Bifu kati ya wanamuziki mahiri nchini, Diamond Platnumz na Ali Kiba ni jambo linaloeleweka wazi. Kuelekea mwishoni mwa mwaka jana wawili hao walizidisha msigano wao baada ya Diamond kumwalika Kiba kushiriki kwenye tamasha la Wasafi – Wasafi Festival.

Lakini Kiba akamtolea nje na kutoa jibu ambalo lilionyesha dhahiri kuwa bifu kati ya wawili hao bado lipo.

Katika jibu lake, Kiba alifananisha mwaliko wa Diamond na michezo ya kitoto.

Lakini hayo ni ya mwaka jana. Habari ya mjini hivi sasa ni hatua ya mdogo wake Ali Kiba ajulikanaye kama Issa Azam, ambaye anaonekana amemgeuka kaka yake na kumkingia kifua Diamond.

Akizungumza na radio moja jijini Dar es Salaam hivi karibuni, Issa alibainisha kuwa anampenda zaidi Diamond kuliko kaka yake.

Kauli hiyo ilimsababishia makubwa, kwani Ali Kiba aliamua kumtolea nje, akisema kwa muda mrefu hana uhusiano wa karibu na mdogo wake huyo.

Mashabiki wa Ali Kiba pia wamemshambulia Issa na kumsababishia majeraha mwilini.

“Linapokuja suala la kuchagua timu huwa ninaamua kulingana na vile moyo wangu unaniambia. Mimi ni mtu wa watu, na watu wengi watanifuata, jambo ambalo limewakasirisha mashabiki wa Kiba. Diamond alisikia kuwa nimejeruhiwa na mashabiki wa Ali Kiba akanisaidia,” anasema Issa.

Uamuzi wake huo, pamoja na kuwa ulimkasirisha kaka yake na mashabiki wake, lakini umemsogeza karibu zaidi na Diamond, kwani wawili hao wameonekana wakipozi kwa picha.

Diamond Platnumz pia alilipa gharama za Issa kuhudhuria onyesho la Ne-Yo wakati mwanamuziki huyo wa Marekani alipozuru Tanzania.

“Kilichonishitua sana ni baada ya Diamond kunipigia simu. Ilikuwa ni mara yake ya kwanza kunipigia, sijui alipata wapi namba yangu na akaniomba nimpelekee kitambulisho changu ili anisaidie kwenda kumuona Ne-Yo kwenye onyesho lake. Mungu ambariki,” anabainisha Issa.

1661 Total Views 3 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!