Kagasheki atiwa majaribuni

Kundi la wafanyabiashara kadhaa wa tasnia ya uwindaji wa kitalii, limekutana nchini Marekani na kuendesha mchango wa mabilioni ya shilingi kufanikisha ugawaji upya wa vitalu vya uwindaji.

Habari za uhakika zilizopatikana kutoka ndani ya Wizara ya Maliasili na Utalii, zimesema fedha hizo zimechangwa kwa kivuli cha kusaidia shughuli za uhifadhi nchini, lakini ukweli wa mambo ni kwamba zimepangwa kutumiwa kuwarubuni baadhi ya viongozi waandamizi wa Wizara hiyo pamoja na vyombo vya dola, hasa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na Mahakama.

 

Kiasi cha dola za Marekani zaidi ya 600,000 kimekusanywa kuhakikisha mpango huo unafanikiwa wakati wowote kuanzia sasa. Dola moja ya Marekani ni wastani wa Sh 1,600.

 

Mpango huo unasukwa ilhali Ikulu, na baadaye Wizara ya Maliasili na Utalii Januari, mwaka jana, zilitoa taarifa ya kutorejewa ugawaji vitalu.

 

Sehemu ya tangazo la Wizara ya Maliasili na Utalii kwa umma, kupitia kwa Msemaji wake, George Matiko, lilisomeka: “Wizara ya Maliasili na Utalii haina mpango wa kurudia ugawaji wa vitalu. Mchakato wa ugawaji ulikamilika mwezi Septemba mwaka jana (2011) na matokeo yake kutangazwa wazi.


Mapema mwezi Septemba 2011, Wizara ilitoa orodha ya kampuni 60 zilizofanikiwa kugawiwa vitalu. Kati ya kampuni hizo, kampuni 51 ni za kizalendo na kampuni 9 za kigeni kwa kuzingatia kifungu 39(3)(b) cha sheria ya wanyamapori Na. 5, ya 2009.


Hata hivyo, kumekuwa na taarifa mbalimbali zilizoripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari kuhusu kuwepo kwa harakati zinazofanywa na waombaji waliokosa vitalu, zikihusisha kuchafuana baina ya kampuni zilizopata na zilizokosa kwa nia ya kuzorotesha sekta ya uwindaji wa kitalii kwa ujumla. Vyombo hivyo vimeripoti kuwa mchakato wa ugawaji wa vitalu utarudiwa.


Wizara inasisitiza kuwa mchakato wa ugawaji wa vitalu hautarudiwa na Watanzania wanahakikishiwa kuwa hatua zilizochukuliwa na serikali za kuleta mabadiliko kwenye sekta hii tangu mwaka 2008, zimesaidia sana kuimarisha usimamizi wa sekta hii.”

 

Uchunguzi wa JAMHURI umebaini kuwa mkakati huo umeratibiwa na mmoja wa wadau kwenye tasnia ya uwindaji, mwenye ushawishi mkubwa anayeishi mkoani Arusha.


Mdau huyo ambaye anashirikiana na baadhi ya raia wa kigeni, amekuwa akihaha kupata vitalu ambavyo kwenye mgawo halali uliokwishafanyika walipewa Watanzania wazawa.


Tangu wakose vitalu hivyo, mdau huyo ambaye kwa sasa jina lake tunalihifadhi, amethubutu kutumia njia mbalimbali zikiwamo za kuwaghilibu wabunge pamoja na viongozi waandamizi serikalini katika kuhakikisha anapata vitalu hivyo.


Moja ya sababu zake ni kwamba kugawanywa kwa vitalu kulikofanywa na wataalamu katika maeneo kadhaa, hasa katika mikoa ya Arusha na Manyara kunaathiri ikolojia.

 

Kwa kuamini kuwa mpango wake wa kupata vitalu kutoka kwa wazawa wenzake utafanikiwa, hadi sasa kampuni nne alizo na uhusiano nazo wa karibu hazijakabidhiwa barua.

 

Chanzo cha habari kimedokeza kwamba Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, licha ya kutamka mara kwa mara, na hata kutoa taarifa rasmi kwenye vyombo vya habari kwamba ugawaji vitalu hautarejewa, sasa anaelekea kukubaliana na kundi linaloshinikiza kurejewa upya ugawaji huo.


Imeelezwa kwamba ameshauriwa kuwa ili kutojiweka kwenye utata na mgongano wa kauli, suala la ugawaji upya wa vitalu sasa liamuriwe na Mahakama Kuu.


Wiki iliyopita kundi la wafanyabiashara hao lilikuwa, ama likutane na viongozi waandamizi wa Wizara ya Maliasili na Utalii mjini Dodoma, au jijini Dar es Salaam kuweka mambo sawa.

 

“Mikutano ya Dodoma na Dar es Salaam ililenga kuhakikisha mahakama inatumiwa kutengua uamuzi wa awali wa ugawaji vitalu. Hawa watu wanajiamini sana.

Wakiwa Marekani wakawa wanawatisha watu wasiuze safari wakisema ugawaji vitalu unarudiwa.


“Njia nzuri iliyoonekana ni ya kuitumia mahakama kubadili uamuzi wa awali. Fedha zilizochangwa zimelenga kutolewa kwa viongozi kadhaa waandamizi ndani ya Wizara ya Maliasili na Utalii na pia ikiwezekana zitumike kuweka mambo sawa mahakamani.


Haya mambo ni ya siri sana, lakini ukweli ndiyo huo,” kimesema chanzo chetu cha habari.

Habari zilizovuja kutoka kwa mmoja wa viongozi wakubwa kabisa wizarani humo, zimesema kwamba kigogo huyo amewataka wafanyabiashara hao wakae kimya, wahakikishe mkakati huo hautolewi kwenye vyombo vya habari.


Aidha, katika kuupa nguvu mpango huo, mmoja wa watoto wa viongozi waandamizi serikalini anayesifika kwa kujiingiza kwenye kila biashara iliyo mbele yake, anatajwa kutumika.


Mtoto huyo hivi karibuni alisafiri kwenda Uarabuni ambako alikutana na koo za kifalme zinazosaka kwa udi na uvumba vitalu vya uwindaji wa kitalii.  Wakati mpango huo ukisukwa, imebainika kuwa kampuni kadhaa za Watanzania zilizopewa vitalu, zimeviuza kwa matajiri raia wa kigeni.


Mmoja wa wanaotajwa kuviuza ni mtu wa karibu na mmoja wa mawaziri walioondolewa wizarani hapo.


Pamoja na ukweli kwamba jambo hilo ni kosa kwa mujibu wa Sheria ya Wanyamapori Namba 5 ya mwaka 2010, Wizara ya Maliasili na Utalii imeendelea kuwa kimya.