Kwa asili nachukia kuomba bila sababu na nilijengewa tabia hiyo na wazazi waliotumia vyema nguvu zao kujitegemea na kututegemeza.

Ukiacha wasiojiweza wa kule vijijini miaka ile michache baada ya Uhuru na wale wasiokuwa na akili timamu waliokuwa wakisaidiwa pasi na hiyana, hapakuwa na kitu hiki ‘ombaomba’. Nilipokuja kufika mjini wakati nakaribia kuhitimu darasa la saba, nilishangaa kuona watu wazima wamekaa wanaomba pesa na chakula huku wakishirikiana na hata watoto wadogo.

Nilipobahatika kuingia mji mkuu wetu wa kibiashara wa Dar es Salaam, haikuingia akilini watu wengi jinsi ile walikuwa wakifanya nini mitaani mchana, nikaja kugundua baadaye kuwa usiku ilikuwa balaa, hasa maeneo ya Kariakoo na mengine kama hayo. Labda hitimisho la mshangao wangu litakuwa hapa London, ambao kwa hakika ni mji ulio mbele kwa kila namna, kutokana na historia ya nchi yenyewe.

Kumbuka kihistoria Uingereza ndiyo kama baba wa mataifa yote (nimesema kama), maana ameitawala hata Marekani, nchi kubwa kabisa kijiografia, kijeshi na kiuchumi. Lakini nashangaa sasa kuambiwa kwamba mji wake mkuu, jiji lisilo la kawaida la London linaanza kuongezeka ombaomba hao hao waliokuwa wakiitesa Moro, Dar na kwingineko bila kuisahau Dodoma.

London bwana inanukia vizuri mchana, na inaonekana vyema inapopigwa picha za matukio ya jubilei, Olimpiki na mambo mengine, lakini ukiangalia kwenye uvungu wake, salaale! Utatokwa machozi hata kama si ya huzuni. Yaani hata maeneo ya karibu na Bunge (tukufu?) wapo watu wanaojidai ni wasiojiweza, wakiombaomba na kulala vibarazani wametapakaa.

Mitaa ya London sasa inaongoza kwa watu wa aina hiyo. Inaelezwa kuwa pamoja na udogo wake, wanaolala hovyo hovyo barabarani, mitaani na kwenye viambaza visivyo na  vyumba wala vitanda wanazidi 4,000!

Awali walikuwa wanaonekana kwa uchache sana na kwa kujificha, lakini kadiri siku zinavyosonga mbele ambako mtu ungetarajia wapungue kwa maana maendeleo yanaongezeka, ndivyo wanavyozidi kuwa wengi!

Nizitulize nyonyo zenu Wabongo hapa, kwamba kati ya wengi wanaolala barabarani si ‘wa kwetu’. Hapo tumeponea, maana ingekuwa aibu ya mwaka. Wengi wa watu wa jinsi hii ni ama Waingereza wenyewe au watu wa kutoka Ulaya Mashariki, ambao huja huku kama njia ya kuponea maisha kwa kuhemea.

Lakini mtu anaposhindwa kupata mahali pazuri pa kuhemea, anaishia kuingia mitaani na kulala mbele ya viambaza vya watu moja kwa moja. Maana hawaondolewi kwani wameingia kama wakimbizi au wasiojiweza, hawarudishwi makwao maana kunachukuliwa kwamba si salama sana.

Wale wa Uingereza hapa hapa ndiyo sugu maana utawapeleka wapi au utawaambia nini? Wapo kwao na kibaya zaidi ni kwamba huwa walevi – bia, pombe kali na tumbaku inayotumiwa kwa njia mbalimbali ikiwamo sigara. Ukitaka kutafuta jambo lisilo zuri kweli hulikosi, nimeona hadi wanafunzi wasio na kwao wakilala shuleni na walimu wakijaribu kuwapatia mahitaji.

Hao sasa huwa wanasubiri hadi asasi zisizo za kiserikali zifike kuwasaidia, pengine kuwachukua na kuwapeleka kwenye nyumba wanayoendesha kama kuna nafasi. Tukiacha ya wanafunzi, turudi kwa wale ‘wagumu’ au ‘machalii wa mitaani’ ambao wana nguvu lakini hawafanyi kazi – wanaomba tu.

Wiki jana mmoja amenisimamisha nikikatiza kukimbilia kazini na kamkoba kangu, akaniambia nimpe paundi moja tu kwa sababu alikuwa amedondosha yake, na alikuwa amebanwa na kiu ya sigara. Ebo! Mie sikumkopesha, nikamwambia siwezi kumpa pesa ya kwenda kununua kifo, tena nikamjulisha kuwa mie mwenyewe dokta, si wa kufoji bali wa kusotea miaka mingi.

Nilimmalizia kwa kumpasulia kimombo kwamba sigara ni kitu ambacho mwisho mmoja kuna moto na mwisho mwingine kuna mjinga. Inapendeza zaidi nikiweka Kizungu: “a cigarette is something with fire at one end and a fool on the other.”

Wenzake walikuwa wakija kuungana naye, na japo watu wengine walikuwa pia wameshuka kwenye treni za chini kwa chini, ilibidi nitimue mbio baada ya kuwamwagia kile walichoona kuwa ni ‘matusi’. Nikajisemea moyoni ujumbe umefika, potelea mbali, liwalo na liwe.

Sasa tangu mwaka 2010 viongozi wa jiji la London wametoa ahadi ya kuwaondoa ombaomba na hawa watu wanaolala hovyo, sijui tuseme walalahoi, lakini inaelekea hawataweza kabisa. Ukosefu wa kazi na watu kuchanganyikiwa kimaisha vinawaweka vijana wengi katika hali mbaya, na wengine wanaona njia bora zaidi ni hiyo ya kulala mitaani.

Maana ukishafikisha umri wa miaka 18 hapa lazima uwe umeondoka au uondoke kwa wazazi wako, isipokuwa kwa sababu ya msingi, lakini ndiyo utamaduni wao. Sasa upate paundi 300 ya chumba kila mwezi, bado chakula na viburudisha mwili kama pombe na hiyo sigara, ndiyo baadhi labda wanaona wakae na kulala mitaani na wenzao wanaotoka Ulaya Mashariki.

London ni jiji zuri, lakini hata wabunge wanasema kwamba ombaomba kwenye maeneo wanalitia aibu, hasa hao wanaolala mitaani. Wenyewe wanasema sasa wao kama wabunge na serikali wataelewekaje ikiwa picha ya kwenye televisheni au hata ya gazeti itawaonyesha hao watu, halafu watu wa nchi masikini wakajua kwamba hata London watu wamefulia?

Tafakari, ipende nchi yako, ijenge, saidia ndugu zako, hata hapo panaweza kuwa na maisha mazuri kuliko ya mtu anayekaa London, maana London na Dar ni majina tu, wanaofurahia maisha ni mimi na wewe kutegemeana na jinsi tunavyojituma. Alamsiki.

leejoseph2@yahoo.com

1429 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!