Matamko ya hivi karibuni ya viongozi wa dini kwa upande mmoja; na wanasiasa na Serikali kwa upande mwingine, yameibua fikra, ishara na tafsiri tofauti kwenye jamii.

Viongozi wa dini wametoa matamko yenye ishara ya kutoridhishwa na mfululizo wa matukio nchini, yakihusu misingi ya haki za binadamu, demokrasia na utu.

Sehemu ya madai yanayohusiana na ‘maeneo’ hayo yaliwahi kutolewa na watu tofauti wakiwamo wanasiasa na wanaharakati wanaotekeleza wajibu wao kupitia asasi za kiraia.

Serikali kwa upande wake, imekuwa nyepesi kutoa majibu ya hoja zinazoibuliwa, na zaidi zinapodhihirika kuikosoa.

Si nia yetu kuingia ndani zaidi kwa kudadavua kila eneo lililoguswa na viongozi wa dini, wanasiasa, wanaharakati au Serikali kupitia wasemaji wake.

Jambo la msingi tunaloliona ni ukweli kwamba taifa linaposhuhudia kukithiri kwa hoja kinzani zinazotolewa na asasi zenye kuungwa mkono na watu wengi katika nchi, ni ishara kwamba kuna mahali ‘mambo hayaendi vizuri’.

Ndio hali tunayoiona nchini hivi sasa. Wakitumia uhuru uliopo katika kujieleza, watu wa kada tofauti wameelezea hisia, matamanio na fikra zao wakiwakosoa ama kuwapongeza watawala.

Hali inapoanza kuwa hivyo, uzoefu wa ndani na nje ya nchi unadhihirisha kwamba kunahitajika mjadala wenye lengo la kuwaleta watu pamoja ili washiriki katika ujenzi wa nchi.

Taifa linalokabiliwa na tofauti kama tulizozianisha hapo juu, kisha ‘likafumba macho’ na kuacha mambo yaendelee pasipo kuchukua hatua zinazotoa majawabu zaidi kwa hoja za pande zote, mgawanyiko utaendelea.

Kushughulikia mapema tofauti zinazoibuka kwenye nchi ni sawa na kitendo cha kuziba ufa wa nyumba, ili kuepuka hasara inayoweza kupatikana ikiwa utaachwa na hatimaye ukuta mzima ukabomoka.

Tunaamini kwamba kwa hali ilivyo sasa, Tanzania haijafikia hatua ya tofauti zilizopo kuibua hofu inayoweza kuhatarisha mifumo ya kiuchumi, kisiasa na kijamii.

Ingawa ukweli unabaki kuwa hivyo, hali hiyo inapaswa kudhibitiwa kwa mazungumzo ili isiendelee kukua, iwe kama ufa ulioachwa, ukasababisha ukuta kubomoka.

Tunaamini kwamba zipo njia na hatua tofauti zinazochukuliwa na mamlaka husika kukabiliana na mkanganyiko unaojitokeza sasa, lakini kati ya hizo inafaa kuwapo mjadala utakaowaleta watu pamoja, wakajadili pamoja na kupata suluhu ya pamoja kwa masuala yanayoihusu Tanzania iliyo chimbuko la amani na utulivu.

Matumizi ya nguvu au vitisho kama tunavyosikia mara kadhaa kutoka kwa viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama na hata wanasiasa hayawezi kuleta suluhu. Umoja na mshikamano wa Watanzania ni tunu. Tuilinde. Kamwe tusikubali kugawanyika.

964 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!