Mwanamuziki asiyependa kujenga jina lake kwa kiki

Kassim Mganga ni msanii wa muziki wa kizazi kipya ambaye amekuwa kivutio kikubwa kwa wapenzi wa muziki wa mwambao, ambapo hivi sasa anatamba katika video yake ya Somo. Wimbo huo una maneno ya kumfunda mwali na kumuonyesha jinsi ya kuishi katika ndoa.

Mganga anaonekana katika video hiyo akiimba kwa kupokezana na wanamuziki wa bendi ya Kilimanjaro; Nyota Waziri na Waziri Ali.

Kassim ni mmoja wa vijana walioingiza aina tofauti ya ladha kwenye muziki wa Bongo Fleva. Ni mwenye nidhamu kwenye muziki na katika maisha ya kawaida.

Aidha, amekuwa haamini kabisa kwamba ili kuwa nyota katika muziki ni lazima utengeneze kashfa itakayofanya jina lako liwe midomoni mwa watu kwa angalau siku mbili, tatu.

Kassim alizaliwa mkoani Tanga katika familia ya watoto wa tatu. Alipata elimu mkoani humo hadi pale baba yake alipohamia jijini Dar es Salaam. Kwa bahati nzuri alipozaliwa na kupata ufahamu, aliwakuta wazazi wake wote wakiwa wanamuziki.

Baba yake, Hemed Salim Mganga, alikuwa mwanamuziki katika bendi ya Legho Stars na mama alikuwa mwimbaji katika vikundi vya Bandari Modern Taarab ya mkoani Tanga na baadaye Coast Modern Taarab.

Kassim alipelekwa kusoma katika Shule ya Msingi Lumumba, akafaulu na kujiunga na Shule ya Sekondari Dar es Salaam, lakini hakuweza kufaulu kwenda kidato cha tano.

Wakati akiwa sekondari, alikuwa akisoma huku akifanya kazi ya muziki.

Aliamua kujiunga katika Chuo cha Elimu ya Biashara jijini Dar es Salaam (CBE), lakini hakumaliza mafunzo.

Baada ya kuacha chuo aliingia mitaani rasmi kupambana na maisha baada ya wazazi wake kuachana.

Huko mitaani alikutana na marafiki wakamshawishi kujifunza kazi ya Clearing and Forwarding.

Kampuni moja ilimuona na kumpa ajira mwaka 2005 hadi 2007, alifanya kazi hiyo kwa muda wa miaka mitatu. Katika kipindi hicho ndipo alipokutana na DJ Muli B.

Baada ya kutoa wimbo wa ‘Haiwezekani’ katika studio ya Saidi Komorie, ndipo aliacha kazi ya Clearing and Forwarding rasmi mwaka 2007 na kujikita katika muziki.

Mwandishi anapatikana kwa simu namba: 0713331200, 0784331200, 0736331200 na 0767331200

By Jamhuri