el2Elirehema Moses Kaaya ni mwanasiasa asiyekata tamaa. Ni kada maarufu wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) anayeamini katika falsafa, itikadi, katiba na imani ya chama hicho japo anakerwa mno na masuala yanavyokwenda ndani ya chama hicho tawala na kikongwe nchini.
 Amegombea ubunge katika Jimbo la Arumeru Mashariki mara tatu bila mafanikio. Mara ya kwanza alijitokeza mwaka 2005 akashindwa, akajitosa tena mwaka 2010 nako kura hazikujaa na hata mwaka 2012 ulipofanyika uchaguzi mdogo katika jimbo hilo kutokana na kifo cha aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo, Jeremiah Sumari, pia hakubahatika kushinda.


Mara zote hizo, Kaaya alishindwa katika kura za maoni ndani ya chama chake na hakuwahi kupata nafasi ya kwenda kwa wapiga kura wote wa Arumeru Mashariki ili wamsikilize sera zake, kuzipima na hatimaye kufanya uamuzi sahihi na pengine magumu.
Mwaka huu wa Uchaguzi Mkuu, Kaaya ameamua kujaribu bahati yake kwa mara nyingine akiamini kwamba wapiga kura wa Arumeru Mashariki wamejifunza vya kutosha na sasa wapo tayari kuchagua kiongozi bora na si bora kiongozi.


 Katika mahojiano na mwandishi wa makala hii nyumbani kwake Patandi, Tengeru wiki iliyopita, Kaaya anaeleza wazi kwamba kutokana na uzoefu wa kisiasa alionao, uvumilivu alioonyesha hata baada ya kushindwa kwa mizengwe mara zote, matatizo sugu ya wakazi wa jimbo hilo yaliyokosa ufumbuzi kwa zaidi ya nusu karne na matamanio ya wananchi wa jimbo hilo kupata kiongozi bora, ana imani kubwa kuwa safari hii kura zitajaa na kutosha ili apeperushe bendera ya CCM katika Uchaguzi Mkuu.
“Sasa nimekomaa kuwa mbunge kuliko wakati mwingine wowote, na nina uelewa mkubwa wa wajibu wa mbunge, ninazifahamu kero nyingi za wananchi wa jimbo letu na namna bora ya kuzitatua, hivyo nimeamua kuja kuomba ridhaa ya kuwatumikia, na nina imani watanipa ridhaa hiyo nami naahidi kutowaangusha hata dakika moja,” anasisitiza Kaaya katika mahoajiano haya na kuongeza:


“Majukumu makubwa ya mbunge kimsingi ni matatu; kutunga sheria, kuisimamia Serikali na kupitisha bajeti ya Serikali kila mwaka. Katika kutunga sheria bungeni nitahakikisha zinaangalia maslahi mapana ya jimbo langu, nitashirikiana na wenzangu kuisimamia Serikali kuhakikisha yale yote yenye manufaa kwa wananchi wetu yanatekelezwa kikamilifu ikiwa ni pamoja na bajeti kutumika kwa manufaa ya wananchi wetu tofauti na ilivyo sasa.”
Kuhusu kero sugu jimboni humo, Kaaya anasema kwamba masuala ya ardhi, maji, ajira hasa kwa vijana, elimu, afya na miundombinu ni mambo ambayo yanamkosesha usingizi na kutokana na mikakati kabambe aliyojiwekea, na endapo atapewa ridhaa na wananchi wa Arumeru Mashariki, anaamini, kwa kushirikiana na wadau wote ikiwamo Serikali Kuu, washirika wa maendeleo, wahisani, wawekezaji na wananchi wenyewe kwa kutumia mbinu shirikishi, baada ya muda mfupi kero hizo zitakuwa historia katika jimbo hilo.


“Niseme tu hapa kwa mfano katika suala la ardhi. Pamoja na kuwa ardhi inamilikiwa kisheria tutatumia mbinu ya mazungumzo na wamiliki katika kuhakikisha wananchi wanapata ardhi ambayo haijaendelezwa, lakini kwa utaratibu na si kushawishi wananchi kuvamia mali za watu. Tutaonana na wamiliki na kuzungumza nao na tukifikia muafaka tutamwomba Rais atumie mamlaka yake kutengua umiliki na ardhi wapewe wananchi.
Anasema kuwa suala la ardhi kwa watu wa Meru ni la kihistoria kwa sababu walowezi wachache wa kizungu walijimilikishia ardhi kubwa tangu wakati wa ukoloni hali iliyomlazimu Mzee Japhet Kirilo kupeleka malalamiko Umoja wa Mataifa mwaka 1958 kudai wananchi warejeshewe ardhi yao.


“Katika suala la ajira, jimbo letu limejaliwa kuwa na wawekezaji wengi katika hoteli za watalii, mashamba ya maua na wengine wengi. Hapa ni suala la kukutana na wawekezaji hao na sisi kama Halmashauri tutatunga  sheria ndogo ambazo zitaweka bayana kwamba zile kazi ndogo ndogo ambazo hazihitaji utaalam na  ujuzi (Common Cadre), zinatolewa kwanza kwa watu wa Arumeru Mashariki ikiwa ni njia mojawapo ya kuwahakikishia ajira vijana wa jimbo letu,” anasema.
Akizungumzia elimu, Kaaya anasema mkazo wake, kwa kushirikiana na wenzake utakuwa kuimarisha na kuongeza vyuo vya ufundi katika jimbo hilo ili kuwawezesha vijana kuwa na ujuzi wa kujiajiri moja kwa moja baada ya kuhitimu mafunzo; jambo litakalosaidia kupunguza tatizo la ajira.
‘‘Njia bora ya kuwasaidia vijana wetu kuwa na kazi ni kuwapa mafunzo ya ufundi stadi. Ajira ni tatizo la kidunia, lakini kazi zipo tele na kinachotakiwa ni mtu kuwa na ujuzi, mathalan kuwa fundi mchundo, seremala, ushonaji, ujenzi, uchomeaji chuma, na hii haihitaji elimu ya chuo kikuu, bali vyuo vya ufundi tu. Naamini tukiweka misingi imara na bora, vijana wetu watakuwa na kazi nami nitalisimamia hili kwa nguvu zangu zote,” anasisitiza.


Anaahidi kuwa na kumbukumbu ya vijana wote wanaohitimu katika vyuo vikuu vitano vilivyopo katika jimbo hilo ili kusaidiana nao kutafuta njia bora ya kupata ajira na ikiwezekana wajitegemee kwa kutumia fursa zilizopo katika jimbo hilo.
Kuhusu kero ya maji, Kaaya anaeleza kusikitishwa kwake na wananchi wa jimbo hilo kukosa maji wakati kuna mito sita inayotiririsha maji kutoka Mlima Meru kwa mwaka mzima huku maji ya mvua yakiwa yanapotea kila msimu.
Anaeleza kuwa katika hili, kwanza atahakikisha sheria ndogo ya kuhifadhi maji ya mvua katika kila taasisi ya elimu, afya, dini na hata watu binafsi, inatungwa ili kuwalazimisha watu kuhifadhi maji ya mvua na kuwa na uhakika wa maji kwa mwaka mzima.


“Tutajenga mabwawa makubwa katika kata za Shambarai, Mbughuni, Kikwe, Majengo na Makiba ili wananchi wetu waweze kutumia maji katika shughuli za kilimo cha umwagiliaji, matumizi ya nyumbani na matumizi ya mifugo kwa uhakika zaidi,” anasema.
Akizungumzia suala la afya, Kaaya anasema kwamba atahakikisha anaboresha hospitali ya wilaya, vituo vya afya na zahanati; na kwamba akiwa mbunge suala la akina mama kudaiwa pamba, nyembe wakati wa kujifungua linakwisha na atatumia sehemu ya mshahara wake kugharimia vitu hivyo.

Mbinu shirikishi
Ili kufanikisha mikakatti hiyo, Kaaya anasema kwamba atatumia Mbinu Shirikishi kwa Maendeleo Endelevu, ikiwa na maana ya kuwashirikisha wananchi:
“Miradi yote ipo kwa ajili ya wananchi na ni lazima waione kuwa ni mali yao kwa kuwashirikisha kuanzia mwanzo na mimi kama kiongozi kazi yangu ni kuongoza njia, kutafuta uwezeshaji na kuwapa mrejesho wa masuala yote wanayohitaji. Kwa kufanya hivyo lazima wananchi watashiriki kwa sababu wao ni sehemu muhimu ya miradi ya maendeleo,” anasema.

Rushwa
Pamoja na kuwa ni kada mahiri wa CCM, Kaaya hasiti kukerwa na utamaduni uliojengeka ndani ya chama hicho wa kupata viongozi kwa kutumia rushwa akisema kwamba hicho ndicho kinachosababisha chama hicho kupoteza mvuto kwa wapigakura, hasa katika miaka ya karibuni.
Anasema kutokana na utamaduni huo kutamalaki ndani ya chama kinyume kabisa na Katiba ya chama, ilani za uchaguzi na ahadi za mwana CCM bado viongozi wa ngazi za juu wameshindwa kuchukua hatua za makusudi za kukabiliana na kansa hiyo.


“Nitaendelea kupiga kelele juu ya rushwa ndani ya chama chetu labda ihalalishwe katika Katiba yetu, miongozo mbalimbali na imani za chama chetu kwa sababu tatizo hili limetuletea matatizo mengi kiasi kwamba chama kinapoteza mvuto wake kwa wananchi baada ya kuwapata viongozi wabovu kwa sababu ya rushwa tu. Hawana sifa yoyote ya uongozi zaidi ya rushwa.
“Imefikia mahali thamani ya kura inalinganishwa na Sh 10,000 au pombe na watu wanafanya uamuzi kwa kutumia mambo hayo maovu badala ya utashi wao, lakini kibaya zaidi viongozi wa chama wanafumbia macho uchafu huu, hawachukui hatua yoyote na mwishowe tunaishia kuwa Taifa la walalamikaji huku tukienda mrama kila kunapokucha.


“Kutokana na kukithiri kwa rushwa imefikia mahali badhi ya wagombea wanadhani sifa pekee ya uongozi ndani ya chama chetu ni kuwa na fedha na kutumia fedha hizo kuhonga na kushawishi wapigakura jambo ambalo si sahihi hata kidogo. Sifa za uongozi ni zaidi ya fedha na wala fedha haijawahi kuwa kigezo cha kumpata kiongozi bora.
“Ni vema wananchi wakajiuliza maswali mawili rahisi; je, mgombea huyo amepata wapi fedha hizo anazogawa ovyo na atazirudishaje akipewa dhamana ya uongozi maana kule ni kwenda kuwatumikia wananchi; na si kujitajirisha na huenda akatumia muda wake mrefu kurudisha gharama zake badala ya kuwatumikia watu.


“Kama wewe ni safi na una uwezo wa kuongoza watu kwanini uhonge? Ole wao wagombea wanaotumia rushwa kusaka uongozi. Naamini siku zao zinahesabaika kwa sababu Watanzania hawatakubali kuwa wajinga kila siku na sasa wameamka, wanachotaka ni kiongozi bora atakayewasaidia katika changamoto zao,” anasema.
Alipoulizwa iwapo atashindwa kwa mizengwe katika kura za maoni anaweza kujiunga na vyama vya upinzani, Kaaya alijibu haraka: “Kamwe siwezi kujiunga na upinzani”.


 Kitaaluma, Kaaya ni tabibu wa mifugo na mwanadiplomasia ambaye anafanya kazi katika Halmashauri ya Jiji la Mwanza akiwa Afisa Uhusiano. Amepata mafunzo ndani na nje ya nchi kikiwamo Chuo cha Mifugo Tengeru na Chuo cha Diplomasia na Uhusiano wa Kimataifa Kurasini jijini Dar es Salaam.
 Ni kada wa CCM akiwa ameshikilia nyadhifa mbalimbali kwa miaka zaidi ya 15 ikiwa ni pamoja na kuwa Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa wa CCM, Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza na pia Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Halmashauri Kuu ya Wilaya ya Nyamagana, Mkoa wa Mwanza.

1725 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!