Kashfa ya nyumba NIC

Shirika la Bima la Taifa (NIC) limeingia katika kashfa ya kuhujumu mali za shirika hilo, ikiwamo ya kuuza nyumba bila kuzingatia maagizo yaliyotolewa na Serikali Oktoba, 2009.

Nyumba zilizopangishwa kwa wafanyakazi wa Shirika hilo zilizoko eneo la Kijitonyama jijini Dar es Salaam katika viwanja namba 75-78, Block 45B ziliuzwa kwa Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA), bila kuingizwa kwenye orodha ya nyumba zilizotakiwa kuuzwa kwa Wakala wa Majengo sawa na maagizo ya Kamati ya Bunge ya Fedha na Uchumi ya Oktoba 15, 2009.

Shirika la Bima la Taifa lililoanzishwa mwaka 1963 na kumilikiwa na Serikali kwa asilimia 100, limelemewa na mzigo wa madeni ambayo yamelimbikizwa kwa kipindi kirefu kutokana na uzembe wa makusudi wa viongozi wa Shirika hilo, ama nia ya kulifilisi liuzwe kwa wawekezaji binafsi.

Shirika hilo liliendelea kuwa shirika pekee katika biashara ya bima hadi mwaka 1996 Bunge liliporuhusu biashara huria ya bima nchini na kuruhusu kampuni binafsi kuleta ushindani katika soko hilo.

Kutokana na ushindani katika biashara ya bima, Mei 1998 Serikali ililiweka Shirika hilo chini ya usimamizi wa Tume ya Rais ya Kurekebisha Mashirika ya Umma (PSRC) huku mkakati wa kuliuza kwa mwekezaji binafsi ukiwa umefikia hatua za mwisho.

Hata hivyo, Novemba 2008, Serikali ilibatilisha uamuzi wake wa kuliuza Shirika hilo kwa wawekezaji binafsi na badala yake kulirekebisha kwa lengo la kuliongezea thamani kutokana na ushauri wa Kamati ya Bunge ya Fedha na Uchumi.

Kufikia Juni 30, 2009 madai ya bima za maisha na zisizo za maisha yalifikia jumla ya Sh bilioni 24.10 na hivyo Kamati ya Fedha na Uchumi katika mpango wake wa kurekebisha Shirika hilo “Kusimamia zoezi la kuuza baadhi ya mali na majengo ya Shirika yasiyokuwa msingi wa biashara ya bima ili kupata fedha za kulipa madai, kugharamia marekebisho ya Shirika pamoja na kukidhi matakwa ya Sheria ya Bima namba 18 ya mwaka 1996,” inaeleza sehemu ya maagizo ya serikali yaliyotolewa na serikali.

Katika mpango huo kikosi kazi kilichoundwa kilikamilisha kazi ya uthaminishaji wa mali zote zisizo za msingi za biashara ya bima hadi kufikia Desemba 31, 2008 zikiwa ni Sh bilioni 31.7.

Maelekezo yaliyopendekezwa ni kwamba nyumba zote za Shirika la Bima zinunuliwe na Serikali kwa bei ya soko kupitia Wakala wa Majengo wa Serikali (TBA), lakini viongozi wa Shirika hilo walishindwa kutekeleza na wakaziuza nyumba hizo holela huku zile za Kijitonyama zilizopangishwa kwa watumishi wake zikiwa hazipo katika mali zilizothaminishwa.

Viongozi wa Shirika la Bima kwa kupuuza maagizo yaliyotolewa na Serikali waliziuza nyumba hizo kwa Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) ambazo zimegeuzwa kuwa Ofisi Kuu za Baraza hilo.

Mkataba wa mauziano wa nyumba hizo kati ya Shirika la Bima na BAKITA ulisainiwa Oktoba 8, 2009 ukihusisha nyumba zenye hati namba 186217/3, 186217/4, 86217/6 na 186217/7 zilizoko katika viwanja namba 75-78, Block 45 B eneo la Kijitonyama jijini Dar es Salaam.

Shirika liliuza nyumba hizo kwa gharama ya Sh bilioni 1.5 ambazo zilitakiwa kulipwa kwa vipindi viwili huku likiendelea kuwatoza kodi ya pango ya asilimia 10 ya mshahara kwa watumishi wake waliokuwa wamepangishwa awali.

 

Aliyekuwa mfanyakazi wa Bima anena 

Rose Roezer aliajiriwa na Shirika la Bima kwa kazi ya kudumu Oktoba 1, 1980 hadi Aprili 4, 2009 walipoachishwa wote wa shirika hilo na kuajiriwa upya kwa mkataba wa miaka mitatu kuanzia Januari 1, 2010.

Roezer akiwa amelitumikia shirika hilo kwa miaka 32, anasema mwaka 2009 Serikali ilipoamua kuliunda upya Shirika la Bima na kuwaachisha watumishi wake huku baadhi yao wakiendelea na kazi, wao waliendelea kukaa kwenye nyumba hizo wakisubiri ajira.

Anasema wao wakiwa hawaelewi chochote, Shirika hilo liliuza nyumba hizo walizokuwa wamepangishwa bila kuwapa taarifa yoyote na kuwaingiza katika mgogoro usiokuwa wa lazima.

Kwa mujibu wa barua ya Shirika hilo ya Mei 28, 2002 yenye kumbukumbu namba NIC/ADM/CIR/6, Sekula Namba 370 kwenda kwa wafanyakazi wake wote kuhusu uuzaji wa nyumba na viwanja vya Shirika la Bima vilivyopo Dar es Salaam, wafanyakazi walitangaziwa zabuni ya kuuza mali hizo chini ya Tume ya Rais ya Kurekebisha Mashirika ya Umma (PSRC).

Sera ya uuzaji wa nyumba za Mashirika ya Umma, waraka namba 60 wa mwaka 2003 kifungu namba 5.1 inaeleza kwamba wafanyakazi wa mashirika na Taasisi za Umma zitakazobinafsishwa wauziwe nyumba za mashirika na taasisi hizo.

Pamoja na kukiuka taratibu za uuzaji wa nyumba hizo, Shirika la Bima lilitoa vitisho vya kuwafukuza kazi watumishi wanaoishi katika nyumba hizo kwa kuwataka wajitoe katika shauri walilokuwa wamelifungua mahakamani kuweka zuio la kuondolewa katika makazi hayo.

Mhasibu huyo alifukuzwa kazi Desemba 31, 2012 kwa kosa la kufuatilia nyumba hizo ambazo waliiomba Wizara ya Fedha na Uchumi kuwauzia.

 

Bima walivyomdanganya Waziri

Uongozi wa Shirika la Bima la Taifa licha ya kutoziorodhesha nyumba hizo katika mali zake zinazotakiwa kuuzwa kulipa madeni ya bima zilizoiva kwa muda mrefu, ulimdanganya aliyekuwa Waziri wa Fedha na Uchumi kipindi hicho, Mustafa Mkulo, kwamba nyumba hizo hazina watu.

Shirika lilitoa madai hayo wakati wanafahamu kwamba bado zinakaliwa na watumishi wake ambao walipangishwa na kuendelea kutozwa kodi ya pango ya asilimia 10 ya mshahara.

Hata hivyo, wakazi hao walimwandikia barua Waziri Oktoba 17, 2009 kutaka kuuziwa nyumba hizo baada ya kusikia matangazo ya kuuzwa nyumba hizo za Bima.

 Licha kutuma maombi yao kwa Waziri, Shirika hilo lilikwishaziuza wiki moja kabla ya tangazo la Serikali.

Mpango wa Serikali kuuza nyumba za Shirika la Bima kwa lengo la kulifufua kimtaji ulitangazwa Dar es Salaam, Oktoba 16, 2009 na aliyekuwa Naibu Waziri wa Fedha na Uchumi, Jeremiah Sumari, wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa marekebisho ya Shirika hilo mbele ya wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Fedha na Uchumi.

Katika taarifa hiyo alisema kikosi kazi cha shirika hilo kimekamilisha kazi ya uthaminishaji wa mali zote za shirika pamoja na majengo yake kwa bei ya soko ambayo ni Sh bilioni 31.7.

Alisema Serikali itafanya hivyo kupitia Wakala wa Majengo wa Serikali (TBA) na kwamba hadi mwishoni mwa mwaka 2009 itakuwa imekamilisha mchakato mzima wa malipo hayo kwa NIC.

 

TBA yafafanua 

JAMHURI imefanya mahojiano na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo (TBA), Elius Mwakalinga, na aliyethibitisha kuwa Bima hawakuwapa majengo hayo kama Serikali ilivyokuwa imeagiza.

“Ilikuwa tukabidhiwe majengo hayo pamoja na lile la Kitegauchumi lakini sielewi kulikuwa na kikwazo gani? Labda niwasiliane nao kwanza hawa waliokuwepo kipindi hicho,” anasema Mwakalinga.

JAMHURI ilipelekwa kwa ofisa mmoja wa TBA ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini kwa madai kwamba yeye si msemaji, ila anasema wao walipelekwa kuziona nyumba hizo za Kijitonyama na Masaki Dar es Salaam, lakini hawakukabidhiwa.

 

BAKITA wawashangaa Bima

Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA), Dk. Seleman Sewangi, ameieleza JAMHURI kwamba walinunua nyumba hizo kutokana na maombi yao waliyopeleka kwa Shirika la Bima.

Dk. Sewangi anasema mlango ulikuwa wazi kwa wanunuzi wa nyumba hizo zikiwamo taasisi na mashirika ya umma, lakini haelewi kama wapangaji wa nyumba hizo walituma maombi yao kuonesha nia ya kuuziwa.

Pamoja na kuweka ofisi za Serikali ndani ya makazi ya watu, inadaiwa kuwa taasisi hiyo imetumiwa na baadhi ya watu wenye tamaa kununua makazi hayo kutokana na usiri mkubwa uliotawala katika mauzo hayo.

 

Wizara ya Ardhi 

Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeweka wazi kwamba eneo hilo lenye mgogoro katika viwanja namba 75-78, kitalu 45B limetengwa kwa ajili ya makazi pekee na matumizi yake hayajabadilishwa.

“Kwa barua hii ninakutaarifu kuwa kwa mujibu wa mchoro wa Mipangomiji namba 1/492/467, matumizi ya viwanja hivyo ni makazi pekee kifungu (a) na (c) kwa mujibu wa kanuni za Upangaji Matumizi ya Ardhi za mwaka 1960 kama zilivyorekebishwa mwaka 1993,” imeeleza sehemu ya barua hiyo kwa Roezer ya Mei 9, 2016 yenye kumbukumbu namba CA.87/171/02/148.

Hadi mwezi uliopita Shirika la Bima limekuwa likilipa kodi za pango la ardhi katika makazi hayo yaliyouzwa kwa BAKITA.

 

Uongozi wa Bima

Uongozi wa Shirika la Bima umetetea uamuzi wake wa kuuza makazi kwa madai kwamba wametekeleza maagizo ya Baraza la Mawazi yaliyotolewa mwaka 2009.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Bima la Taifa, Sam Kamanga, anasema shirika lilifuata utaratibu katika mauzo hayo.