Serikali imewaomba wabunge waiunge mkono kwenye azma yake ya kuhakikisha utaratibu mpya wa kutoa ardhi kwa wawekezaji kwa misingi ya kugawana hisa kwenye Halmashauri za Vijiji unatekelezwa.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, amesema utaratibu wa sasa wa kupewa gawio lisilozingatia misingi ya kichumi, kwa mfano, wawekezaji kutoa zawadi ndogondogo kama visima vya maji, madarasa, barabara za vumbi na zahanati, lazima ukomeshwe.

 

Amezungumzia uanzishwaji wa Hazina ya Ardhi (Land Bank) na kusema Wizara hiyo kwa kushirikiana na wadau wengine inaendelea kuchukua hatua za kuanzisha Hazina ya Ardhi na Mfuko wa Fidia ya Ardhi.

 

“Taratibu zitakapokamilika tutawasilisha muswada wa sheria ya kuanzisha rasmi vyombo hivyo,” amesema Waziri Tibaijuka.

 

Kuhusu Mabaraza ya Ardhi ya Wilaya, Profesa Tibaijuka amesema kwamba Mabaraza ya Nzega, Kilosa na Manyoni yameanza kufanya kazi.

 

“Aidha, Mabaraza ya Ardhi ya Wilaya katika Wilaya za Ngorongoro, Tunduru, Mpanda, Muleba, Karagwe, Kyela na Ngara yako hatua za mwisho kuundwa.  Taratibu za ukarabati wa majengo hayo na ununuzi wa samani na vitendea kazi zinaendelea ili Mabaraza haya yaweze kuanza kufanya kazi katika mwaka 2013/2014.

 

“Wizara yangu inakusudia kuunda Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya katika wilaya tano; za Kilindi, Mbulu, Kahama, Sengerema na Kasulu kwa lengo la kusogeza huduma ya utatuzi wa migogoro ya ardhi karibu na wananchi,” amesema na kuendelea:

 

“Ninapenda kutumia fursa hii kuwashukuru viongozi wa mikoa na Halmashauri za Wilaya husika ambao wameonesha ushirikiano mzuri wa kuhakikisha kuwa Mabaraza haya yanaundwa kwa kutoa majengo yatakayotumika kama ofisi.”

 

Mashauri ya ardhi

Waziri Tibaijuka amesema hadi Juni, 2012 kulikuwa na mashauri 17,654 na kuanzia Julai, 2012 mashauri 12,074 yalifunguliwa.

 

“Katika mwaka wa fedha 2012/2013 jumla ya mashauri 9,831 yameamuriwa na mashauri 19,897 yaliyobaki na yatakayofunguliwa yataendelea kusikilizwa katika mwaka 2013/2014,” amesema.

 

Kwa mujibu wa Waziri huyo,  kuongezeka kwa mashauri hayo kunachangiwa na utendaji hafifu usioridhisha wa Mabaraza ya Ardhi ya Vijiji na Mabaraza ya Kata.

 

“Natoa wito kwa Halmashauri zote kuimarisha Mabaraza ya Ardhi ya Vijiji na Mabaraza ya Kata kwa kuyajengea uwezo ili yaweze kutatua migogoro kwa ufanisi na kwa haraka na hivyo, kupunguza msongamano wa mashauri katika Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya.

 

“Wizara yangu imeshughulikia malalamiko ya wananchi dhidi ya utendaji wa kazi usioridhisha wa baadhi ya Wenyeviti wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya kwa kuchukua hatua mbalimbali kulingana na sheria na kanuni. Wizara inaendelea kufuatilia utendaji wa kazi wa Wenyeviti ili kuhakikisha kuwa wanajiepusha na matendo ambayo ni kinyume cha Sheria na Maadili ya kazi zao,” amesema Profesa Tibaijuka katika hotuba yake ya bajeti bungeni, juzi.

 

By Jamhuri