Rudi na nyumba ni maneno ya Kiswahili na kila moja lina maana na umuhimu wake katika matumizi. Unapoyatumia maneno haya katika matukio yako ni dhahiri shahiri una nia ya kufanya jambo ambalo kwako na kwa wenzako lina faida. Ni maneno yenye maana kubwa ya ustaarabu na uungwana mbele ya jamii.

Neno rudi lina maana nne. Lakini leo nitazungumzia maana mbili tu. Rejea na rekebisha. Kadhalika neno nyumba lina maana kuu mbili, jengo la kuishi na mke wa mtu. Katika fasihi hii nitazungumzia jengo la kuishi, kwa ufafanuzi wa familia au kundi la watu katika umoja wao ( klabu, chama, taasisi n. k.)

Wiki tatu zilizopita, maneno haya yalitumiwa na kiongozi maarufu wa kisiasa na kiserikali hapa nchini, ambaye alionyesha nia ya kurejea katika makazi yake ya kisiasa, baada ya kujirekebisha kuhusu uamuzi wa kuhama chama kimoja cha siasa na kuhamia chama kingine cha siasa kwa masilahi yake na wanasiasa wenzake. Namzungumzia Edward Lowassa.

Ilikuwa Machi  Mosi, mwaka huu katika hafla fupi iliyofanyika mbele ya viongozi na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), katika Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya chama hicho, Mtaa wa Lumumba, jijini Dar es Salaam, ilishuhudiwa Lowassa akitamka maneno haya: “Narudi nyumbani.”  Kurudi si kosa, ni hiari.

Katika kuzamisha maneno haya masikioni na akilini mwa wanasiasa na Watanzania, katika mkutano wa hadhara Arusha, Edward Lowassa alikaririwa akitamka: “Narudi nyumbani kwa sababu narudi nyumbani.” Hapa ndipo FASIHI ilipopata chambi ya kuzungumzia, narudi nyumbani katika mkondo wa siasa.

Narudi nyumbani ni kauli au tamko lenye maneno mawili yenye kurudiwa. Narudi ni kitendo cha kuonyesha nia. Nyumbani ni kuweka msisitizo wa makazi asili. Tamko hili halihitaji sababu wala  mkasa, lakini linapaswa kueleweka vizuri kisiasa.

Kwa mtazamo wa nje kauli hii ni kama kucheza na akili za watu kwa maana ya mzaha au kejeli. Jambo ambalo si sahihi. Lakini kwa mtazamo wa ndani uliojaa ukweli, falsafa na fasili, siasa ni sayansi. Ndiyo maana wapo watu wanaofurahia na wapo wasiofurahia uamuzi wa Edward Lowassa wa kurudi CCM na kuhama Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Naomba ieleweke,  siasa si ajali,  si  mchezo mchafu na si bla blaa. Ajali, bla blaa na mchezo mchafu ni matokeo ya mwanasiasa mwenyewe katika kuelewa, kufasili, kutetea na kusimamia shughuli za siasa. Wanasiasa uchwara huelea katika vipengele hivi na kufanya mambo ya ajabu au yasiyo na majawabu ya kisiasa.

Siasa ni sayansi yenye mfumo wa kiitikadi unaotumiwa na kikundi cha watu au jamii fulani kuendeshea shughuli zao kwa kutumia nadharia, muono, vipimo, uchunguzi na uthibitisho wa jambo katika hali halisi. Wanasiasa makini hutumia vipengele hivi kujipambanua mbele ya jamii, na kuleta maendeleo ya wananchi katika misingi ya uhuru wa mtu, haki na utawala wa sheria.

Ukitumia siasa ni sayansi, ni nadra kupata shaka katika mazungumzo, matumizi na ulinzi wa shughuli zako. Aghalabu kuepuka kutumia harakati za kisiasa na propaganda za kugawa watu na kufifilisha jitihada za kuleta maendeleo ya wananchi kwa faida ya wote.

Narudi nyumbani ni kauli iliyoshitusha na kuduwaza wanachama wa CCM na wa Chadema pamoja na Watanzania wengi. Kauli iliyopiga mshindo mkubwa na kutikisa nchi. Kipi kilichomsibu Lowassa hata kuamua kukihama Chama Cha Mapinduzi na kuhamia Chadema, mwaka 2015, na baada ya miaka minne (2019) kurudi Chama Cha Mapinduzi?

Je, katika kuhama na kurudi CCM ni uamuzi wa busara au ni msukumo wa kiharakati? Lipi kati ya mawili haya yana sifa ya siasa ya sayansi? Wanasiasa na Watanzania tunapoendelea kuzungumza na kuulizana maswali kama haya tunatafuta nini zaidi ya jibu narudi nyumbani?  Lakini, sina haki ya kukukataza kuuliza wala kusema uwezalo.

Mambo mengi yanayozungumzwa kuhusu mwenendo na itikadi ya vyama hivi ni tofauti katika kuleta maendeleo ya wananchi, ujenzi wa uchumi wa nchi na tabia ya mwanachama wao kisiasa. Maswali na majibu yatolewayo yana ufahamu na uanaharakati wa kisiasa na baadhi yana muono na kanuni za siasa ya sayansi.

‘Narudi nyumbani’ iwe ni kaulimbiu ya kushawishi, kuhamasisha na kufafanua maana sahihi ya kuleta mabadiliko ya kweli, si mabadiliko ya uanaharakati. ‘Kurudi’ ni mabadiliko na kusahau yaliyopita na kujaza yajayo ni mabadiliko. Yanawezekana, tutimize wajibu wetu.

Please follow and like us:
Pin Share