Pengine mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara Simba, wangetamani kuona Kagera Sugar hairudi ligi kuu, lakini ndiyo kama ulivyosikia wamerudi.

Uzoefu na mipango vimezifanya timu za Kagera Sugar na Mwadui kurejea ligi kuu msimu ujao wa 2019/2020, timu hizo zimefanikiwa kubaki ligi kuu baada ya mechi za marudiano ya ligi ya mchujo.

Kagera Sugar imewafunga Pamba ya Mwanza 2-0, katika mchezo uliopigwa katika Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba, mechi ya kwanza ilipigwa jijini Mwanza ambapo timu hizo zilitoka suluhu.

Wachimba Almasi, Mwadui kutoka Shinyanga, wao waliifunga Geita Gold 2-1, katika mechi kama ya Kagera Sugar, hivyo kubaki ligi kuu.

Mechi ya kwanza timu hizo zilitoka suluhu, hivyo ushindi wa Mwadui umekuwa muhimu sana. Kabla ya timu hizo kukutana kuna hali ya tafrani ilizuka kutokana na mgogoro wa kimasilahi. Kutokana na kuwagomea Azam Media Group kuonyesha mtanange huo.

Kocha wa Kagera Sugar, Mecky Mexime, amesema alijua timu yake itashinda na wataendelea kusalia katika ligi kuu kwa msimu mwingine unaokuja.

“Sikuwa na presha yoyote…nilijua hawa Pamba tutawachinja tu. Lakini pamoja na kushinda na kusalia ligi kuu, kuna upungufu ambao nitauzungumzia kwa uongozi ufanyiwe kazi.

“Ninamshukuru Mwenyezi Mungu, tumebaki ligi kuu. Lakini tumejifunza kitu ambacho nadhani msimu ujao tutarekebisha makosa ili tusiende huku,” amesema Mexime.

Kocha wa Mwadui, Ali Bushiri, amefanikiwa kuibakiza timu yake katika ligi kuu katika msimu ujao. Naye kama yule wa Kagera Sugar amesema watayafanyia kazi makosa yaliyojitokeza kwenye ligi kuu.

Akitoa maoni yake baada ya mchezo, Kocha wa timu ya Pamba, Ally Kisaka, amesema kulikuwa na mbinu za nje ya uwanja, ikiwamo polisi kuwatisha wachezaji wake.

“Tangu siku ya kwanza tunakuja kufanya mazoezi Kaitaba, kumekuwa na vitendo vya ajabu kutoka kwa askari polisi, tunajua hizo zilikuwa mbinu chafu kuwatisha wachezaji wangu.

“Mpira wa miguu hauhitaji vitisho, tumetishwa sana hadi wakati tunaingia kwenye mchezo, hizo si mbinu za soka…” amesema Kisaka.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Brigedia Jenerali Marco Gaguti, amesema msimu uliopita Kagera Sugar walijisahau hadi wakacheza katika hatua ya mtoano ili kusalia katika ligi kuu, huku akiahidi msimu ujao watajipanga vizuri.

By Jamhuri