Mikataba ya kuchimba dhahabu hapa nchini ilianza kusainiwa na Serikali ya Awamu ya Tatu chini ya Mzee Benjamin William Mkapa.

Mikataba hii imesainiwa katika taratibu na mazingira ya kifisadi, kwa vile kwanza muda wa mikataba ni miaka 99 na mrahaba wa asilimia tatu (3%). Mikataba ya aina hii haipo popote duniani zaidi ya hapa Tanzania!

 

Najiuliza Mzee Mkapa alifikiria nini kusaini mikataba ya asilimia tatu tena kwa kipindi cha miaka 99 wakati alijua kwamba yeye amechaguliwa kwa kipindi cha miaka 10 tu! Je, alijiona amepata wawekezaji wajinga sana kiasi kwamba wamekubali kutoa asilimia tatu hivyo aliona akiwaachia hawawezi kupatikana tena?

 

Ndiyo maana akaona madhali wamekubali kusaini mikataba basi asiwape nafasi bali awakandamize kwa kuwapa mikataba ya miaka 99? Ni kwanini Mkapa asingelisaini mikataba hata ya asilimia 0.1 lakini iwe mikataba wa miaka 10 tu! Tukiachana na mrahaba, migodi yetu ya dhahabu inafanyiwa hujuma ambazo huwezi kuamini kama nchi hii kweli ina wenyewe, na hata kama wapo wenyewe basi watakuwa wameshakufa!

 

Nasema hivyo kwani kulingana na taratibu za uchimbaji wa madini duniani, na katika nchi kama Afrika Kusini; mgodi wa madini wowote ni lazima uajiri wafanyakazi ambao hutekeleza majukumu mbalimbali katika mgodi husika kulingana elimu au ujuzi walionao.

 

Wafanyakazi wanapata mishahara na kutunza familia zao. Wanasomesha watoto, matibabu, kuwalisha na kuwavalisha. Serikali yoyote makini lazima ihakikishe inalinda ajira za wananchi wake kwa kuhakikisha kwamba umri wa mgodi unadumu muda mrefu kadri inavyowezekana, ili uendelee kutoa ajira kwa wafanyikazi waliopo kwenye mgodi huo na wapya wanaoajiriwa kila mwaka.

 

Hii inawezekana tu kwa kuhakikisha kwamba serikali inawadhibiti hao wanaoitwa wawekezaji, wasivuke viwango vya uchimbaji vilivyowekwa na taratibu za kimataifa za uchimbaji madini. Nasema hivyo kwa vile machimbo yetu ya dhahabu yamekuwa yakihujumiwa na hawa wanaoitwa wawekezaji, kwani wanachimba madini kwa fujo na kumaliza madini ardhini haraka kama vile wametaarifiwa kwamba wenyewe wamelala wataamka si muda mrefu na kuwafukuza.

 

Udongo unaochimbwa kwa siku moja kwenye machimbo yetu ya kule Geita na Bulyankulu, ni sawa na udongo unaochimbwa kwa mwezi mmoja kwenye machimbo ya Afrika Kusini au Ghana. Hii inaonesha kwamba tunafupisha maisha (life span) ya migodi yetu kwa mara thelathini. Ina maana kama mgodi ungedumu kwa miaka 90 basi inabidi mgodi huo udumu kwa miaka mitatu tu!

 

Hivi dhahabu ikiisha haraka kiasi hicho wafanyakazi wanaotegemea mgodi huo watakwenda kufanya kazi wapi au wataishi vipi wakati kazi itakuwa imekwisha? Je, wanaotegemewa na familia zao itakuwaje?

 

Mwaka jana nilikutana na ‘Mine Engineer’ mmoja kutoka Ghana aliyekuja hapa nchini kwa muda mfupi kwa shughuli hizo hizo za madini. Hata yeye alikuwa anashangaa kiasi cha udongo kinachochimbwa kwa siku kuwa ni kikubwa mno kiasi kwamba kinahatarisha maisha ya Watanzania wanaotegemea sekta ya dhahabu.

 

Hii inaonesha wazi kwamba serikali haina mpango mkakati wa kulinda ajira za wafanyakazi kwa muda mrefu hapa nchini. Viongozi, wanasiasa, wabunge na wanaharakati wamekuwa wakipiga kelele kuhusu tatizo la ajira nchini; lakini hawana mbinu za kulinda ajira zilizopo.

 

Wahubiri na mawakili wa bomu la ajira kama akina Edward Lowassa, wanashindwa nini kutumia muda wao kwenda kwenye migodi yetu na kuzihimiza kampuni zinazochimba madini zipunguze kiwango cha udongo kinachochimbwa kwa siku? Je, kasi hii ya uchimbaji inatuelekeza wapi?


Usikose sehemu ya pili ya makala haya.

Mwandishi wa makala haya, Dk. Noordin Jella (Ph.D. in Economics), ni Mhadhiri mstaafu wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Chuo Kikuu Huria, Chuo Kikuu cha Kampala (KIU) na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Kwa sasa ni Mwandishi wa Kujitegemea na Mchambuzi wa masuala ya Siasa. Anapatikana kwa

Email: norjella@yahoo.com

Simu: +255 782 000 131


3210 Total Views 15 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!