DC adaiwa kumtisha Roboyanke

Mwenyekiti wa Kijiji cha Mnyara, Makoye Roboyanke (CCM), ambaye inadaiwa alivuliwa madaraka hayo na Mkuu wa Wilaya ya Geita, Manzie Mangochie, amedai kuwa Septemba 10, 2013 mchana akiwa shambani kwake kijijini hapo, alipokea simu ya vitisho kutoka kwa kiongozi huyo wa Serikali.

“Alijitambulisha kwa jina moja la Mangochie na kwamba ndiye Mkuu wa Wilaya ya Geita, akaniuliza jina langu nami nikamjibu… akaniuliza ninachofanya kwa wakati huo na kazi yangu hasa ni nini, nikamwomba arekebishe kauli, na baada ya kurekebisha kauli na kuniuliza maswali ya msingi nilimpa ushirikiano.

“Nilimwambia mimi ni Roboyanke, naishi  Mnyara, ndipo nilipozaliwa, kazi yangu ni mkulima na sasa nipo shambani. Akaniuliza wewe ni kiongozi? Nikamjibu kwamba suala la uongozi wanajua wananchi, akakata simu,” amesema Roboyanke.

Hata hivyo, Roboyanke amedai kuwa siku chache baada ya maongezi yake na Mangochie, Septemba 24, 2013 alipokea barua yenye Kumbu. Na NK/DC/MIC/5/28 kutoka kwa Afisa Mtendaji wa Kata ya Nkome, Frances Kagoma, inayosomeka kama ifuatavyo:

YAH: KUACHISHWA UONGOZI WA KIJIJI CHA MNYARA NA KITONGOJI CHA MAKURUGUSI

Rejea mada tajwa hapo juu. Nimepokea maagizo toka kwa Mkuu wa Wilaya ya Geita, Manzie Mangochie, ya tarehe 24/09/2013 saa 11:20 jioni, umeachishwa uongozi ulionao kwa kuwa wewe ni mfungwa wa shauri namba 23/2012 na hukumu ilitolewa kwenye Mahakama ya Mwanzo Bugando 08/6/2012.

Kuanzia tarehe ya barua hii si Mwenyekiti wa Kijiji na Kitongoji, umeamuriwa kurudisha vifaa vya Serikali unavyofanyia kazi za kiofisi kwa Mtendaji wa Kijiji cha Mnyara.

Nakala ya barua hiyo ilipelekwa kwa DC huyo kwa taarifa ya utekelezaji wa agizo lake la 24/09/2013, Mkurugenzi wa Wilaya ya Geita, Diwani wa Kata ya Nkome na Mtendaji wa Kijiji cha  Mnyara, ili ahakikishe anafuatilia vifaa alivyokuwa navyo ukiwamo muhuri wa Kijiji na Kitongoji cha Makurugusi.

“Baada ya kupokea barua hiyo, nilifunga safari hadi ilipo ofisi ya mtendaji wa kata na nilipofika nilimwambia siko tayari kukabidhi vifaa hivyo hadi nitakapopokea barua kutoka kwa DC mwenyewe, ikinitaka nifanye hivyo au kutoka ofisi ya Mkurugenzi wa Wilaya,” anasema Roboyanke.

Roboyanke akamatwa, akubali yaishe

Roboyanke anasema baada ya kugoma kukabidhi vifaa hivyo, Oktoba 8, 2013 mkuu huyo wa wilaya alitumia askari polisi kumkamata na kumfikisha katika Kituo Kidogo cha Polisi cha Nkome kwa hatua zaidi.

“Nikiwa kituoni hapo, askari mmoja aitwaye Telana alimpigia simu Mangochie kumtaarifu kuwa wameshanikamata na nilimsikia Mangochie akitoa maelekezo nihakikishe ninakabidhi vifaa vya ofisi mara moja na kama nitakataa niwekwe rumande.

“Nilichowaeleza wale polisi ni kwamba kwa kuwa hiyo kazi ya uenyekiti si baba yangu wala mama, ambayo siku moja ningepata urithi wake baada ya kumaliza muda wangu wa kiuongozi, nilikubali kukabidhi vifaa hivyo kwa maandishi na nilivikabidhi kwa Ofisa Mtendaji wa Kata ya Nkome, nikiwa chini ya ulinzi wa polisi akiwapo askari G8305 PC Simon Miyomba,” anasema.

DC aitisha uchaguzi mdogo

Aliongeza kuwa baada ya kukabidhi vifaa hivyo na kuvuliwa kinyemela nyadhifa alizokuwa nazo, Oktoba 22, 2013 Mkuu huyo wa wilaya alizuru kijijini Mnyara akiwa amefuatana na askari polisi akaitisha mkutano wa hadhara.

Kwa mujibu wa Roboyanke, baada ya wananchi kujikusanya, Mangochie alisema “… naitisha uchaguzi mwingine na uwe wa kura za wazi kwa kujipanga mgongoni kwa mgombea.’’

Hata hivyo, Roboyanke anasema mkuu huyo wa wilaya hakuweza kufanikisha shughuli ya uchaguzi kwa siku hiyo, badala yake alizungumzia mambo machache ya uchaguzi na kimaendeleo kijijini hapo, kisha akaondoka akiahidi kufanyika kwa uchaguzi huo muda mfupi ujao.

Uchaguzi waitishwa kwa mara ya pili

Roboyanke anasema Desemba 3, 2013 kama alivyoahidi Mangochie, uliitishwa uchaguzi mdogo wa Mwenyekiti wa Kijiji kwa utaratibu wa kura za wazi, ambapo CCM ilimteua Evalist Musiba na Chama cha Wananchi (CUF) kilimsimamisha Pastori Mashauri kugombea wadhifa huo.

Inaelezwa kwamba mgombea wa CUF alionekana kupata kura nyingi dhidi ya mgombea wao wa CCM, lakini cha ajabu msimamizi wa uchaguzi ambaye ni Mtendaji wa Kijiji hicho, Peter Mlela, aligoma kutangaza matokeo ya uchaguzi huo.

Uchaguzi waitishwa tena, CCM yabwagwa tena

Desemba 14, 2013 uchaguzi ulifanyika kwa mara nyingine ambapo safari hii CCM ilisimamisha mgombea mwingine, Kamuli Kanumbu, kwa kudhani yule wa kwanza hakuwa na mvuto wakati CUF ilimsimamisha yule wa awali.

“Zilipigwa tena kura za kusimama mgongoni kwa mgombea, lakini CCM kwa mara nyingine walibwagwa na mgombea yule wa CUF, na hata uchaguzi huo waligoma kutangaza matokeo na mpaka leo kijiji hakina mwakilishi wa wananchi,” anasema.

Kutokana na hali hiyo, ilizuka tafrani ya wananchi wakitaka watangaziwe matokeo, hali ambayo ilimfanya msimamizi wa uchaguzi huo kutimua mbio kujinusuru na kipigo kutoka kwa wananchi hao.

Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Mnyara, Peter Mlela, alikiri uchaguzi huo wa wazi kufanyika huku akidai kuwa aliyewaamuru kufanya hivyo huku wakijua ni kinyume cha taratibu za uchaguzi ni mkuu wa wilaya hiyo.

“Ni kweli uchaguzi wa kwanza nilisimamia mimi, lakini kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wangu uliahirishwa tena na aliyeniagiza ni Mkuu wa Wilaya ya Geita, Mangochie.

“Uchaguzi wa pili ambao pia matokeo hayakutangazwa muulize Mtendaji wa Kata maana ndiye aliyesimamia, lakini baadaye tulipokea maagizo kutoka ofisi ya Mkurugenzi kwamba hatupaswi kufanya uchaguzi wa wazi, kwani ni kinyume cha utaratibu na wakadai wanafanya utaratibu wa kuitisha uchaguzi unaoruhusiwa kisheria wa kura za siri, hivyo mpaka sasa tunasubiri maelekezo kutoka kwa Mkurugenzi,” amesema Mlela.

Fedha za maendeleo zatafunwa

Uchunguzi uliofanywa na JAMHURI umebaini kuwa lengo la kung’olewa kwa Roboyanke ni kutafuta upenyo wa kufuja fedha za Serikali zinazotolewa kijijini na kata hiyo kugharimia maendeleo.

Imebainika kwamba tangu mwenyekiti huyo avuliwe madaraka, mamilioni ya shilingi yameshatafunwa na hakuna hatua zozote zilizochukuliwa dhidi ya wahusika.

Fedha zinazodaiwa kuyeyuka ni za ujenzi zilizokuwa zimepangwa kumalizia Kituo cha Polisi cha Nkome, zilizotolewa na Halmashauri ya Wilaya ya Geita.

Fedha nyingine zilizoyeyuka ni za waathirika wa Ukimwi ambapo shilingi zaidi ya milioni tatu hazijulikani zilipo. Imebainika kuwa fedha zilizotolewa na halmashauri hiyo kwa ajili ya kusaidia waathirika hao ni Sh milioni 7.3.

Mgawanyo wa fedha hizo kwa waathirika hao walioko katika vikundi vinne — Huruma, Tumaini, Upendo na Amani– kwa kila kikundi ni Sh 1,056,000. Hivyo, fedha zilizotoka ni Sh 4,224.

Kwa hiyo, fedha ambayo haijulikani ilipo ni Sh 3,168,000 ili kukamilisha kiasi kilichotolewa na Halmashauri ya Wilaya mwanzoni mwa mwaka huu.

Wananchi wamtuhumu DC

Wakizungumza na JAMHURI, baadhi ya wakazi wa kata hiyo wameelekeza lawama zao kwa Mkuu wa Wilaya ya Geita, Mangochie, kwamba ndiye chanzo cha upotevu wa fedha hizo baada ya kumvua madaraka mwenyekiti wao aliyekuwa mstari wa mbele katika kupambana na mchwa kwa kutekeleza Ilani ya CCM ipasavyo.

“Yaani amemng’oa mwenyekiti wa chama chake, lakini leo DC huyu amesababisha hiki kijiji kiwe na upinzani kiasi kwamba kwa sasa hata wapinzani wakiweka jiwe wanapita… na ninyi waandishi mtusaidie kufikisha kilio chetu,” amesema Justa Mashauri, mkazi wa Mnyara.

Kwa upande wake, Renartus Nkuba amesema kitendo cha mkuu huyo wa wilaya kumng’oa Roboyanke kimewapa wakati mgumu kuinadi CCM kijijini hapo, kwa kile alichodai mbali ya kuwa eneo hilo lilikuwa ngome ya chama hicho, kwa sasa ni ngome ya upinzani kutokana na tukio hilo kuwachukiza wapigakura wa mwenyekiti aliyevuliwa madaraka.

DC avuruga mkutano wa CCM

Kituko kingine kinachoashiria ni kuivuruga CCM huku akiwa ni kada wa chama hicho, ni tukio lililotokea baada ya Mangochie kujibu swali la Mkazi wa Kata ya Kasamwa, Godwine Kasazi, katika mkutano wa hadhara wilayani Geita.

1451 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!