DAR ES SALAAM

Na Mwalimu Paulo Mapunda

Mwishoni mwa mwaka 2021, katika mitandao ya kijamii kulisambazwa picha zikionyesha matukio kadhaa ya watu kuuawa hasa kutokana na visa vya mapenzi. 

Kulikuwa na picha za watoto watatu walionyongwa hadi kufa na mama yao mzazi kisa eti baba wa watoto husika kula chakula mara nyingi zaidi kwa mke mwingine kuliko kwa mama huyo, ambaye pia ni mke wa baba wa watoto walionyongwa. 

Kwa hiyo mama wa watoto hao alipata hasira na kutenda jambo hilo, Mungu aingilie kati. 

Katika mfululizo huo, zilirushwa picha za mwalimu mmoja huko mkoani Singida aliyeuawa na mkewe kwa kumwagiwa mafuta na baadaye kuchomwa moto, moto ambao ulimuathiri pia mhusika na watoto,  japo wao hawajafa. 

Hapo kabla viliripotiwa vifo vya watoto wanne wa familia moja huko Bashnet, Babati mkoani Manyara ambao waliuawa na mama yao kwa kupewa sumu iliyowekwa kwenye embe, sababu ikitajwa kuwa ni mume wa mama huyo kuoa mke mwingine.

Huko Kanda ya Ziwa hususan mikoa ya Mara, Shinyanga, Mwanza na Simiyu, matukio yanayonasibishwa na visa vya kimapenzi yamekuwa yakiripotiwa kila uchao na vyombo mbalimbali vya habari. 

Hapo zamani lilikuwa ni jambo la kawaida kusikia habari za kujiua hasa kwa kujinyonga kule mkoani Iringa (Njombe ikiwamo), hasa kutokana na sababu za kihistoria zinazofungamanishwa na ushujaa. Hilo linasababu kwa kile  alichokifanya Mtwa Mkwavinyika (Mkwawa) akikwepa fedheha ya kukamatwa mateka na wakoloni wa Kijerumani, hiyo ilikuwa ni katika robo ya mwisho ya karne ya kumi na tisa.

Mbali ya Wahehe, habari hizi mbaya tulikuwa tukizisikia kwa uchache kwa vijana walioanza kupevuka, hasa inapotokea wamekorofishana au wameachana kutokana na sintofahamu katika mapenzi yao, uamuzi ulikuwa ni ama kunywa vidonge au sumu ili kujiua, hali hii kwa kiasi kikubwa ilitokana na uchanga au ulimbukeni wa mapenzi au kudhani kuwa anamkomoa yule aliyemuacha.

Katika nyakati hizi, habari ni tofauti, wanandoa waliosimama kwa utashi wao bila kushinikizwa na mtu, mbele ya padri, mchungaji au sheikh au bomani na kuuthibitishia umma pasipo shaka yoyote kwamba wanapendana kutoka ndani ya mioyo yao na kwamba wako tayari kuishi kama mke na mume katika nyumba moja, kitanda kimoja na kujifunika shuka moja, ghafla wanageuka na kuwa maadui wakubwa, na kama hiyo haitoshi wanaishia kuuana na pengine kuua hadi watoto waliowazaa wao wenyewe. Wanaua viumbe visivyo na hatia (wanaasisi halikadhalika wanashiriki kuuondoa uhai kwa kuwaangamiza wale waliowazaa na kuwaleta duniani).

Kadiri siku zinavyoyoyoma, hofu ya Mungu, akili, maarifa na utashi alivyoumbwa navyo na kuwekewa mtu ndani yake vinayeyuka kama barafu juani, binadamu anaelekea kufanana kwa hali zote na hayawani wa mwituni. Kama fisi anaua mtu, na mtu naye anaua mtu, tofauti kati ya mtu na fisi iko wapi? Au mtu ni fisi aliyestaarabika,  hivyo kuvaa nguo ili kuficha nyeti zake zisionekane? 

Nini hasa kinasababisha mapenzi moto moto ya awali yabadilike na kuwa uadui mkubwa hadi kusababisha vifo kwa wahusika na wasiohusika (watoto)? 

Kutoelewana kwa wapenzi kwanini kuhitimishwe kwa kutoana roho? Ujiue, uue au uue watoto, shetani wa aina hii ametokea wapi? Chuki nzito ya aina hii chanzo chake ni nini hasa ambacho hakiwezi kutatulika?

Mungu mwenyewe ameruhusu majadiliano, msamaha wa dhambi zako unategemea kwa kiwango kikubwa uwezo ulionao wa kupeleka hoja zenye nguvu mbele za Mungu. 

“Njoo tusemezane asema Bwana wa Majeshi, dhambi zako zijapokuwa nyekundu kama damu, upo uwezekano zikasafishika na kuwa nyeupe kama theluji.” 

Chuki yenu ninyi wapenzi wa hapo kabla ni ipi hasa, ambayo suluhisho pekee ni ama mmoja au ninyi nyote mfe, ndipo amani ipatikane? Tangu lini upatanisho ukatafutwa kati ya aliye hai na mfu au kati ya wafu?

Upatanisho hutafutwa kati ya watu wawili au zaidi walio hai, hakuna upatanisho kwa wafu. Hata Adamu na Hawa, walipoiharifu amri, Mungu hakuwaua (japo kiroho walikufa), bali aliua mnyama, na ile damu ya mnyama isiyo na hatia ikatumika kutengeneza upatanisho (uhai mpya). 

Tukio kama hilo laweza kufanywa hata na wanandoa wanaosigana ndani ya nyumba, kwamba pale chuki inapokuwa nzito ndani ya mioyo yao basi watafute jogoo, bata, njiwa, mbuzi au ng’ombe (kulingana na kipato chao) wamtoe kafara, damu itakayomwagika itatengeneza upatanisho na kuwa mbadala wa damu ya wapenzi wanaohasimiana. 

Wasipotenda jambo hilo, ardhi itafunua kinywa chake na kunywa damu zao, kwakuwa chuki ni roho yenye mashabihiano na ukaribu na roho ya mauti. 

Chuki inapopevuka huiweka kazini roho ya mauti ambayo nayo hutenda kazi kwa kuwasukumia wahusika kwenye mauti. 

Rejea visa vifutavyo katika Msahafu wa Kikristo kuhusiana na roho ya chuki; Kisa cha Kaini na Habili (watoto wa baba na mama mmoja); Chuki ya Esau kwa Yakobo (watoto wa baba na mama mmoja); Chuki ya wana wa Yakobo kwa ndugu yao Yusufu; Lakini kisa cha wazi zaidi kihusianacho na mapenzi na kifo ni kile kinachomhusisha Mfalme Daudi na jemedari wake Uria Mhiti na Betsheba bila kusahau kisa maarufu sana cha Samsoni na Delila, orodha ni ndefu ila itoshe kusema kwamba kuna uhusiano mkubwa kati ya mapenzi, chuki na roho ya mauti.

Jiulize swali, ni timamu gani atayekorofishana na mpenzi wake kisha aue watoto au mpenzi wake au kujiua yeye mwenyewe au kutenda yote matatu? 

Kuna nguvu (kani) isiyoonekana inayowasukuma watu kutenda hayo wayatendayo pasipo kujua walitendalo. Ziko sababu kadhaa za kimaumbile (physical reasons) zinazotajwa kama chanzo cha ongezeko la vifo vitokanavyo na visa au wivu wa kimapenzi. Lakini ni vema ikafahamika kwamba sababu za nje (zionekanazo) ni matokeo ya sababu za ndani (zisizoonekana -spiritual causes). 

Yote tuyatendayo nje ni matokeo ya kile kilicho ndani yetu kisichoonekana kwa macho ya damu na nyama, na ni kwa sababu hiyo maendeleo ya kweli huletwa na badiliko la nafsi. Safisha kikombe ndani ili na nje kipate kuwa safi. Sababu ya msingi ya haya yote yatokayo katika nyakati zetu ni ya kiroho zaidi kuliko mwili. Hali hii Mtume Paulo alipata kuisema katika Rumi 1:18-26.

Kunapochafuka ndani nje kamwe hakuwezi kuwa safi, kwa sababu msingi wa nje uko ndani. Kwa hiyo msingi ukiharibika hakuna namna kuta na paa vitabaki salama. 

Kuna uvunjifu mkubwa sana wa maadili leo hii duniani kote kwa kuwa shetani amejiinua na wanadamu wamempa nafasi ya kutawala maisha yao (mawazo na fikra zao). 

Upungufu wa kinga ya mwili (ukimwi) ni matokeo ya upungufu wa kinga ya roho (UKIRO), tatizo kubwa linalotukabili kama watu ni kupaka rangi makaburi (kusafisha nje) ilhali ndani yamehifadhi mizoga (ndani kumeoza).

 paulomapunda78@gmail.com

 0755 671 071

256 Total Views 4 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!