January-MakambaWakazi wa kata za Boko na Bunju jijini Dar es Salaam ambao wamekilalamikia kiwanda cha Saruji cha Twiga Cement (Wazo) kwa kuharibu mazingira wamewalalamikia Mawaziri wa Wizara ya Muungano na Mazingira kwa kushindwa kuchukua hatua kwa kiwanda hicho.

Pamoja na Mawaziri hao kufikishiwa taarifa za uharibifu wa mazingira unaosababishwa na kiwanda hicho ambao umeathiri makazi na uharibifu wa mali za wakazi wa kata hizo, hali wanayoitafsiri kama kushindwa kuchukua hatua ni dalili za kumwogopa mwekezaji.

Toleo lililopita JAMHURI liliandika habari za kiwanda hicho kuharibu mazingira na kusababisha baadhi ya nyumba na mali za wakazi hao kusombwa na maji yaliyokuwa yakitoka kwenye mabwawa ya maji kiwandani hapo.

Baada ya kuripotiwa kwa habari hizo, JAMHURI limeshuhudia kiwanda hicho cha Wazo kikifukia mashimo makubwa na mabwawa matatu yaliyokuwa yakilalamikiwa na wananchi kwamba yanapeleka maji katika makazi yao hasa kipindi cha masika.

Kazi ya ufukiaji wa mashimo makubwa na makorongo yaliyosababishwa na maporomoko ya maji yaliyokuwa yakitoka katika mabwawa hayo yaliyofukiwa bado inaendelea huku wananchi hao wakieleza ni jitihada za kuficha ushahidi baada ya baadhi yao kutapeliwa fidia walizoahidiwa kulipwa.

“Baada ya kuripotiwa habari katika gazeti lenu (JAMHURI) ndio wameanza kufukia mashimo haya makubwa kwa lengo la kupoteza ushahidi na fidia zetu tusilipwe kama Wazo walivyotuahidi baada ya nyumba zetu kusombwa na maji,” anasema Alicheraus Mwesiga mkazi wa Boko CCM ambaye nyumba yake iko hatarini kuanguka.

Mwesiga nyumba yake imezungukwa na shimo kubwa lililotokana na maji yanayotoka katika Kiwanda hicho cha saruji na malalamiko yake aliyafikisha katika Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Wizara ya Muungano na Mazingira na Chama Cha Wanasheria Watetezi wa Mazingira (LEAT) bila mafanikio.

Anasema kiwanda hicho cha Saruji kimewaathiri sana na sasa wanaishi maisha magumu yaliyojaa mashaka kutokana nyumba zao kuzungukwa na makorongo makubwa yaliyosababishwa na maporomoko ya maji.

Aprili 2, 2013 walimwandikia barua Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wanasheria wa Mazingira (LEAT) ambako walipewa msaada wa kisheria dhidi ya kiwanda hicho cha saruji kwa kushindwa kusimamia sheria namba 20 ya mwaka 2004 ya mazingira.

LEAT walipeleka barua za kuwataka wahusika kusimamia sheria vinginevyo watafungua mashtaka dhidi yao Aprili 22, 2013 ikiwa na kumbukumbu namba LEAT/BOKO/NEMC/1 lakini waliendelea kuachilia maji hayo.

Baraza la Usimamizi wa Mazingira (NEMC)  kwa upande wao walijibu barua hiyo Juni 22,2013 yenye kumbukumbu namba NEMC/508/1/VOL.11/32 ikieleza tatizo la mfumo mbovu wa miundombinu ya kiwanda hicho kwamba ni chanzo cha uharibifu huo wa mazingira pia hakikuwa na cheti cha tathmini ya athari za mazingira na kutakiwa na Baraza hilo kufanya uhakiki wa mazingira yake.

Pamoja na maagizo hayo ya NEMC, kiwanda kimeshindwa kufanya marekebisho na kusababisha wakazi wa Boko CCM, Basihaya, Chasimba, Shule ya Msingi ya Mtambani, Kanisa Katoliki la Boko, Boko ofisi za CCM, Zahanati na maeneo mengine kuathiriwa na mmomonyoko wa ardhi unaotokana na maji hayo.

Kabla ya kuripotiwa kwa habari hiyo, JAMHURI, lilitembelea maeneo yote yanayolalamikiwa na wananchi hao na kushuhudia uharibifu mkubwa wa mazingira unaohatarisha maisha ya watu unaosababishwa na maporomoko hayo ya maji.

Hata hivyo kile kinachotafsiriwa na wakazi wa maeneo hayo kwamba ni kushindwa kuzingatia sheria za utunzaji wa mazingira ama kutowajali wananchi ni uongozi wa kiwanda hicho cha saruji umechimba mfereji wa kupeleka maji mto Nyakasangwe lakini mfereji huo haujajengwa kabisa na siku chache zijazo linaweza kuwa korongo kubwa ndani ya makazi ya watu.

 “Mfereji umechimbwa lakini haujajengwa na hii inadaiwa kuwa ni kazi ya Mhandisi wa kiwanda. Kiwanda kinahatarisha maisha ya watu na vyombo husika vinaona sawa hata kama mamia ya Watanzania watapoteza maisha,” anaeleza Jumanne Hamis mkazi wa Boko.

Waliotapeliwa na kiwanda

Baadhi ya wakazi wa maeneo ya Boko CCM na Basihaya ambao nyumba zao, maduka na mali zingine zimesombwa na maji wanakusudia kufikisha malalamiko yao kwa Rais John Pombe Magufuli baada ya kutowaamini Mawaziri, January Makamba na naibu wake Luhaga Mpina.

Wakazi hao wanasema wamechoshwa na mwenendo wa mawaziri hao kwa kushindwa kuchukua hatua mapema kuzuia uharibifu huo ama ni woga wa kukabiliana na mwekezaji huyo.

“Suala hili ni la muda mrefu lakini tunasikitishwa na viongozi hawa kupuuza madai yetu pamoja na kwamba wote wanazo taarifa hizo mapema. Hata kitendo cha Naibu Waziri kuzuiwa kuingia ndani ya kiwanda hicho cha saruji kufanya ziara yake ya kushitukiza kinaonesha wazi hapa kuna tatizo ambalo kwa kiasi kikubwa limechangiwa na utendaji kazi wa mazoea wa viongozi,” anasema Bakari Hassan mkazi wa Boko.

Joseph Mabwati mkazi wa Boko ambaye nyumba yake ilisombwa na maji yaliyotoka katika mabwawa ya kiwanda hicho yaliyokuwa yamekatika kutokana na wingi wa maji Machi 2014 na kutapeliwa fidia aliyoahidiwa na uongozi wa kiwanda.

Mabwati anasema walichobaini ni kwamba hakuna kiongozi yeyote anayeweza kuwasaidia kupata haki zao zaidi ya Rais Magufuli kwani wote waliofikishiwa taarifa hizo wameshindwa.

MPINALUHAGATaarifa za uharibifu wa nyumba hiyo pamoja na mali zilizokuwemo zilitakiwa kuwasilishwa kwa siri kati yake na uongozi wa kiwanda kwa lengo la kuwafanya wananchi wengine walioathirika na maporomoko hayo ya maji wasielewe na wao kuanza kudai fidia.

Pamoja na siri hiyo taarifa yake aliyoifikisha kiwandani hapo ikiwa na picha zinazoonesha uharibifu uliotokea katika nyumba yake,alielezwa Gerald Magoda, ambaye ni afisa mazingira wa kiwanda hicho, kwamba kiwanda hakiwezi kumlipa fidia yake.

Akizungumza na JAMHURI, Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais- Muungano na Mazingira Luhaga Mpina anasema, malalamiko hayo ya wananchi walioathirika na uharibifu wa mazingira kutoka kiwanda cha Wazo ameyapata na kuwaagiza NEMC kufanya ukaguzi.

Anasema pamoja na kuwaagiza NEMC yeye mwenyewe amefanya jitihada za kufuatilia suala hilo na mwezi uliopita alifika kiwandani hapo lakini hakuruhusiwa kuingia ndani kwa madai yaliyotolewa na uongozi  kwamba walikuwa wamepuliza dawa ya kuua vijidudu katika eneo lote la kiwanda.

Magoda kwa kushindwa kujibu maswali ya mwandishi wa JAMHURI aliyoulizwa alituma ujumbe mfupi wa maneno (sms) yenye maelezo haya “unadhani sisi ni wajinga kwa kiwango hicho?”

Please follow and like us:
Pin Share