*Dk. Nangale ‘achukua’ mitambo ya redio

Redio ya Sibuka imeingia katika kashfa nzito baada ya kubainika kuwa mitambo inayotumia redio hiyo kurusha mawimbi ya sauti ni mali Chama cha Msalaba Mwekundu (TCRS).

Uchunguzi ulifanywa na JAMHURI  kwa miezi sita sasa na kuthibitishwa na Mkurugenzi wa Redio hiyo, Dk. George Nangale umebaini kuwa mitambo hiyo ilitolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kwa ajili kutoa taarifa za maafa kwa watu wa Wilaya ya Rufiji.


“Ni kweli vifaa hivi vimekaa kwa muda mrefu sana pale Msalaba Mwekundu na madhumuni yake ni kama ulivyosema lakini naomba kwanza nikurekebishe kuwa usiseme nimechukua mimi kama George bali ni Redio Sibuka mimi ni Mkurugenzi wake.


“Sasa baada ya kuona vifaa hivyo vimekaa kwa muda mrefu Sibuka iliamua kujitolea na kuingia mkataba kati ya  TMA, Msalaba Mwekundu wakatukabidhi mitambo hiyo. Ndio maana unasikia Sibuka ikitangaza katika Mikoa ya Pwani. Moja ya kazi hiyo ni kutangaza maafa. Bila hivyo mitambo hiyo ingerudishwa ilikotoka.


“Lakini ndugu yangu haya yote yanakuja kwa ajali ya uchaguzi. Kuna watu wanataka kutuvuruga tu, Bw. Edmund chama kimetulia sisi tunataka kujitolea wanatuvuruga tu. Njoo siku ya Jumatatu tuongee vizuri,” amesema Dk. Nangale.


Mmoja ya wanachama amelimbia JAMHURI kuwa mitambo hiyo ilitakiwa kufungwa Wilaya ya Rufiji mwaka 2009. Mazungumzo ya kufunga mitambo yalifanyika ofisini kwa Mkuu wa Wilaya wakati huo akiwa Kasimu Majaliwa ambaye kwa sasa ni Naibu Waziri wa Elimu Mafunzo ya Ufundi.


Hata hivyo, JAMHURI haikufanikiwa kumpata Waziri Majaliwa kuzungumzia suala hilo baada ya kujaribu mbinu nyingi ikiwamo kwenda ofisini kwake.


“TMA walitoa mitambo hiyo kwa ajili ya kutoa taarifa za maafa katika Wilaya ya Rufiji kwa kuwa maeneo hayo hutokea maafa kila wakati, lakini kwa bahati mbaya au nzuri kwao nasikia kuna mtu anayo cha msingi muulize Mkurugenzi wa Maafa, Dk. Kejo (Julius) ndio anajua kinachoendelea kuhusu hiyo kitu,” amesema.


Katika mazungumzo na JAMHURI, Mkurugenzi wa Maafa wa TCRS, Dk. Julius Kejo amesema hajui lolote kuhusu mitambo hiyo, hivyo amemtaka mwandishi wa habari hizi kuwauliza TMA.

JAMHURI ilivyozungumza na mmoja wa wafanyakazi alikiri mitambo hiyo kuwa mali ya chama.


Hali ndani ya chama

Katika hatua nyingine hali ndani ya chama hicho imechafuka kutokana na wanachama na wenyeviti wa chama hicho kutoka mikoa minne ya Tanzania kutishia kupinga uchaguzi mkuu mahakamani.


Uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Mwanza Januari 28 hadi 29, mwaka huu kumchagua Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho.


Hatua hiyo imekuja baada ya bodi ya chama hicho kutuhumiwa na baadhi ya wanachama kuwa inaendesha mambo kibabe ndani ya chama hicho bila kufuata Katiba na kanuni za uchaguzi.


Mambo yanayolalamikiwa na viongozi na wanachama wa chama hicho ni ukiukwaji wa Katiba, matumizi mabaya ya ofisi na wanachama wa chama hicho kunyimwa haki ya kushiriki katika ujenzi wa chama.


JAMHURI imebaini kuwa mwanya wa upungufu katika Katiba kwa kuwaruhusu viongozi kufanya watakalo bila kuwashirikisha wanachama ambao wapo kwa mujibu wa Katiba ya chama hicho ndilo chimbuko la tatizo.


Katiba ya chama hicho haitambui cheo cha Naibu Katibu Mkuu, lakini Bodi ya chama hicho imekuwa ikimtambua, Peter Mlebusi kama Naibu Katibu Mkuu.

 

Katiba ya Chama

Kifungu cha 20 kinaeleza mfumo wa Bodi ya chama hiyo ambayo itahusika na usimamizi wa jumla wa shughuli za chama. Bodi hiyo inaundwa na Mwenyekiti wa Taifa, Makamu Mwenyekiti, Katibu Mkuu ambaye atakuwa Katibu wa Bodi.


Wengine ni Mweka Hazina wa Taifa, wajumbe sita wa Bodi waliochaguliwa na Mkutano Mkuu wa Taifa na wajumbe wengine wasiozidi watatu watakaoteuliwa na Mwenyekiti wa taifa.


Pia kutakuwa na Halmashauri Kuu ya Taifa itakayoundwa na wajumbe saba, Mwenyekiti wa Taifa, Makamu wa Mwenyekiti wa Taifa, Katibu Mkuu, Mweka Hazina wajumbe sita wa taifa wenyeviti wote wa mikoa.


Wengine ni wajumbe saba waliochaguliwa na Mkutano Mkuu  wa Taifa na wajumbe wasiozidi watatu walioteuliwa na Mwenyekiti wa Taifa kwa kuzingatia uwiano wa jinsia.


Halmashauri Kuu itakuwa na madaraka yafuatayo: Kuthibitisha ajira na kumuondoa madarakani Katibu Mkuu kwa mujibu wa sheria, kuweka kanuni na taratibu kama itakavyokuwa ni lazima na inafaa.


Mdaraka mengine ni kuchuja majina ya wagombea wote wanaowania nafasi za kuchaguliwa kwenye chama ngazi ya taifa, kubuni sera na kusimamia maadili ndani ya chama, kumfukuza kiongozi au mjumbe yeyote atakayethibitika kuwa na makosa kinyume na taratibu.


JAMHURI imebaini kuwa katika kinyanganyiro cha uchaguzi wa mwaka huu, bodi haikufuata Katiba ya chama hicho. Bodi ilipoka madaraka ya Halmashauri Kuu na kuchuja majina ya wagombea wa ngazi ya taifa na mkoa ambapo ilitakiwa kuchuja majina ya wagombea wa mikoa pekee kama iliyoinishwa katika Katiba.


Pia Bodi hiyo imevunja kanuni za uchaguzi ya mwaka 2011 kwa kumpitisha, Dk. Zainab Gama, ambaye kwa sasa ni makamu mwenyekiti kwa kipindi cha miaka kumi,  kikatiba anatakiwa kuondoka madarakani.


Hata hivyo bodi hiyo kwa kuangalia maslahi ya wajumbe wake wanaotuhumiwa kutafuna fedha na mali ya chama  wametengeneza utaratibu mwingine ili agombee tena katika kipindi kijacho.


Pamoja na kuwa kikatiba kutokitambua cheo cha Naibu Katibu Mlebusi amekuwa akiratibu vikao vya bodi, ilihali sio Katibu Mkuu wa chama ambaye kikatiba ndiye Katibu wa Bodi.


Tangu mwaka 2006 hakuna kikao chochote kilichofanyika kwa Msalaba Mwekundu, iwe cha Bodi au Mkutano Mkuu kinachopaswa kufanyika kila baada ya miaka miwili kwa mujibu wa Katiba.


Hatua hiyo imesababisha Bodi kutokuwa na ushindani wa ndani kwa kuwa wametengeneza kanuni za uchaguzi kinyume na Katiba wakachuja majina ya wagombea wenzao na kuengua wapinzani wao.

Kutokana na hali hiyo hakuna mjumbe anayeweza kuhoji jambo lolote ndani ya Bodi hiyo kutokana na kuwa wamepewa cheo kwa hisani.


Mkurugenzi wa Fedha na Utawala, Ali Rajabu amekiri kuwa chama hicho hakijafanya ukaguzi wa hesabu kwa kipindi cha miaka 10 isipokuwa miradi inayosimamiwa na wahisani. Rajabu ameliambia JAMHURI kuwa chama hicho hakijafanya ukaguzi tangu mwaka 2004.


Sheria ya TRCS haisemi kuwa lazima wa ukaguzi hesabu hizo upelekwe Wizara ya Afya au Ulinzi kwa kuwa haijulikani kama wako chini ya wizara ipi kati ya hizo.


Lakini sheria ya vyama vya kiraia Namba 337 ya 2002 inavitaka kuwasilisha taarifa za ukaguzi Wizara ya Mambo ya Ndani kila mwaka.


Pia sheria ya mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) Na 24 ya 2002 inasema vyama hivyo vipo chini ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Mama na Watoto.


Kwa utaratibu uliopo sheria zilizotajwa zinawataka kutoa taarifa kila mwaka, na wasipofanya hivyo msajili anatakiwa kuvifuta vyama visivyotoa taarifa za fedha.


TRCS si NGO wala chama cha Kiraia, ni shirika la kutoa huduma za kibinadamu lililoanzishwa kwa sheria ya Bunge mwaka 1962 na linalindwa na Makubaliano ya Geneva ya 1949.


Mkubaliano hayo yaliidhinishwa na Bunge, lakini pamoja na uhuru walio nao kwa kulingana na sheria lazima wote wachapishe hesabu zao na kuzikabidhi serikalini na kwa wanachama wao kujua kinachoendelea kila mwaka.


Akizungumza na JAMHURI kuhusu ripoti ya ukaguzi wa hesabu za chama hicho, Dk. Nangale amesema ukaguzi wa hesabu ulikwama kutokana na chama kukosa fedha.


Dk. Nangale amesema sasa wamepata fedha na kazi ya ukaguzi imeanza watatoa majibu ya ukaguzi huo muda si mrefu na watawasilisha kwenye Bodi.


Wanachama TCRS walalamika

Wanachama waliozungumza na JAMHURI mwishoni mwa wiki kwa nyakati tofauti wamesema chama hicho kimeoza na hakina mwelekeo kutokana na ufisadi unafanyika ndani ya chama hicho. Mmoja wa wanachama amesema kati ya ufisadi unawakera ni uwekezaji wa jengo la chama hicho linalojukilaka kama Viva Towers lilipo Upanga.


Jengo hilo la kibishara na makazi ya watu linajengwa na Kampuni ya Ujenzi ya Estim Construction kwa ubia na Chama cha Msalaba Mwekundu na Virgin Plaza.


Amsema hadi sasa wanachama hawajui jinsi gani TCRS imeingia mkataba huo na kwa muda gani.

Mwanachama mwingine amesema jengo lililopo mtaa wa Kisutu, Dar es Salaam, nalo limepangishwa bila ya wanachama wa chama hicho kujua nini kinaendelea hadi sasa.


“Jengo hilo ni la Red Cross mkoa lakini walimsainisha mama Mayasa Bashehe ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Mkoa [wa Dar es Salaam] kwa kumwahidi kuwa Red Cross mkoa watapewa ghorofa mbili, lakini kumbe ilikuwa ni danganya toto. Hadi leo Mayasa ametoka katika kiti chake hawajapata fedha hizo [wala ghorofa mbili],” alisema.


Mayasa alionekana kubabaika kutoa majibu kuhusu kuufahamu mkataba baada ya kupokea simu na kumwomba mwandishi kumpigie baadaye.


Baada ya kupigiwa mara ya pili amesema hafahamu lolote kuhusu mkataba huo na hivyo waulizwe wahusika waliopo ofisini ndio wataeleza ukweli wa jambo hilo.


“Baba mie siku hizi nipo nyumbani. Niliacha Red Cross na sasa niko Lindi nauguza mama yangu. Kwa habari hiyo unazidi kunichanganya zaidi. Hayo mambo baba waulize ofisi ya mkoa wako hapo ofisini,” amesema Mayasa.


Katibu wa chama hicho Mkoa wa Dar es Salaam, Grace Mawalla alipozungumza na JAMHURI amesema hajawahi kuona mkataba huo tangu ashike cheo hicho.


“Mie ninachojua ni Jengo la Makao Mkuu na sijui vinginevyo,” amesema Mawalla.


By Jamhuri