita katikati ya ziwa hilo, kutoka pale Malawi na Mozambique (Msumbiji) wanapopakana, usawa wa nyuzi 11 kusini hadi mwisho wa ziwa kule Kyela kwenye digrii 9 katikati ya ziwa.

 

Mheshimkiwa Spika, msingi wa madai yetu hayo ni kwamba kwa mujibu wa nyaraka na ramani zilizotengenezwa na wakoloni wetu Waingereza mwaka 1928, 1937 na mwaka 1939 zinaonyesha kuwa mpaka wa ziwa hilo upo katikati.


Aidha, mkataba huo huo wa Anglo-German wa mwaka 1890 unaotumiwa kama msingi wa madai yao umebainisha katika ibara ya sita kwamba nchi zinazohusika – yaani Tanganyika na Nyasaland – wakati huo au Tanzania na Malawi sasa, zikutane ili kurekebisha kasoro katika mazingira yatakayolazimu. Jambo hili si jipya, tumeshafanya jambo hilo upande wa mpaka wa bahari yetu na nchi ya Comoro na Msumbiji Desemba 5, 2011 na mwaka huu Februari 17, 2012 Tanzania na Ushelisheli tumekaa, tumejadili na tumerekebisha mpaka wetu kule baharini kati ya Tanzania na Ushelisheli.


Mheshimiwa Spika, madai ya Tanzania yanakuwa na nguvu zaidi tunapolinganisha ‘case’ kama hii na iliyotokea kati ya Cameroon na Nigeria kuhusu mpaka wao kwenye Ziwa Chad lililopo katikati ya Nigeria na Cameroon. Katika ‘case’ hiyo iliyopelekwa kwenye Mahakama Kuu ya Dunia, Mahakama Kuu ya Dunia iliamua kwamba mpaka huu upite katikati ya Ziwa Chad ukifuata mstari ulionyooka, yaani ‘median line’ hadi kwenye mdomo wa mto….Uamuzi huu ulitokana na sheria za kimataifa ambazo zinaeleza, pamoja na mambo mengine, kuwa mstari upitao katikati ya ziwa ndiyo mpaka unaokubalika kati ya nchi na nchi zinazopakana na ziwa.

 

Mheshimiwa Spika, kutokana na maelezo yote haya ni dhahiri kuwa tunalo tatizo linalopaswa kutatuliwa kati yetu na Malawi kuhusu mpaka wa Ziwa Nyasa. Tatizo hili ni la muda mrefu. Kutokana na mazingira ya miaka ya 1960 na 1970 suala hilo lisingeliweza kutatuliwa kwa sababu mbili kubwa; mosi, kiongozi wa Malawi wa kipindi hicho Dk. Hastings Kamuzu Banda alikuwa rafiki wa serikali ya makaburu wa Afrika Kusini, wakati sisi tulikuwa marafiki wa wapigania ukombozi ikiwamo ANC ya Afrika Kusini.


Lakini kulikuwa na sababu ya pili, ni kuwa kutokana na Tanzania kuwa makao makuu ya vyama vya ukombozi duniani, wapinzani wa Serikali ya Malawi walikimbilia Tanzania na hivyo kumfanya kiongozi wa Malawi wa wakati huo kuamini kuwa Tanzania ilikuwa kichaka cha maadui dhidi ya Serikali ya Malawi. Haya hayakuwa mazingira mazuri ya kuanza mazungumzo ya kidiplomasia kutatua tatizo la mpaka wetu kati ya Tanzania na Malawi.


Mheshimiwa Spika, baada ya utawala wa Rais Kamuzu Banda kuondoka, utawala mpya wa Rais Bakil Muluzi, Rais Bingu wa Mutharika, na Rais Joyce Banda kuja madarakani, uhusiano kati ya Tanzania na Malawi ukaanza kuwa mzuri zaidi na kukaribisha mazingira ya kujadili suala hili la mpaka kidiplomasia.

 

Mheshimiwa Spika, Juni 2005 aliyekuwa Rais wa Malawi, Mheshimiwa Mutharika, alimwandikia Mheshimiwa Rais Benjamin Mkapa barua ya kumwomba iundwe kamati ya pamoja chini ya wataalamu, yaani joint committee of experts kuchambua, kushauri na kutatua tatizo la mpaka kati ya nchi zetu mbili.

 

Kwa kuwa mwaka huo ulikuwa ni kipindi cha uchaguzi, Mheshimiwa Rais Mkapa alikuwa anaondoka na alimwachia kazi hiyo rais ajaye kushughulikia tatizo la mpaka. Mheshimiwa Rais Kikwete akaja, na alikutana na tatizo hili. Wakati wa utawala huu wa Rais Kikwete, alikutana na hayati Rais Mutharika mara mbili kwenye mikutano ya AU, Addis Ababa, na kwa pamoja walikubaliana kwamba ziundwe timu za wataalamu chini ya mawaziri wa mambo ya nchi za nje na timu za wataalamu ili zifanye kazi hiyo.


Mheshimiwa Spika, timu iliundwa na timu zote mbili zikaanza kukutana tangu mwaka 2010 kwa kutengeneza hadidu za rejea kuhusu ufumbuzi wa tatizo hilo la mpaka. Wakati kamati hizo zikiendelea kukutana na kuweka mkakati wa kutatua tatizo hili, suala hili likachukua sura mpya ya kuashiria kuhatarisha usalama wa nchi yetu.


Serikali yetu ilipata habari za kuaminika kupitia shirika la TPDC (Shirika la Taifa la Maendeleo ya Petroli) kuwa eneo lote la Ziwa Nyasa, kaskazini mwa Msumbiji limegawanywa kwenye vitalu, na kwamba Serikali ya Malawi imetoa vitalu hivyo kwa kampuni ya utafiti ya mafuta na gesi. Aidha, kampuni hizo ziliomba kibali cha kuruhusu ndege za utafiti; ombi ambalo Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania ililikataa.


Pamoja na katazo hilo, serikali yetu ilipata ushahidi kwamba ndege ndogo za utafiti zenye uwezo wa kutua majini na ufukweni zinazokadiriwa kuwa tano zilionekana zikivinjari na kuwa katika Ziwa Nyasa upande wa Tanzania na ufukwe wake. Matukio hayo yalitokea kati ya Januari 29 na Julai 2, mwaka huu.

Serikali iliwasiliana na Serikali ya Malawi kwa maandishi tukiomba ufanyike mkutano kwa ngazi ya mawaziri na wataalamu kujadili mustakabali wa mpaka huu.


Mheshimiwa Spika, mkutano wa mawaziri na wataalamu ulifanyika Julai 28, 2012 jijini Dar es Salaam na kujadili tatizo hili. Baada ya majadiliano marefu, mambo matatu yalijitokeza. Mosi, pande zote mbili zilikubaliana kwamba lipo tatizo kwa kuwa kila upande ulishikilia msimamo wake. Pili, serikali zetu mbili zilikubaliana kuendelea na mazungumzo, na zikakubaliana Agosti 20-27, mwaka huu mkutano wa wataalamu na baadaye wa mawaziri ufanyike mjini Mzuzu, Malawi. Tatu, Serikali ya Tanzania iliitaka Serikali ya Malawi kutoruhusu mtu au kampuni yoyote ile kuendelea na shughuli za utafiti kwenye eneo lote linalobishaniwa.

Mheshimiwa Spika, hayo ndiyo maelezo yetu yanayohusu matatizo yetu ya mpaka na Malawi.


Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inathamini sana uhusiano mzuri uliopo baina ya nchi mbili na ina dhamira ya kudumisha na kuimarisha ujirani mwema kwa manufaa ya watu wetu. Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inapenda kuchukua nafasi hii tena kuitaka Serikali ya Malawi kuheshimu makubaliano yetu ya Julai 27, 2012 kwamba njia nzuri ya kutatua tatizo hili ni ya kidiplomasia. Njia nzuri na bora ya kutatua tatizo hili lililoko mbele yetu ni ya mazungumzo ya amani, na kwamnba katika kipindi chote cha mazungumzo hayo, Serikali ya Malawi isiruhusu mtu, kikundi au kampuni yoyote ile kufanya utafiti kwenye eneo la Ziwa Nyasa lililoko kaskazini-mashariki mwa Ziwa Nyasa kati ya nyuzi 11 hadi 9 kwani eneo hilo ni sehemu ya Tanzania.

 

Mheshimiwa Spika, tunazungumzia maisha ya Watanzania wapatao 600,000 wanaoishi kwenye mwambao wa Ziwa Nyasa. Kwao wao, Ziwa Nyasa ni urithi wao – natural heritage. Kwao wao, Ziwa Nyasa ni chanzo cha uzima wao na maendeleo yao. Kwa vyovyote vile Serikali inayo dhamana ya kuwalinda watu hawa kwani ni wananchi wetu.

 

Mheshimiwa Spika, Serikali ya Tanzania inapenda kuchukua nafasi hii kuyaonya na kuyataka makampuni yote yanayofanya shughuli za utafiti kwenye eneo la ziwa hilo kusitisha kuanzia sasa – napenda kurudia sehemu hiyo – napenda kuyaonya makampuni yote yanayofanya utafiti kwenye eneo hilo kuanzia leo Jumatatu kuacha shughuli za utafiti katika maeneo hayo. Serikali haitaruhusu – narudia – Serikali haitaruhusu utafiti huu kuendelea hadi makubaliano na majadiliano kuhusu mpaka yatakapofikiwa kati ya nchi mbili, yaani Tanzania na Malawi. Let us give diplomacy a chance.

 

Mheshimiwa Spika, Serikali inapenda kuwahakikishia wananchi wote wa eneo la Ziwa Nyasa kuendelea na shughuli zao ziwani na nchi kavu kama kawaida na bila wasiwasi yoyote kwa sababu serikali yao ipo macho, ipo imara, ipo tayari kulinda mipaka ya nchi yetu kwa gharama yoyote.