Leo nipo Makao Makuu ya nchi, Dodoma. Nimekuja kuendeleza uenezaji wa ujumbe wa haki ya kupata habari. Tumepata fursa ya kuendesha semina kwa wabunge na waandishi wa habari juu ya umuhimu wa wabunge kufanya kazi pamoja na vyombo vya habari. Suala la ‘Bunge Live’ limeibuka kwa nguvu katika semina hii. Imeandaliwa na Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika (MISA-TAN).

Nikiacha hoja hii ya mafunzo ya haki ya kupata taarifa tuliyoyaendesha hapa, nchi imekuwa na matukio kadhaa. Matokeo ya mtihani wa kidato cha nne yameacha maswali mengi. Jijini Dar es Salaam, shule zake ufaulu umepungua kwa kiasi kikubwa. Shule sita kati ya 10 za mwisho zimetokea Dar es Salaam. Hii imezaa maswali mengi na naamini Serikali itafanya uchunguzi wa kina kufahamu nini kilitokea.

Tayari majibu yameanza kujitokeza. Kuwa baadhi ya shule za kata, zinazomilikiwa na Serikali ni sawa na vituo vya malezi na si shule. Shule hazina walimu wala vifaa vya kufundishia. Wadau wanataka Serikali iongeze nguvu kwa kutoa fedha stahiki kwa ajili ya kuhakikisha kila mtoto anayeingia darasani apate fursa ya kufundishwa na si kugeuza shule vituo vya kulelea watoto.

Sitanii, nimesema matukio yamekuwa mengi. Sitanii ya leo itagusa matukio mengi pia kwa maslahi ya Taifa. Treni ya kasi ya kutoka Kigoma kuja Dar es Salaam imepata ajali. Mabehewa sita yametoka kwenye reli na kuanguka. Ingawa watu hawakufariki, ila najiuliza nini kilichojiri. Yapo maneno kuwa mabehewa haya hayana viwango. Ni matumaini yangu kuwa Serikali itafanya uchunguzi wa kina kubaini nini kilichotokea.

Ni jambo jema kuwa wiki hii Serikali imeingia mkataba wa kujenga reli ya umeme kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza. Kwa awamu ya kwanza kampuni za kutoka Ureno na Uturuki, zitajenga wastani wa kilometa 300 kutoka Dar es Salaam-Morogoro. Itakuwa na kasi ya kilomita 160 kwa saa. Napendekeza Serikali iangalie uwezekano wa kuongeza kasi hii, maana tayari China treni yao ya umeme inakwenda hadi kasi ya kilomita 540 kwa saa.

Kimsingi, Tanzania kwa ukubwa wake inastahili reli ya umeme. Nchi hii kutoka ncha moja hadi nyingine ni zaidi ya kilomita 1,800. Treni ikitoka Dar es Salaam hadi Kigoma kwa saa angalau 8, ni faraja kwa kuanzia. Hii itashusha gharama ya usafiri na biashara zitafanyika kwa kasi kubwa kuliko hali ilivyo sasa. Mabasi na malori yanayohatarisha maisha ya wananchi barabarani yatapungua.

Sitanii, Februari 2, 2017 limetokea tukio la kishujaa. Rais John Magufuli akiwa mgeni rasmi katika Siku ya Sheria, alikubali kumpokea mama mjane Swabaha Mohamed Shosi. Mama huyu alikuwa anadhulumiwa nyumba na mali alizochuma na mume wake. Rais ameagiza mama huyu apewe ulinzi. Tayari wapambe wameanza kumzonga huyu mama na wanasambaza ujumbe wa kuonesha huyu mama ni tapeli. Naomba tuwachunguze hawa wanaosambaza ujumbe huu.

Watu wengi wanapoteza haki zao katika mazingira ya kutatanisha. Zipo hati za viwanja nyingi zinazopandikizwa juu ya hati. Watu wanajua jinsi wanavyofanya. Wananchi wanapokwa viwanja, ardhi na uharamia wa kutisha. Napenda kuamini Serikali ya Rais Magufuli italifanyia kazi hili kwa kina. Watu wengi wanapoteza haki usipime. Mfumo wa kutoa haki una mafinyufinyu mengi nchi hii.

Suala la mwisho, na ambalo limebeba kichwa cha makala ya leo ni hatua ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, kutangaza majina ya wauzaji na wasafirishaji wa dawa za kulevya, maarufu kama ‘unga’ hapa nchini. Hakika nimeona baadhi ya watu wakimbeza Makonda kwa hatua hii, ila nadhani hatuitendei haki nafsi yetu.

Sitanii, ilihitaji ujasiri wa hali ya juu kutangaza majina ya wauza ‘unga’. Nimesikia baadhi ya watu wakisema ametaja dagaa, mapapa na ‘marafiki’ zake amewaacha. Najiuliza kama kuna mtu anawafahamu hao mapapa kwa nini asiwataje? Kimsingi Makonda ameonesha ujasiri wa hali ya juu. Sisi Gazeti la JAMHURI tumeandika mno mambo haya, ila hatukupata kiongozi yeyote kupata ujasiri wa kutuunga mkono kwa kiwango haki.

Binafsi nasema ikiwa kuna mtu anayo majina ya nyongeza, basi ayataje badala ya kumnyamba Makonda. Naamini alichokifanya ni jambo kubwa linalostahili kupongezwa na kumtia moyo kwani tukiendelea kuonesha kuwa hajafanya chochote mwisho wa siku tutawakatisha tamaa viongozi kupambana na maovu nchini. Mungu ibariki Tanzania.

By Jamhuri