Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) inakabiliwa na kashfa nzito inayohatarisha usalama wa nchi kutokana na uamuzi mbovu walioufanya hivi karibuni; uchunguzi wa JAMHURI umebaini.

Kashfa hii imetokana na masilahi binafsi, kiburi cha viongozi, kupuuza wataalamu, weledi mdogo wa baadhi ya watendaji ambao sasa unaelekea kusimamisha mfumo mzima wa vitambulisho na kuliingizia taifa hasara kubwa.

Mkurugenzi Mkuu wa NIDA, Dk. Arnold Kihaule, anatajwa kufanya uamuzi wa kushangaza kwa kuamua kununua mashine mpya mbili za kuchapa vitambulisho kutoka Ujerumani, lakini kutokana na kupuuza ushauri wa wataalamu, mashine hizo walizozinunua kwa Euro 3,304,650 (karibu Sh bilioni 8), pamoja na kuwa na uwezo mkubwa wa kila moja kuchapa vitambulisho 9,000 kwa saa; haziwezi kufanya kazi kwa sasa. 

Mkataba wa kununua mitambo hii miwili ulisainiwa Julai 22, mwaka jana. Mkataba huu umesajiliwa kwa No. EA/061/2018-2019/HQ/G/01-LOT 3 ukiwa na thamani ya kiasi hicho cha fedha.

“Mkurugenzi Mkuu wa NIDA [Dk. Kihaule] aligoma kusikiliza ushauri wa wataalamu, matokeo yake sasa tumegota. Taarifa hii [JAMHURI linaonyeshwa taarifa ya kutisha] wameiandaa pale NIDA, lakini wanatumia hadi mablanketi kuhakikisha Rais [John] Magufuli haimfikii. Mashine zimefungwa tangu Novemba, 2019, lakini zimeshindikana kufanya kazi. 

“Mkurugenzi Mkuu wataalamu walimwambia kuwa kama tunanunua hizi mashine tunapaswa kununua na vifaa vyake, akakataa akasema zinunuliwe mashine vifaa vingine vitatumika hivi vinavyotumika katika mashine za zamani,” kimesema chanzo chetu cha habari. 

Mashine hizo mbili zenye uwezo wa kuchapa vitambulisho 9,000 kwa saa moja, baada ya kufungwa Novemba, mwaka jana, imebainika kuwa zinahitaji vifaa vitatu ili ziweze kufanya kazi. Gharama ya vifaa hivyo kwa ujumla ni zaidi ya Sh milioni 600. 

Vifaa vinavyohitajika ni: 1. HSM ambacho kina nywila za kuendeshea mashine hizo. 2. Compressor za kuendeshea mitambo hiyo; na 3. Servers kwa ajili ya kuhifadhi kumbukumbu za taarifa za Watanzania na wageni watakaotengenezewa vitambulisho.

“Mashine hizi haziwezi kufanya kazi bila vitu hivyo vitatu. Mbaya zaidi, hata baada ya kubaini makosa haya, wataalamu wanasema compressor inunuliwe ya umeme, mkurugenzi anasema kuna watu anawafahamu wanauza compressor za dizeli kwa bei rahisi. Hili ni janga,” ameongeza mtoa taarifa wetu. 
Wataalamu kutoka Kampuni ya Atlantic Zeiser GmbH ya Ujerumani iliyotengeneza na kuuza mashine hizo walifika nchini wakijua kila kitu kipo, wakafunga mashine hizo mbili na walipouliza kuhusu hivyo vifaa vitatu wakaonyeshwa mashine tatu za zamani zilizokuwa zinatumika kuchapisha vitambulisho vya taifa, ndipo wakasema mitambo hiyo haiingiliani. Wakaondoka kwa maelezo kuwa vikipatikana waitwe wamalizie kazi.

Ukifuatwa mchakato wa ununuzi kwa mujibu wa Sheria ya Manunuzi ya Umma ya Mwaka 2004 kama ilivyorekebishwa mara kadhaa, mchakato wa kupata vifaa hivyo vitatu ambao hadi tunaandika habari hii haujaanza, utachukua siku 189, yaani miezi sita kuanzia sasa. 

Hadi sasa NIDA wamesajili Watanzania milioni 21, na waliopata vitambulisho ni milioni 5.9 pekee; hivyo watu milioni 15.1 wanasubiri kupewa vitambulisho. Kwa idadi hii, ikiwa hizi mashine zitafanya kazi vizuri kwa saa 12 kila siku bila kupumzika, zinaweza kuchapisha wastani wa vitambulisho 200,000 kwa siku moja, hivyo kuchapa vitambulisho milioni 15.1 kwa siku 75; sawa na miezi miwili na nusu. 

Fedha hizi ‘zilizoteketezwa’ kwa kununua mashine ambazo kama zitafanya kazi itakuwa ni miezi 9 kuanzia sasa zilitolewa na Rais John Mafuguli mwaka 2016. Akawataka NIDA wahakikishe wanatengeneza vitambulisho kuwezesha wananchi kutambuliwa; suala ambalo si tu linaimarisha usalama wa nchi, bali pia kwa Watanzania kutambulika, inapunguza riba za benki, inaipa serikali uhakika wa kukusanya kodi na manufaa mengine mengi. 

Aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa NIDA, ambaye baadaye alihamishwa na kupewa nafasi nyingine nyeti, Dk. Modestus Kipilimba, aliondoka NIDA akiwa ameshauri vizuri kabla ya kuhamishwa kuwa uamuzi wowote wa kubadili mzabuni anayetengeneza vitambulisho vya sasa unapaswa kuwa suala la mwisho kufanywa, kwani likifanyika kuna hasara kubwa na mambo mengi yatajitokeza. Ushauri huo wa Dk. Kipilimba haukusikilizwa na tayari hasara zimeanza kuingia. 

Hasara ya kwanza na ya wazi inayotokea ni kwamba hadi sasa NIDA ina akiba ya kadi za vitambulisho milioni 4.7 kwenye ghala. Baada ya wataalamu kufunga mitambo hii, walionyeshwa kadi zilizopo wakasema mitambo hii haitumii kadi hizo – badala yake inatumia aina nyingine.

Kadi hizi zimenunuliwa kati ya dola 2 na dola 2.5 (wastani wa Sh 5,000) kwa kila kadi moja. Hii ina maana kuwa kadi milioni 4.7 zilizopo kwa kuwa hazitatumika kwenye mashine hizi mpya itabidi zitupwe. Ukizidisha kadi hizo kwa Sh 5,000 serikali itakuwa imepata hasara ya Sh bilioni 23.5.

Hasara si hiyo pekee. Sasa umeibuka mgogoro mpya. Programu ya kompyuta (software) iliyokuwa inatumiwa na Kampuni ya IRIS Corporation Berhad ya Malaysia kutengeneza vitambulisho vya sasa, nayo inapaswa kubadilika. Ikitumika gharama ya kutengeneza vitambulisho itakwenda juu maradufu, maana kampuni mpya itapaswa kulipia gharama za hakimiliki za kutumia mfumo huo uliojengwa na Kampuni ya IRIS.

Hata mfumo huo ukiachwa ukaletwa mfumo mpya, itabidi hata watu milioni 5.9 waliokwisha kutengenezewa vitambulisho vya taifa nao wabadilishiwe, kwani utakuwa mgogoro mkubwa kuwa na vitambulisho vyenye mifumo miwili katika nchi moja. 

Mjadala mzito unaendelea na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene, amewaita vigogo wa NIDA ofisini kwake waeleze kuhusu ‘mkoroganyo’ wote huo na kwanini wameliingiza taifa katika mgogoro huo. 

Ikumbukwe suala la vitambulisho vya taifa lilizungumzwa tangu miaka ya mwanzo ya Uhuru na mchakato ulianza rasmi mwaka 2008. Kitambulisho cha kwanza kilitolewa Februari 8, 2013. Kabla ya hapo, kuanzia mwaka 2002 ulikuwapo mgogoro mkubwa wa aina ya software ya kutumika; na kampuni ipewe zabuni. Mvutano huo ulichelewesha mchakato na sasa Mkurugenzi wa NIDA amerejesha mkanganyiko huo.

Mashine za zamani

Kampuni ya IRIS Corporation Berhad ya nchini Malaysia iliyoanza kutengeneza vitambulisho mwaka 2012 ilifunga mashine tatu za kuchapa vitambulisho. Ufanisi wa mashine hizo ulikuwa ni kila mashine moja kuzalisha vitambulisho 5,000 kwa sasa. 

Hata hivyo, mashine hizi hazikufanyiwa matengenezo (service) na zimepungua uwezo wa kuzalisha kutoka vitambulisho 5,000 kwa saa na kuwa vitambulisho 500 kwa siku. 

Uchunguzi wa JAMHURI umebaini kuwa haikuwa kusahau au kutofahamu umuhimu wa kuzifanyia matengenezo mashine hizi, bali wapo watu ‘waliopiga pasi ndefu’ wakijua kuwa ufanisi wa mashine hizi ukishuka, mzabuni hataongezewa muda wa kufanya kazi ya kuchapa vitambulisho; jambo ambalo limetokea kweli. 

Tangu Machi 14, 2018 mkataba wa mkandarasi huyu ulipokwisha, NIDA inafahamu kwanini iligoma kumwongezea mkataba angalau wa miezi 10 alioomba na kukarabati mashine hizo. Mashine moja imesimama kabisa kufanya kazi; na hizo mbili zilizosalia zina uwezo wa kuzalisha vitambulisho 1,000 kwa siku.

Kwa idadi ya vitambulisho vinavyotakiwa kwa sasa ikiwa zitaendelea kutumika mashine hizi za zamani, ambapo imeelezwa kuwa moja ndiyo inafanya kazi kwa ufanisi kwa kuchapisha vitambulisho 500 kwa siku, basi vitambulisho hivi milioni 15.1 italichukua taifa miaka 82 kuvichapisha. Hii ni nje ya waombaji wapya na kwa mujibu wa taarifa ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu ya mwaka 2019, Watanzania milioni 27 walistahili kupatiwa vitambulisho na idadi inaongezeka.

IRIS ambaye ndiye mkandarasi anayetengeneza vitambulisho kwa sasa, ilifika hatua kutokana na deni kuwa kubwa akasitisha kutengeneza vitambulisho mwaka jana. Alikuwa anadai dola milioni 30.18 za Marekani (Sh bilioni 69.98). JAMHURI lina uhakika kuwa tayari ameshalipwa Sh bilioni 53.

Faida za kitambulisho cha sasa

Kitambulisho cha taifa cha sasa kinatumia smart card – mfumo ambao umefunikwa, au kwa Kiingereza Contactless Smartcard. Mbali na teknolojia hii kudumu kwa muda mrefu, na kadi hii kuwa imewekewa karatasi ya naironi kuepusha hata ikiloa maji isiharibike; kadi zijazo hazitakuwa na kinga hiyo. 

Kadi za sasa zinatumika kama kitambulisho cha Mpiga Kura, Leseni ya Udereva, Kadi ya ATM, TIN Number, Kadi ya NHIF, inaweza kuhifadhi fedha (E Wallet), inaweza kutumika kulipa kaya maskini kupitia TASAF na shughuli nyingine nyingi.

Kutokana na uzembe, hadi sasa NIDA imepata hasara ya Sh bilioni 18.5 ilizopaswa kulipwa na kampuni za simu. “Kanuni inasema kila laini ya simu ikitumia d6ata kutoka NIDA kwa kusajiliwa inapaswa kulipa Sh 500. Kanuni za mwaka 2014 ziko wazi. Kampuni za simu ziko tayari kulipa, ila Dk. Kihaule hajafanya lolote kuingia mikataba na kampuni hizo ili kupata fedha hizo.

Hili la kutumia ‘data’ watu wakalipia, tayari linafanya kazi hapa nchini. Wakimbizi kila mmoja anapaswa kulipa dola 20 za Marekani (ingawa hadi leo hakuna aliyelipa), wafanyakazi wanaoingia nchini kufanya kazi miezi sita au zaidi wanapaswa kulipa dola 50 za Marekani na wamekuwa wakilia. Wawekezaji wanapaswa kulipa dola 100 za Marekani.

“Hizi ndizo zilizalisha gawio la Sh bilioni 2. Rais anahangaika kutafuta fedha, watu wenye uwezo wa kupata fedha wamelala, hawazichukui, nchi inakosa hela,” kimesema chanzo chetu. 

Mtoa habari mwingine, amesema yeye anaifahamu mitambo iliyopo NIDA. “Ile mitambo inaweza kuwa serviced kwa gharama ndogo, ikachapa vitambulisho angalau 12,000 kwa sasa kwa ujumla wake. Tunaiingiza nchi katika hasara pasipo ulazima… Mkurugenzi Mkuu wa NIDA anapaswa kuwaheshimu wataalamu… sasa hata hiyo compressor isiwe ya dizeli, iwe ya umeme. Yeye anatafuta ya dizeli,” amesema mmoja wa wataalamu. 

Kampuni iliyoleta mashine hizo mpya mbili, licha ya kuwaambia kuwa kadi zilizopo haziingiliani na mashine zao, hawajaeleza wakileta za kwao zitauzwa bei gani. Wakizungumza na JAMHURI kwa nyakati tofauti, wataalamu wameomba Rais Magufuli aingilie kati sakata hili kwani kuna hatari ya kuua mfumo mzima wa vitambulisho vya taifa nchini.

“Nafahamu Waziri Simbachawene amewaita, lakini akicheka nao tumekwisha. Tayari nchi imekwishafungwa bao moja la mitambo, sasa tunakwenda katika mchakato wa mfumo wa kompyuta -ni gharama mpya ambayo hatukustahili kuiingia. Mitambo yenyewe haijakamilika vifaa, kuna hatari mfumo mzima ukafa. Wanapaswa kujibu wakileta mfumo mpya wa kompyuta kadi za zamani zitasomwaje au kama itatumika mifumo miwili kwa pamoja au vinginevyo. Huu ni mkanganyiko mbaya sana,” kimesema chanzo chetu.

Shilingi milioni 100 za TRCA

JAMHURI limemuuliza Dk. Kihaule taarifa kuwa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imempatia Sh milioni 100 kuiwezesha NIDA inunue servers mpya ziwahishe upatikanaji wa namba za utambulisho kwa wananchi wanaoteseka kupata usajili wa simu, lakini NIDA wanajua wamezitumiaje fedha hizo.

“Kwa kweli inakera. TCRA wemetupatia Sh milioni 100 tununue servers, lakini DG amekwenda kuomba servers ambazo ni used katika kampuni moja  ya simu za mkononi (jina tunalo). Sasa tunajiuliza, mbali na kwamba waliishazitumia wakazichoka na kuziondoa kwenye matumizi, zinapotumika kuhifadhi taarifa za Watanzania tuna uhakika gani kuwa hizo taarifa ziko salama hazijaungwa kwenye mitandao mingine ya nje ya nchi kwa matumizi wanayoyajua waliozitoa? Kwa kweli anachofanya Dk. Kihaule ni jambo la hatari. 

“Tunaomba serikali iingilie kati servers hizi za msaada ziondolewe. Nchi yetu siyo maskini hivyo. Fedha alizopewa azitumie kwa matumizi yaliyokusudiwa. Rais wetu Dk. Magufuli anapambana ila watu wanamwangusha kwa makusudi,” amesema mtoa taarifa mwingine.”

Simbachawene anena

JAMHURI lilipomtafuta Waziri wa Mambo ya Ndani, George Simbachawene, hakuwa na mengi ya kusema: “Kwa kweli mimi nina wiki mbili hapa wizarani, ila nimeyasikia hayo matatizo, nimeelezwa hatari iliyopo na nimewaita wiki ijayo (Alhamisi, wiki hii), waje kwangu na majibu ya maswali yote hayo uliyoniuliza na mengine. Ninaloweza kusema ni kuwa tunapaswa kuwa wazalendo, kuitendea nchi hii haki katika kila uamuzi tunaoufanya na hili tutalifanya.”

Mkurugenzi Mkuu Dk. Kihaule

JAMHURI limemtafuta Dk. Kihaule mara kadhaa bila mafanikio. Hata Msemaji wa NIDA, Thomas William, mara zote hakuwa akitoa jibu. Ilipofika Jumapili saa chache kabla ya kwenda mitamboni, akatuma ujumbe huu kwa JAMHURI: “Habari Ndugu Balile, tafadhali tunaomba utume maswali uliyonayo NIDA itakujibu kwa maandishi.”

William alileta ujumbe huu baada ya JAMHURI kumpelekea maswali Dk. Kihaule. Awali, William alikuwa akisema hana majibu ya moja kwa moja. Haijulikani kama William aliwasiliana na Dk. Kihaule kutoa jibu hilo, au la! 

Watendaji waliozungumza na JAMHURI kwa sharti la kutotajwa gazetini, wamesema Mkurugenzi Mkuu, Dk. Kihaule anapuuza ushauri wa wataalamu na ameigawa ofisini kwa kuendekeza majungu.

“Kwa sasa anaendeshwa na wafanyakazi wawili wanaoweza kumfikishia majungu wakati hawana utaalamu. Mwishowe tunaona NIDA inaanguka mikononi mwa Dk. Kihaule,” amesema mfanyakazi mwandamizi.

By Jamhuri