DAR ES SALAAM

Na Mwandishi Wetu 

Wiki iliyopita Yanga walimalizana na Mganda Klalid Aucho. Aucho ni kiungo wa ulinzi anayefanya sana kazi kiwanjani. Hapa Yanga wamepata mtu wa shoka. Binafsi ni shabiki wa Aucho. Tena ni shabiki wake mkubwa.

Tangu nilivyoanza kumuona miaka kadhaa iliyopita katika michuano ya Kombe la Kagame, akikipiga na Gor Mahia katika ardhi ya Tanzania, Aucho ni mchezaji ninayemhusudu. 

Ndani ya kiwanja, Aucho ni MNYAMA. Ni mshindani halisi. 

Inawezekana usajili wake Yanga usiwe na kelele nyingi wala mbwembwe kama walivyosajiliwa mastaa wengine, lakini ninaamini huu utakuwa usajili mkubwa ligi ikianza. 

Kiwanjani Aucho ana vitu vingi. Ana kimo, ana nguvu, mpambanaji, mtu mgumu, mwisho kabisa anaweza mpira. Viungo wengi wenye sifa zake wanasifika kupiga mateke, kucheza rafu, Aucho si kiungo wa hivyo. Ukimfuata hovyo hovyo anakuaibisha.

Soka letu limewahi kuwakataa mastaa wengi ambao walikotoka walifanya vema na kuimbwa, lakini hapa wakashindwa kuwika. Sitamani Aucho aingie katika kundi hili. 

Licha ya hivyo sijamuona Aucho muda kidogo. Sijui amekujaje nchini. Kama atakuwa Aucho yule wa juzi na jana atacheza Yanga asubuhi, mchana, jioni na usiku. Hakuna wa kumuweka benchi. 

Aucho aliye ‘fit’ hakuna timu atakayokosa nafasi. Si Simba, si Azam FC wala si Yanga iliyomsajili. Kila timu atacheza, tena vizuri tu. 

Lakini ninapata matumaini kila ninapokitazama kikosi cha Uganda kinapotangazwa. Iwe mechi ya kirafiki au kutafuta nafasi Aucho ni sehemu ya wachezaji wanaoitwa na wanaocheza kikosi cha kwanza mara kwa mara. Haiji kwa bahati mbaya.

Waganda wametuacha mbali kisoka. Ukiona mchezaji anakuwa tegemeo katika kikosi chao, huyo si mchezaji wa mzaha. Aucho ni mchezaji tegemeo Uganda. 

Mwisho wa yote, ninawakaribisha katika ‘show za Aucho’. Ninawakaribisha sana. Naamini kwa Aucho Yanga hawajatupa fedha zao. Wametoa fedha kwa mtu sahihi katika muda sahihi. Hii ni biashara nzuri kwa Yanga na biashara nzuri kwa Aucho, kila mmoja amenufaika. 

593 Total Views 4 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!