Sheria ya Udhibiti wa Uzito wa Magari ambayo ni sheria ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki tumeiridhia na imeshaanza kutumika.

Maelezo ya wakubwa ni kwamba sheria hii inalenga kupunguza uzito wa shehena inayopakiwa kwenye malori, lengo kuu likiwa ni kulinda barabara zetu. Hii ndiyo sababu kuu kati ya sababu zote zilizowashawishi viongozi wetu kutunga sheria hii.

Sheria ilipaswa ianze kutumika Januari, mwaka huu. Ikasogezwa mbele kwa kile kilichoelezwa na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwamba ni kuwapa wadau muda wa kuifahamu vema, pia kufanya maandalizi ya kuipokea na kuanza kuitumia.

Mpango wowote wa kulinda barabara zetu ni mpango mzuri. Fedha za walipa kodi zinatumika mabilioni kwa mabilioni kwa ajili ya kujenga na kukarabati barabara zetu. Hali hii imesababishwa na ongezeko la usafirishaji wa kutumia malori. Ndiyo maana hatuna budi kuunga mkono juhudi zozote za uboreshaji wa miundombinu ya reli na majini.

Chanjo ya hakika ya kuzilinda barabara zetu ni kuwa na reli madhubuti na za uhakika kwa sehemu kubwa ya nchi yetu. Gharama za malori haziko kwenye uharibifu wa barabara pekee, bali hata kwenye uchumi wa watu wa kawaida ambao hulazimika kukamuliwa fedha nyingi ili kufidia gharama za usafirishaji.

Kwa hiyo mpango wa kudhibiti uzito wa shehena si jambo baya. Shaka ninayopata kwenye sheria hii ni athari tutakazopata kama nchi kwenye uchumi wetu. Nitajaribu kueleza kwa ufupi.

Miaka mitatu iliyopita niliandika makala ndefu mno kwenye matoleo kadhaa ya gazeti hili kuhusu ‘Kupungua kwa Shehena katika Bandari ya Dar es Salaam’.

Kwa kutumia taarifa za utafiti, niliainisha sababu kadhaa za kupungua kwa mizigo. Kati ya sababu hizo niligusia sheria kali za matumizi ya barabara nchini. Kwa mfano, kutoruhusu matumizi ya magari makubwa ya inter-links. Nchi jirani za Kusini mwa Afrika ikiwamo Zambia zinaruhusu matumizi ya magari hayo, hivyo kutoa wigo mpana kwa mteja kusafirisha mizigo yake kupitia katika bandari nyingine ambazo zinaruhusu magari ya aina zote.

Sababu nyingine kwenye suala hili la barabara ni udhibiti wa kupindukia na kuwapo kwa vituo vingi vya ukaguzi – mizani na polisi. Hali hii huwachelewesha wateja na kuwasababishia gharama kubwa za usafirishaji kupitia Bandari ya Dar es Salaam.

Nyingine ni utitiri wa ‘Regulatory agencies’, ambao huchelewesha uondoshaji wa mizigo bandarini na kuongeza gharama kwa wateja.

Lakini moja kubwa na hatari ni kuongezeka kwa ushindani wa kibiashara ambako mgawo wa shehena (traffic share) kupitia Bandari ya Dar es Salaam umekuwa ukipungua ikilinganishwa na mgawo katika Bandari ya Mombasa.

Ndugu zangu, tumekuwa tukisikia kuundwa kwa ‘vikosi kazi’ vya kila aina, lakini sina kumbukumbu za kusikia kuundwa kwa kikosi kazi cha intelijensia ya uchumi. Hata kama kipo, basi inawezekana, ama kimeshindwa kazi, au hakina kazi ya kufanya.

Sheria hii mpya ya uzito wa magari kwa nchi za Afrika Mashariki ni janga kubwa kwa uchumi wa Tanzania. Ni sheria inayotaka kuifanya Bandari ya Dar es Salaam na ile ya Tanga zikose mizigo mizito inayopelekwa katika mataifa jirani. Kimsingi, sheria hii ni maumivu makubwa mno kwa Tanzania. Sheria hii haiwezi kuiathiri Kenya ambao ndio washindani wetu wakuu.

Kenya wana soko la uhakika la mataifa ya DRC, Rwanda, Uganda na Sudan Kusini. Haya ni masoko yake ambayo kwa namna yoyote hayawezi kuikwepa Kenya hata kama kutatungwa sheria ya kusafirisha shehena yenye uzito wa tani 5 pekee!

Kijiografia Tanzania iko pazuri, lakini pia iko pabaya. Tunapeleka shehena Uganda, Rwanda, DRC, Burundi, Zambia, Malawi na hata Zimbabwe. Kusini mwa DRC, Zambia, Malawi na kidogo Zimbabwe, tayari wana mbadala. Kuna bandari za Beira (Msumbiji), Durban (Afrika Kusini) na Walvis Bay nchini Namibia.

Sheria hii ya Afrika Mashariki inawafanya DRC, Malawi na Zambia wageukie Beira, Durban na Walvis Bay. Ukiacha sababu nyingine mbalimbali, bandari hizo hata kwa umbali haziko mbali na mataifa hayo. Kero za ukaguzi na vikwazo barabarani ni ndogo mno.

Nini kinachokuja? Kinachokuja kwa sheria hii mpya ni kuwakimbiza wateja kutoka mataifa hayo. Wakati sisi tukikimbiwa, Kenya wao wataendelea kunufaika kwa shehena za Rwanda, Uganda na Sudan Kusini kwa sababu nchi hizo zitake zisitake, lazima zitumie Bandari ya Mombasa. Hazina mbadala (ukiacha usafiri wa ndege). Lakini kwa Tanzania wale wanaotumia Bandari ya Dar es Salaam au Tanga wana mbadala kwa bandari nilizozitaja za Beira, Durban na Walvis Bay. Kwenye sakata hili wenye kupata maumivu ni Tanzania tu. Ndiyo maana ukitazama vema sheria iliyotungwa kulinda barabara unaona kabisa mlengwa mkuu wa kuyafaidi haya maumivu ni Tanzania.

Ndiyo maana najiuliza, ilikuwaje wabunge wetu kwenye Bunge la Afrika Mashariki wakapitisha sheria hii hatari? Walijua athari zake? Je, hawakuwa na mbadala wa namna nyingine ya kulinda barabara zetu hasa kwa kuangalia aina na idadi ya matairi ya malori?

Nitoe tu mwito kwa mamlaka zinazohusika kulitazama jambo hili upya. Kenya ni wataalamu sana wa kutuingiza ‘mkenge’. Tulipoazimia kuweka VAT kwenye shehena wao wakatuacha kwenye mataa. Wakatuacha tuumie. Tudhibiti uzito wa magari, lakini tuwe makini kuhusu mbinu iliyo nyuma ya sheria hii. Tutakimbiwa, mwishowe tutaumia kiuchumi.

By Jamhuri