Viongozi Maziwa Makuu waufanye kwa Uangalifu – 4

 

Tangu Kagame na RPF waitwae Rwanda ni wazi kuwa nchi hiyo inapokea fadhila za Washington DC kuliko nchi yoyote nyingine katika Maziwa Makuu.

Misaada ambayo inatoka Marekani na Uingereza kuelekezwa Kigali ni mingi na ya aina mbalimbali. Kwa hesabu rahisi misaada hiyo inafafanua ustawi wa uchumi wa Rwanda tunaouona leo.

Lakini cha ajabu katika hesabu hiyo ni jinsi ambavyo misaada inawekezwa. Kwa uwiano wa kimahitaji na wastani wa bajeti, Uingereza na Marekani huelekeza misaada kwenye ufadhili wa jeshi la RPA kupita sekta yoyote nyingine. Pana fumbo hapa!

Uwekezaji huo jeshini hauishii kwenye masuala ya fedha tu. Jeshi la Marekani limekuwa na mlolongo wa kupeleka wataalamu wengi Kigali kwa ajili ya mafunzo ya hapa na pale, hasa wataalamu waitao wa vikosi maalum. Hili tendo limesababisha ‘americanization’ ya Jeshi la Rwanda kiutaalamu.

Ukiangalia video za Jeshi la Rwanda wakati wa tafrija, sherehe za  mafunzo au programu mbalimbali – zilizopo kwenye ‘You-tube’, unawaona wanajeshi wengi ambao ipo wazi kuwa ni Wamarekani na Uingereza! Sasa wamekuwa ni kiungo cha uhai wa Jeshi la Rwanda.

Naomba nikukumbushe msomaji kuwa mwanzoni nilionesha kuwa Kagame, zaidi ya kuwa Rais wa Rwanda, ni mtihani kwa Maziwa Makuu. Hili ndilo linalonifanya nianze sehemu hii kwa kuonesha kuwa mpaka leo majeshi ya Marekani na Uingereza yameendelea kuwa ni sehemu ya egemeo la nchi hiyo. Tukumbuke kuwa haya ni mataifa mabepari.

Uwepo wa majeshi ya Marekani na Uingereza Rwanda kama alivyoelezea Bridgette Kasuka ni wa muda mrefu – toka miaka ya tisini. Hayo majeshi ya kigeni yamefanya kazi kulifundisha Jeshi la RPA likingali ni uasi na wakaendelea hivyo hata baada ya uasi huo kuwa Jeshi la Rwanda mwaka 1994.

Jamani huo unaitwa uwekezaji na usiamini kuwa Marekani na Uingereza ni wajinga wa kufanya hivyo bila kujua mustakabali. Walikuwa wakipalilia njia.

Kuliimarisha jeshi, wataalamu wanaonesha kuwa inahitaji kuwa na uzoefu wa operesheni za hapa na pale na makabiliano uwanja wa vita. Hili ni mbali ya mafunzo ya kila mara kambini na vyuoni. Pia kuwepo sehemu za vita kama walinda usalama ni namna moja ya kupata ‘exposure’. Haya yote hulifanya jeshi kuwa bora na makini.

Ona unafiki wa Marekani na Uingereza! Toka Rwanda iivamie Kongo mwaka 1996 – 1998, mataifa hayo yanaliorodhesha jeshi la Rwanda kama jeshi shupavu, lenye heshima na la kisasa. Hii imekuwa mbinu ya kulivumisha Jeshi la Rwanda kwenye korido za Umoja wa Mataifa (UN)!

Malengo makubwa ni Marekani na Uingereza kuliwezesha jeshi hilo kuteuliwa kwenye duru mbalimbali za kulinda usalama chini ya UN ili:

Kwanza, liendelee kuwa mstari wa mbele penye mapambano na makabiliano ili jeshi hilo liendelee kupata uzoefu wa kivita. Yaani, kulinoa ‘practically’! Kwa sababu toka mwanzo Jeshi la RPA lilitungwa kwa adhima hiyo, linatakiwa liwe bora katika hilo.

Pili, ili majeshi ya Rwanda yaendelee kuwapo katika mazingira ya kujifunza na kujua jinsi ya kutumia zana za kisasa za kijeshi! Rwanda haina bajeti ya kununua vyombo bora vitengenezwavyo kila kukicha. Marekani ingepata ugumu kufadhili hilo mara kwa mara!

Kwa kwenda kwenye duru za Umoja wa Mataifa mara kwa mara, basi vikosi vya Rwanda vinazitumia na kuzijua silaha za kisasa kwa kasi kuliko nchi nyingine katika Maziwa Makuu.

Tatu, majeshi ya Rwanda yanajikuta kwenye nafasi nzuri ya kuingiliana na kujuana na wengineo toka nchi mbalimbali. Hili ni jambo kubwa kiusalama na katika kutengeneza urafiki miongoni mwa ‘makamanda’.

Kwa taarifa yako msomaji wangu, hilo ndilo limewezesha ‘link’ ya uuzwaji haramu wa silaha kutoka nchi moja kwenda nchi nyingine katika soko bubu la dunia. Kuelewana kwa maofisa wa juu jeshini wakafunda yao mara nyingi si heri.

Kwa mfano, japokuwa ni kweli kuwa mafunzo ya pamoja kijeshi na mazoezi kama yale ambayo nchi za Afrika Mashariki zinaendesha yanaleta kujuana na uzoefu: Marekani na Uingereza wanayaunga mkono kwa sababu ni wakati murua wa kukusanya taarifa za kiintelijensia!

Ukiangalia wazo la mazoezi ya pamoja Afrika Mashariki lilitokea Rwanda na Uganda. Wanyarwanda walilihamasisha sana kwa madai kuwa litaleta usalama na kuaminiana!

Marekani ilikuwa nchi ya kwanza kusifia kuwa jambo hilo litaleta amani na ufanisi kiusalama. Mimi ninaogopa kuwa urafiki kati ya ‘makamanda’ wetu na ‘wengineo’ unaweza kupika uswahiba na kuzaa hujuma.Ushahidi wangu: Marekani imeutumia uhusiano wa aina hii kupenyeza rupia na kuiba taarifa nyingi za kijeshi!

Kwa mfano, makamanda wa Pakistani ndio walio ‘dukua’ taarifa za kijeshi Afghanistan kabla haijashambuliwa mwaka 2001.

Baada ya kuelekeza ni kwa mbinu zipi Marekani na Uingereza wametengeneza uimara kiusalama na uwezo ki-mbinu katika majeshi ya Rwanda naomba uelewe kitendawili cha uchumi wa nchi hiyo.

Tofauti na wengi wanaotembelea Kigali wakafikia kwenye hoteli za nyota kadhaa, wakabwatuka, ‘Rwanda imesonga mbele’ naamini kwa ushahidi kuwa uchumi wa Rwanda uko hivyo kwa sababu za nyakati. Si uchumi endelevu.

Nchi zote ambazo Marekani iliwachukua vibaraka ikawaandaa na kuwapa hatamu pia iliwatengenezea sifa ya hadhi. Iliwawezesha vibaraka hao kuratibu uchumi na kutengeneza uongozi wenye hadithi. Rwanda imepewa kijiko hicho pia. Uchumi wa Rwanda ni wa matokeo anuai:

Kwanza, huruma itokanayo na mauaji ya halaiki. Ni baada ya mauaji ya kimbari ambapo mataifa mengi duniani yaliletwa kuijenga Rwanda. Hili lilijitokeza kwa namna ya misaada ya ki-utu, mshikamano wa kiuchumi na kuwasaidia manusura wa mauaji.

Kwa sababu ya majonzi hayo Rwanda ilipokea thamani ya mamilioni ya dola kuliko mradi wowote ule wa ki-utu uliopata kunadiwa na viongozi Afrika.

Pili, ili Marekani na Uingereza waifanye Rwanda ‘Anglophone’ na baadaye mwanachama wa ‘Commonwealth’ japo si koloni la Mwingereza walitakiwa wawekeze Kigali. Katika hili Marekani iliikumbatia sana Rwanda kwa hali na mali huku ikizishawishi nchi nyingi duniani kuikopesha na kuifadhili RPF. Hili liliimwagia Rwanda mamilioni ya dola.

Tatu, toka Rwanda imalize vita ya mwaka 1994 Marekani na Uingereza wamebadilika kuwa ‘omba omba’ wa misaada na fadhila kwa niaba ya Rwanda. Hili limesababisha wafanyabiashara wakubwa Marekani (Howard Buffets, Bill Gates na wengineo) na Uingereza kumwaga fedha nyingi Rwanda. Hili limesaidia thamani ya maisha.

Aibu kidogo hii hapa: Mpaka leo Bill Clinton na Tony Blair wanaendelea kuwa ‘vipeperushi’ vya Rwanda kuiombea dola za ufadhili. Wameingiza fedha lukuki.

Nne, uvamizi wa Zaire ambayo sasa inaitwa Kongo. Ukisoma wataalamu wengi wa uchumi wanaoichambua Rwanda wanaonesha takwimu elekezi. Toka mwaka 1996 baada ya kuitwaa Kinshasa, Rwanda, Uganda na Burundi zimebadilika na kuwa ‘majangili’ dhidi ya nchi jirani.

Takwimu za wataalamu wa UN (2012) zinaonesha Jeshi la Rwanda kwa kuendesha uporaji ama wa moja kwa moja, au kupitia vikundi vya uasi Kongo chini ya Laurent Nkunda, Bosco Ntaganda, Sultani Makenga na wengineo wengi limekuwa na wastani wa kuchuma dola milioni 60 za Kimarekani kwa mwezi! Hesabu hiyo inamaanisha wameiba kutoka Kongo dola 720,000,000 kwa mwaka.

Ona sasa yale magorofa, kasino na majumba mazuri ya Kigali, barabara, umeme, maji, benki na shule vimetoka wapi!

Kwa vile uasi umeanza mwaka 1996 na umeisha 2013 ni sawa na miaka 17. Dola 720,000,000 kwa mwaka ukizidisha miaka 17 ni sawa na dola 12, 240, 000,000. Naomba ujue kuwa haya ni makadirio ya chini kwa mujibu wa taarifa za wataalamu wa UN.

Fedha hizo zimetokana na uibaji, uporaji na unyang’anyi wa mali kutoka Kongo Mashariki, kama vile dhahabu, almasi, shaba, ‘coltan’ na ‘cobalt’. Msomaji wangu, unaweza kuipata nakala ya ripoti hiyo ya wataalamu wa Umoja wa Mataifa kwenye mtandao. Pia wataalamu wengi wamelionesha hili na nakala zao zipo mitandaoni.

Wakati huo huo, Rwanda, Uganda na Burundi zilichanua na kuwa wauzaji wakubwa wa madini yatokayo Kongo kwa kiwango ambacho Kongo yenyewe haijapata kufikia.

Kwa mfano, takwimu za ripoti hiyo hiyo ya Umoja wa Mataifa zinaonesha kuwa Rwanda ilikuwa imefikia kiasi cha kuuza na kusafirisha madini yenye thamani ya dola milioni 6.7 za Kimarekani kwa siku. Hizi ni tofauti na hizo tulizozitaja hapo juu ambazo ziliporwa na jeshi. Cha kushangaza ni kwamba Rwanda haina hata shimo moja la kuchimba madini hayo!

Uchunguzi wa jopo la UN ukathibitisha kuwa Rwanda ilikuwa imetengeza mtandao wa kuvusha thamani za Kongo mpaka Kigali na baadaye kuziuza kama madini halali yatokayo Rwanda.

Nadhani kufikia hapa, msomaji wangu, utakuwa unaona ni jinsi gani Rwanda imepata kuwa na uchumi ilionao sasa. Uchumi ambao unazifanya Marekani na Uingereza kuisifia. Kwa kifupi ni kwamba Rwanda ina uchumi uliojengwa kwa machozi, jasho, damu na yatima Wakongo. Uchumi wenye laana!

Marekani na Uingereza, nchi kubwa, wamekiuka misingi ya kibinadamu na utu. Wametekeleza ‘umafia’ dhidi ya Kongo, tena kwa gharama kubwa ya damu ya watu wa Kongo na Rwanda. Hata wale ambao ni wahanga, ambao Marekani na Uingereza wanawajua, wameteketezwa na kuuawa ili kuhalalisha uvamizi dhidi ya Kongo.

Makala ijayo, ya mwisho juu ya Kagame ni mtihani, nitatoa ushahidi wa kina ujue kwanini Rwanda haina hadhi ya kujiita taifa lililofanikiwa kuhamasisha ukuaji wa kiuchumi.

Uchumi wa Rwanda si endelevu na hautapata kuwa endelevu kwa sababu ni ‘mtego wa ukoloni mamboleo’. Nitawasilisha kwanini wakulaumiwa kwa mauaji ya halaiki wa kwanza ni Marekani na Uingereza; wa pili Paul Kagame, halafu wa tatu – Interahamwe na RPF!

Itaendelea

wagfterc@gmail.com

2749 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!