Jumamosi iliyopita nilikuwa katika kipindi cha Jicho la Habari kinachorushwa na Televisheni ya Star. Moja ya hoja nilizozizungumza ni kubadili utaratibu wa sasa jinsi mikopo inavyotolewa kwa wanafunzi wa elimu ya juu. Binafsi nimejiridhisha pasipo shaka kuwa utaratibu huu umechangia kwa kiasi kikubwa kushusha kiwango cha elimu nchini.

Nimepata wazo hili baada ya kuwa nimetembelea vyuo kadhaa katika muda wa miaka kama mitatu iliyopita. Nimekwenda pale Iringa – Tumaini University College, nimekwenda Chuo cha Ushirika Moshi, nimeangalia wanavyuo wa St. Augustine cha Mwanza, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na vingine vingi jinsi wanavyosaga fedha.

 

Sitanii, najua makala hii baadhi ya wanafunzi hawataipenda na wataishia kunitukana. Fedha hizi ambazo wamezibatiza jina ‘bumu’zinawageuza vichaa watoto wetu. Nakumbuka wakati nasoma shule katika ngazi ya sekondari na chuo mimi sikupata kushika fedha mkononi. Mara zote, tulikuwa tunasafiri kwa warrant na chakula tulikuwa tunakula kwa coupon.

 

Hata wakati nakwenda jeshini, Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) nilipewa warrant ambayo iliniwezesha kupanda meli kutoka Bukoba hadi Mwanza, kisha nikapanda treni kutoka Mwanza hadi Dar es Salaam, hapo nikapanda treni ambapo nilisafiri kutoka Dar es Salaam hadi Arusha. Nikafika JKT Oljoro na kupangiwa CTS baadae nikapelewa Farming.

 

Pale farming tukawa tunachunga mitamba, tunakamua maziwa chini ya Afande Erick na Dadu Muna, bila kumsahau Koplo (wakati huo) Chiku. Ilikuwa tunakwenda kulenga shabaha, tunafanya kazi kwenye mashamba mawili; Dunia na Embakasi. Wakati huo akina Kibatara na Big Ox wakifanya zoezi la kukwepa ndege, huku akina Antipas Anathory wakijongo na kuishia kukaanga bisi mlimani.

 

Sitanii, akina Mussa Hassan Bujo na Waziri Ali Mdeme, wao hawakusita kwenda Milongoine, Nadosoito na Laroi, kila tulipopatiwa kichere (hapa ni jeshini si chuoni). Huko walikuwa wanakwenda kufanya kazi ya ‘ukemia’. Nimejaribu kuyazungumza haya zikiwa ni kumbukumbu za zaidi ya miaka 20 iliyopita. Wanachuo walikuwa wanapata uji safi, ugali na mara chache wali.

 

Ilikuwa chakula kikipungua ubora tunalalamika, mara chache kwa maandamano, kisha hali inarekebishwa tunarejea masomoni. Enzi zetu ilikuwa tunalala na kuamkia shuleni na vyuoni. Hatukupata kwenda kwenye klabu za usiku. Tulikuwa tunaandamana vitabu vikipungua kwenye maktaba, lakini leo ni kinyume.

 

Kinachonisikitisha ni kwamba Serikali imeharibu wanafunzi wetu. Kila siku wanapewa Sh 7,500 wanapokuwa vyuoni. Kwa mwaka fedha hizi ni wastani wa Sh 1,800,000 maana wanakaa vyuoni siku 240 kwa mwaka. Kiasi hiki bado kinaongezewa fedha za vitabu, utafiti na mafunzo kwa vitendo. Zikitolewa hizi, wanachuo wanapata wastani wa Sh 350,000 kwa mwezi kila kitu kikijumuishwa.

 

Badala ya fedha hizi kuzitumia vyema, wanafunzi walio wengi wanaziwekeza katika kununua kompyuta pakatwa, iPod, simu za gharama kama Blackberry, televisheni na redio kubwa. Wanashinda mabwenini wakiangalia picha za ngono badala ya kwenda darasani. Wakimaliza kuangalia ngono wanakwenda kunywa pombe wanalewa chakali.

 

Wakipata bumu baa zilizo jirani na Hosteli ya Mabibo kama  Zambezi, KGB, Chonya, ABC Hoteli ya Best Point na Lunch Time   hazifungwi kutokana na wanafunzi hawa kukesha wakinywa kwa kushindana kuanzia asubuhi hadi usubuhi siku ya pili.

 

Baadhi ya wanafunzi wanashindana kuvaa vidani vya dhabau na vito vya gharama kubwa. Hawa wanaokuwa wameishi maisha sawa na watu walioko kwenye mapumziko, wanapokwenda kazini wanakuta mshahara ni Sh 250,000 (tena wenye majukumu) wanakuwa wa kwanza kusema mishahara haitoshi. Wanashiriki vitendo vya ufisadi.

 

Sitanii, tena moja nimelisahau. Baadhi ya wanafunzi wananunua hadi magari kutokana na mikopo hii. Kwa bahati mbaya, fedha hizi zinakuwa hazitoshi hivyo wanaingizwa mikenge na ‘watoto wa mjini’ kwa kuuziwa magari mikweche kwa gharama za milioni mbili hadi tatu, ambapo baada ya muda mfupi mikweche hii inawadodea. Ninayo majina ya wanafunzi waliopata hasara kwa njia hii.

 

Ninachoamini, ni kwamba tumejaribu utaratibu huu umeua elimu yetu zaidi. Unawapa wanafunzi fursa ya kuwa walevi na wengine kugeuka malaya kwa kukimbizana na machangudoa mijini, badala ya kuwa darasani. Matunda yake tunayashuhudia. Wakija kazini hawajui kitu. Hata barua za maombi ya kazi wana-copy na ku-pest.

 

Sitanii, ni vigumu kutumikia mabwana wawili. Fedha na elimu haviwezi kwenda sanjari. Watoto wetu tuwape kazi moja tu ya kusoma shule, wakihitimu masomo wafanye kazi ya kutafuta fedha. Utaratibu wa sasa wa mikopo ufutwe. Wanafunzi wapewe warrant na coupon. Vyuo viwe na wapishi wa mikataba kama sisi tulivyokuwa na Kashekulo pale Nyegezi Social Training Institute.

 

Kwa kufanya hivyo, wanafunzi hawatakuwa na hamu ya kwenda baa, bali watakimbilia makitaba. Watakwendaje baa bila hela? Ni kwa njia hii muda mwingi watautumia kusoma na kutuwezesha kupata wasomi walioiva kweli. Narudia, najua wapo watakaokasilishwa na makala hii, ila nasisitiza utaratibu wa sasa haufai kwa maslahi ya elimu bora nchini. Ubadilishwe.

 

 

Please follow and like us:
Pin Share