Wiki iliyopita, wadau wa habari kupitia Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari Tanzania (MOAT), waliunda kamati ya watu 16 kwa ajili ya kukutana na wakuu wa vyombo vya usalama nchini.

Kamati hiyo, inayoongozwa na Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Dk. Reginald Mengi, imekabidhiwa majukumu ya kukutana na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi; Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Said Mwema; na Mkuu wa Usalama wa Taifa, Othman Rashid, miongoni mwa viongozi wengine.

 

Mazungumzo ya kamati hiyo na viongozi husika yamepangwa kujikita katika suala la usalama wa wananchi wanaolengwa na vitendo vya kutekwa, kushambuliwa na kuuawa nchini.

 

Inakumbukwa kwamba kamati hiyo imeundwa siku chache baada ya Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) na Mhariri Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya New Habari (2006) Limited, Absalom Kibanda, kutekwa na kushambuliwa hadi kuumizwa vibaya.


JAMHURI na Watanzania kwa jumla tunatambua na kuthamini umuhimu wa vyombo vya habari katika jamii, hivyo tunasubiri kwa shauku kuu kusikia matokeo ya kamati hiyo yanaleta ufumbuzi thabiti wa tatizo kulegalega kwa usalama wa raia nchini.


Tukio la kuumizwa kwa Kibanda na mengine kadhaa ya aina hiyo yaliyotangulia, yamesababisha Watanzania kuishi kwa hofu ya kutekwa, kushambuliwa na kuuawa wakati wowote ndani ya nchi yao huru.


Mengi na wajumbe wengine wa kamati hiyo ya wadau wa habari wajue kuwa jukumu walilokabidhiwa limebeba matumaini ya Watanzania katika suala zima la usalama wa maisha yao.


Kwa msingi huo, matarajio ya wengi ni kwamba kamati hiyo itaibuka na mawazo, ushauri au mpango mkakati wa kisayansi utakaokuwa nyenzo madhubuti ya kudhibiti kwa ufanisi matukio ya utekaji, utesaji, ushambuliaji na mauaji ya watu yanayoelekea kuota mizizi nchini.

 

Sisi JAMHURI tunaamini kuwa kamati hiyo itatekeleza majukumu yake hayo kwa uzito unaostahili, si tu kwa kufuatilia ili kuhakikisha maadui wote waliohusika katika tukio la Kibanda wanaangukiwa na rungu la dola, lakini pia inawaondolea Watanzania hofu ya kuvamiwa, kuumizwa na kuuawa wakati wowote.


By Jamhuri