*Operesheni Tokomeza’ yaanza rasmi

*Inashirikisha, Usalama wa Taifa, Polisi

*Majangili kadhaa hatari yakamatwa

 

JESHI la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limeanza rasmi operesheni ya kuwatokomeza majangili.

Operesheni hiyo iliyopewa jina la Operesheni Tokomeza ilianza rasmi Oktoba 5, mwaka huu ikilenga kuwalinda wanyamapori, hasa ndovu na faru walio hatarini kumalizwa na majangili.

Habari za uhakika kutoka serikalini zinasema uzinduzi wa Operesheni Tokomeza ulifanyika siku hiyo katika Hifadhi ya Taifa Mikumi. Inaongozwa na mmoja wa makamanda wa JWTZ mwenye cheo cha juu.

 

Pamoja na makamanda na wapiganaji kutoka JWTZ, Operesheni Tokomeza inahusisha vyombo vingine vya ulinzi na usalama vikiwamo Usalama wa Taifa na Polisi.

Kwa kuanzia, watuhumiwa kadhaa wa ujangili tayari wameshatiwa mbaroni. Kukamatwa kwao kumekuwa ‘rahisi’ kutokana na kazi ya kiintelejensia iliyofanywa kwa weledi wa hali ya juu na mmoja wa maofisa Usalama wa Taifa wanaoaminiwa kwa kazi hiyo. Jina la ofisa huyo tunalihifadhi kwa sasa.

 

Baada ya Operesheni Tokomeza kuzinduliwa Mikumi, kilichofuata ni kusambazwa kwa askari katika mapori mbalimbali, wakianza na yale yaliyoandamwa mno na majangili. Miongoni mwayo ni Pori la Akiba Selous ambalo linajulikana miongoni mwa majangili kama ‘shamba la bibi.’

“Ninachoweza kukuhakikishia ni kwamba tayari tumeshawatia mbaroni majangili wengi pamoja na zana wanazotumia. Operesheni hii inatisha, tumejiandaa vya kutosha. Waliojaribu kujibu mapigo kwa kurusha risasi tumewakabili,” amesema mmoja wa viongozi wa Operesheni Tokomeza.

 

Ikiwa ni wiki chache tangu kuzinduliwa kwa Operesheni Kimbunga iliyolenga kuwaondoa nchini wahamiaji haramu na kukamata silaha kutoka kwa watu wanaozimiliki kinyume cha sheria.

 

Kamati ya Bunge: Tembo wanakwisha

Kamati ya Kudumu ya Bunge imesema ujangili dhidi ya tembo kwa sasa ni janga la kitaifa.

“Ni ukweli usiofichika kwamba leo hii si tu tembo wanauawa, bali wanateketezwa. Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori (TAWIRI), taarifa zinazoshabihiana na za utafiti wa kimataifa zinaonesha kwamba tembo wasiopungua 30 wanauawa kwa siku, tembo 850 wanauawa kwa mwezi, na tembo 10,000 wanauawa kila mwaka (TAWIRI 2011).

 

“Kutokana na kasi kubwa ya kuuawa kwa tembo, taarifa za kitaalamu kutokana TAWIRI zinathibitisha kwamba idadi ya tembo imepungua kutoka 109,000 mwaka 2009 hadi tembo chini ya 70,000 mwaka 2012.

“Endapo kasi hii ya ujangili wa tembo itaendelea bila kudhibitiwa mara moja, ni wazi kuwa tembo watakuwa wametoweka nchini katika kipindi cha miaka saba ijayo,” imeonya Kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Kahama, James Lembeli.

 

Kamati hiyo imeongeza kusema, “Hali hii ni hatari na aibu kwa nchi yetu ambayo ni ya pili barani Afrika kwa kuwa na idadi kubwa ya tembo. Kinachosikitisha ni kwamba Wizara imekuwa na kigugumizi katika kuitikia kauli ya Rais Jakaya Kikwete iliyoitaka Wizara kuomba msaada kwake kama tatizo la ujangili limewashinda. Jambo hili linaweza kutafsiriwa kuwa ni hujuma inayofanywa na baadhi ya watendaji wa Wizara ambao wamepuuza kauli ya Mheshimiwa Rais.”

 

Kamati inapendekeza kufanywa kwa Operesheni kama Operesheni Uhai kwa nchi nzima kama ilivyofanya miaka ya 1980. Pia imependekeza Sheria ya Wanyamapori Namba 5 ya mwaka 2009 ifanyiwe marekebisho kwa kuweka adhabu kali kwa watu watakaothibitika kuhusika na ujangili, hasa wa tembo.

1623 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!