Takriban siku tatu zimebaki kabla ya michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kuanza rasmi mwaka huu. Katika michuano hiyo mechi nyingi zitachezwa katika makundi manne, na kila kundi hujumuisha timu nne. Kuanzia kundi A, ambalo linaongozwa na timu mwenyeji, timu ya taifa ya Misri hadi kundi F.

Waandaaji wa mashindano hayo, Misri wakiwa katika kundi hilo la A, wataongozwa na nahodha wao, Mohamed Salah, wakianza kucheza katika mchezo wa ufunguzi dhidi ya timu ya taifa ya Zimbabwe siku ya Ijumaa katika Uwanja wa Kimataifa wa Cairo.

Mashindano hayo yanaweza kuja katika muonekano tofauti na miaka mingine iliyopita kwa sababu yanafanyika wakati ambao ligi nyingi zimehitimisha msimu.

Itakumbukwa kuwa katika fainali za mwaka 2017, kwenye michuano ya aina hii hali ilikuwa tofauti, wachezaji walikuwa wanazitumikia timu zao za taifa kwenye michuano hiyo katika wakati ambao vilevile walikuwa wanashiriki katika ligi mbalimbali na hata katika mashindano mengine ya klabu, tofauti na ligi hizo.

Kwa sababu hizo, imekuwa ikielezwa kuwa wachezaji wengi wamekuwa na uzembe katika kujituma kwa sababu ya kuhofia kuumia, lakini imekuwa ikielezwa kuwa miongoni mwa wachezaji wamekuwa hawajitumi kwa kiwango cha juu kutokana na kutopewa posho ya kutosha katika timu zao za taifa ikilinganishwa na kiasi wanachopata wakiwa katika klabu zao.

Lakini huenda hali ni tofauti katika fainali za msimu huu, ushindani unatarajiwa kuwa mkubwa kutokana na sababu nyingine, mojwapo ni wachezaji wengi kung’aa katika klabu zao hususan wanaocheza barani Ulaya, wachezaji hao ni pamoja na Mohamed Salah wa Misri ambaye ameshinda zawadi ya kiatu cha mfungaji bora katika Ligi Kuu ya Uingereza.

Mchezaji mwingine ni raia wa Senegal, Sadio Mane, na raia wa Cameron, Joel Matip, ambao wanakipiga katika Klabu ya Liverpool.  Lakini kuna Mtanzania, Mbwana Samatta, ambaye ameshinda kiatu cha ufungaji bora katika Ligi Kuu ya Ubelgiji. Vilevile yupo raia wa Ivory Coast, Wilfried Zaha.

Katika fainali za msimu huu, ushindani ni dhahiri; kwa mfano, mchezo kati ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) dhidi ya Uganda, huu ni mtanange wa pili kuchezwa baada ya Ijumaa itakapoanza mechi ya utangulizi, kati ya Zimbabwe dhidi ya mwenyeji timu ya taifa ya Misri.

Licha ya timu ya taifa ya DRC kuundwa na wachezaji wengi wanaocheza nje kama Yannick Bolasie, Cedric Bakambu, Remi Mulumbu, timu ya taifa ya Uganda ni timu isiyostahili kubezwa.

Mchezo kati ya Senegal na Algeria ni mechi nyingine ngumu katika kundi C, ambalo linajumuisha timu za Kenya na Tanzania. Timu za Senegal na Algeria zinatarajiwa kuweka ushindani mkali zaidi kutokana na kuwa na wachezaji wanaocheza Ulaya au katika ligi nyingi zenye ushindani wa hali ya juu. Wachezaji hao ni pamoja na Riyad Mahrez, Sadio Mane, Idrissa Gueye na wengine wengi.

Mchezo wa Ivory Coast dhidi ya Afrika Kusini nao utakuwa wa aina yake. Timu hizi zinazopatikana katika kundi D zinajumuisha timu za Namibia, Morocco, Ivory Coast na Afrika Kusini. Mechi hii itachezwa Juni 24, na itakuwa mechi ya ufunguzi katika kundi hili.

Mechi hii itakuwa ngumu kutokana na timu ya Ivory Coast kuwa na historia nzuri katika mashindano hayo, ikitajwa  kuwa na wachezaji wengi wanaocheza soka la ushindani barani Ulaya, wakati timu ya Afrika Kusini ikiundwa na wachezaji ambao baadhi licha ya kucheza ligi ya ndani wamekuwa na ubora wa hali ya juu kutokana na ligi hiyo ya ndani kuwa ya kiwango cha juu cha ushindani.

Lakini mchezo kati ya Kenya na Tanzania huenda pia ukawa mchezo wenye ushindani wa hali ya juu kutokana na kucheza soka linalofanana na kwa kiasi fulani ligi za Kenya na Tanzania zinaendana katika viwango vya wachezaji, na uzoefu unaonyesha kuwa mara kwa mara timu hizi zinapokutana, mojawapo inaweza kuibuka mshindi.

1012 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!