Taifa Stars imeanza vibaya mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) kwa kukubali kipigo cha magoli 2-0 dhidi ya Senegal (Simba wa Teranga) katika dimba la Juni 30, jijini Cairo, Misri.

Goli la kwanza la Senegal lilifungwa na Keita Balde katika dakika ya 28 ya kipindi cha kwanza. Bao hilo lilidumu hadi kipindi cha pili baada ya Diatta kufunga goli la pili katika dakika ya 64.

Dakika 45 za kwanza zilionyesha Taifa Stars kuelemewa, huku kutoelewana kimchezo kwa viungo wa Stars kukitumiwa kama kombeo la kuiangamiza.

Upungufu uliojitokeza katika idara ya kiungo ulimlazimu Kocha wa Stars, Emmanuel Amunike, kumpumzisha Feisal Salum katika dakika ya 44 ya kipindi cha kwanza na nafasi yake ikachukuliwa na Farid Musa.

Mchezo huo ambao umefuatiliwa kwa karibu na Watanzania wengi, ulishuhudia wachezaji wanne wa Taifa Stars wakionyeshwa kadi za njano. Wachezaji hao ni Simon Msuva, Himid Mao, Feisal Salum na Hassan Kessy.

Taifa Stars itacheza mechi ya mzunguko wa pili keshokutwa (Alhamisi), mechi itakayowakutanisha na Kenya, ambao mechi yao ya kwanza walicheza na Algeria.

Kiwango cha umiliki wa mpira kilikuwa upande wa Senegal ambao walimiliki mpira kwa asilimia 61 ikilinganishwa na Taifa Stars iliyomiliki mpira kwa asilimia 39 tu.

Simba wa Teranga walipiga mashuti 23, kati ya hayo ni mashuti 13 ndiyo yalilenga goli huku mawili yakitinga nyavuni na kumwacha mlinda mlango wa Taifa Stars, Aishi Manula, akiwa hana la kufanya.

Kinyume chake ni kwamba Taifa Stars ilipiga mashuti matatu ambayo pia hayakulenga goli.

Mshambuliaji tegemeo wa Senegal na Klabu ya Liverpool, Sadio Mane, hakucheza katika mechi ya Taifa Stars kutokana na adhabu ya kutumikia kadi mbili za njano alizozipata wakati wa kusaka tiketi ya kushiriki AFCON.

Kutokana na kipigo hicho, Taifa Stars wanahitaji kupambana ili kuhakikisha wanashinda michezo yote iliyosalia, ambapo mchezo wa pili watacheza siku ya Alhamisi dhidi ya timu ya taifa ya Kenya ( Harambee Stars).

Alama tatu katika mchezo huo ni muhimu ili kurejesha matumaini ya kusonga mbele katika hatua zinazofuata kabla ya kuvaana na timu ya taifa ya Algeria katika mchezo wa kuhitimisha hatua ya makundi.

Kabla ya mchezo huo timu ya Senegal na Tanzania zilikutana mwaka 2007 wakati Stars ilikuwa ikinolewa na Kocha Mbrazil, Marcio Maximo, katika mchezo wa awali katika hatua ya kutafuta tiketi ya kufuzu kucheza Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2008, ambapo Simba wa Teranga walishinda magoli 4-0.

Mchezo wa marudiano uliofanyika Tanzania katika dimba la CCM Kirumba, jijini Mwanza walitoka sare ya 1-1.

Taifa Stars iko kundi C, ikiwa pamoja na Kenya, Senegal na Algeria.

1898 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!