Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Halima Mdee, juzi aliwasilisha hotuba yake bungeni na kueleza mambo mengi. Miongoni mwa hayo ni uporaji wa ardhi uliofanywa na kiongozi wa CCM. Ifuatayo ni sehemu ya hotuba hiyo:

Mheshimiwa Spika, dhuluma hii inalihusisha shamba  namba 24 Lorkisalie (OLDUPAI SEED CO. LTD), lililopo wilayani Simanjiro, Jimbo la Simanjiro, Kitongoji cha Lemooti, Kijiji cha  Loiborsoit A.

 

Kwa mujibu  wa barua ya Ofisi  ya Msajili  wa Hati Kanda  ya  Kaskazini- Moshi  ya Machi Mosi, 2010 yenye kumbukumbu namba LR/MS/T/1127 4/15 inaonyesha kwamba  shamba husika lilisajiliwa  Novemba  28, 1994 na kupewa hati namba 11274.

 

Mhusika mkuu katika mgogoro huu ni  Bwana  Brown Mathew Oleseya, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Simanjiro, ambaye amejimilikisha kiujanja-ujanja  hekta za kijiji 3,425 ambazo ni sawa na ekari 8,562.5.  Licha ya kujipatia eneo husika kimizengwe, mheshimiwa huyu wa chama tawala  amefungia wananchi  njia zote za chemchem za maji na  malisho ya mifugo.

 

Barua yake ya maombi ya shamba  ya Aprili 14, 1978, yenye kumb na: PF/MI/40 inaonyesha kwamba  aliomba eneo  tofauti  na analolitumia kwa sasa. Barua inaonyesha aliomba eneo la LESHUTA, ambalo lipo katika Kijiji cha Engonongoi, Kata ya Terat na  shamba ‘analolimiliki’  kwa sasa lipo eneo la  LEMOOTI Kijiji cha Loiborsait A.

 

Muhtasari wa kikao cha kamati ya maendeleo ya Kata kilichoketi Aprili 26, 1978 kilichohudhuriwa na wajumbe 19 kinachosemekana kilimpatia Mwenyekiti huyu wa CCM Ardhi (ekari 5,000, ekari 2,000 za kulima na 3,000 kwa ajili ya mifugo), haujaidhinishwa na mamlaka yoyote  na hakuna  mhuri wala sahihi  ya mwenyekiti, katibu wala wajumbe. Barua pekee yenye sahihi, bila mhuri wowote ni ya Katibu Kata ya Aprili 26, 1978 ikimtaarifu kwamba amepewa shamba husika.

 

Kamati ya Ushauri wa Ardhi ya Wilaya ya Kiteto iliyoketi Januari 16, 1979 iliyohudhuriwa pia na na Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya kipindi hicho, Ndugu ole Kone  na katibu wa CCM (W), Ndugu P. Bura,  pamoja na mambo mengine,  walijadili maombi ya mashamba, yaliyopitishwa na ngazi ya Kata pamoja na shamba la Bwana Brown Mathew ole Suya. Kikao husika  kiliamua kwamba katika ekari 5000 zilizoombwa, ekari 2000 za kilimo atazitumia kwa miaka mitano kisha zirejeshwe kijijini, na ekari 3,000 apewe hati ya miaka 33, lakini asiingilie hifadhi, sehemu ya Jeshi na Wilaya ya Monduli. Kama ilivyo nyaraka zilizotangulia, muhtasari wa kikao husika hakikuwa na sahihi ya mwenyekiti wala katibu!

 

Licha ya kwamba nyaraka husika (anazozitumia kiongozi huyu kama ushahidi wa kupewa shamba) hazina uhalali wowote kisheria, kwa mujibu wa makabidhiano ya ardhi husika, kama ilivyoamuriwa na Kamati ya Ardhi ya Wilaya, Bwana Brown alitakiwa arejeshe ardhi ya kijiji (ekari 2000 za kilimo) mwaka  1985, na ardhi ya mifugo (ekari 3000 kwa ajili ya malisho) mwaka 2011. Mwaka  1985, shamba la kijiji halikurudishwa  (ekari 2,000), mwaka 1991 kada huyu aliendelea kupora ardhi  ya kijiji kwa kuongeza ukubwa wa eneo lake kutoka hekta 2,000 za awali hadi hekta 3,425 (ekari 8,000), ambayo ni hekta 1,425 zaidi ya kiasi ‘alichopewa’. Eneo hilo jipya liliingia kwenye Kijiji cha Lolksale  Wilaya ya Monduli.

 

Mheshimiwa Spika, kada huyu wa CCM, licha ya kutokuwa mmiliki halali wa eneo husika Agosti 31, 2009  kwa kushirikiana na watumishi wa Serikali wasio waaminifu walibadilisha  matumizi ya shamba  kutoka kilimo  na ufugaji  na kuwa hifadhi ya kitalii.

 

Uhalali wa kubadilisha matumizi ya ardhi na mwenye mamlaka ya kubadilisha matumizi

 

Kanuni na  na taratibu  za kubadilisha matumizi hazikufuatwa:

i)        Bango kwa lengo la kukusanya maoni  ya wananchi majirani kuhusu nia ya mmiliki kutaka  kuongeza matumizi  kama inavyotakiwa kwenye waraka wa kitaalamu Na.1  wa mwaka 2006.

ii)     Kibali cha Mkurugenzi wa Mipango Miji na Vijiji  kama inavyotakiwa  kwenye Sheria ya Mipango Miji  Na. 8  ya mwaka  2007 kifungu 32 (1) na 6 (3).

 

iii)   Kibali cha nyongeza ya matumizi katika miliki (Land Form na. 28) kimetolewa  na kusainiwa  na Paulo E. Kibona ambaye hana mamlaka  kisheria kusaini Fomu hiyo. Fomu hiyo husainiwa na Kamishna wa Ardhi kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi Namba 4 ya Mwaka 1999 kifungu 35(4).

 

Nyaraka ambazo Kambi Rasmi ya Upinzani inazo zinaonyesha kwamba Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, kupitia kwa Kamishna Msaidizi Kanda ya Kaskazini kwa barua yenye kumbukumbu na. LD /NZ/6014/22/DW ya Septemba  22, 2010  ilimtaka arejeshe hati iliyoofanyiwa mabadiliko ya matumizi….lakini alipuuza amri ya mamlaka halali! Hali iliyoilazimu  Kamishna  msaidizi kuandaa hati ya marekebisho  ya mabadiliko ya matumizi (deed of rectification) na kuiwasilisha kwa Msajili wa Hati Msaidizi Kanda ya Moshi ili afanye marekebisho kwenye daftari lake. Marekebisho  yalifanyika Januari 26, 2011 na kusajiliwa  kwenye FD. na. 29828 ambako matumizi kwenye hati yalitakiwa yabaki yale ya awali (japokuwa hakuwa na uhalali wowote wa umiliki).

 

Licha ya kuwa na uelewa wa mgogoro husika  bado Kada huyu wa CCM  aliuza eneo husika (ardhi ya kijiji) kwa raia wa kigeni, mmiliki wa Kampuni Maasai Steppe Conservancy Limited  mnamo Desemba  14, 2010.

Kwa mujibu wa taarifa za BRELLA, kampuni ya Maasai Steppe  Conservancy Limited ina hisa 10,000, kama ilivyoainishwa  hapa chini:

i)                   BCZV Holdings limited ni kampuni inayomilikiwa na  Baastian  Bruins  (Mdachi) na Jerome Bruins  (Mdachi) wana hisa 9,700.

ii)                 John Warren (Mwingereza ) ana hisa 100.

iii)               Brown Mathew ole Suya (Mtanzania) ana hisa 200.

 

Kutokana na hisa nyingi (9,800) za kampuni ya Maasai Steppe Conservancy kumilikiwa na wageni, ni dhahiri kwamba kampuni hiyo ni ya kigeni.

 

Kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi Namba 4 ya mwaka 1999, fungu la 20; kampuni/raia wa kigeni kabla ya kumiliki ardhi wanatakiwa wapate  kibali  (Certificate of Incentives) kutoka TIC. Utaratibu huu haukufuatwa! Wakati nchi inakabiliwa na changamoto kubwa ya ardhi kumilikiwa na wageni, kada/kiongozi wa Chama Cha Mapinduzi amegeuka kuwadi namba moja wa kuuza nchi kwa wageni.

 

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ana taarifa zote kuhusiana na uvunjwaji huu wa sharia kuanzia na uporaji wa eneo la kijiji, kubadilishwa kwa matumizi ya ardhi pasipo kufuata sheria na taratibu na kuuza ardhi kwa raia wa kigeni kinyume cha sharia za nchi. Waziri aliahidi kwenda kulishughulikia toka mwaka 2011 mpaka sasa hajatia mguu.

 

Kambi ya upinzani inataka kupata majibu ya maswali yafuatayo:

I)                   Wizara ya ardhi ilitumia vigezo gani kumpatia hati?

II)                 Wizara ilitoaje uhalali wa kubadilisha matumizi  ya ardhi?

III)               Wizara imeafiki vipi  umiliki wa ardhi kwa raia wa kigeni (Mdachi)?

IV)            Hatua gani zitachukuliwa kwa kada huyu wa CCM kwa  kukiibia kijiji na Watanzania ardhi yao na kwa kuvunja sheria?

1343 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!